Ukisikia neno fisadi unaanza kupata hasira kwa sababu unajua ni jinsi gani ufisadi ulivyo na madhara kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Tunawachukia sana mafisadi na tunapiga kelele nyingi kuwapinga na kuwakemea mafisadi. Bahati mbaya sana hatujui kama sisi wenyewe ni mafisadi wa maisha yetu. Ndio wewe ni fisadi wa maisha yako.

  Mara nyingi tukisikia ufisadi mawazo yetu yanakwenda moja kwa moja kwa wezi na wabadhilifu wa mali za umma. Wizi na ubadhilifu huo unakuwa na madhara makubwa kwa maendeleo na kufanya watu wakose huduma za msingi.

  Je kama kuna mtu anayebadhilifu maisha yake mwenyewe hafai kuitwa fisadi?

  Wengi wetu tuna sehemu mbili za maisha, maisha tunayoyaishi na maisha ambayo bado hatujayaishi ila yapo ndani yetu. Tatizo kubwa ni kwamba maisha unayoishi huyafurahii na maisha yaliyopo ndani yako hujaanza kuyaishi.

maisha2

  Unajiuliza ni maisha gani yaliyopo ndani yako ambayo hujayaishi?

1. Unapokuwa umetulia ama wakati wa usiku unapopumzika ni picha gani ya maisha inakujia kichwani mwako. Ni maisha gani unayotamani ungekuwa nayo, nyumba gani ungeishi, gari gani ungeendesha? Kama kazi unayofanya haikuridhishi ni kazi gani ambayo ungetamani sana uwe unaifanya? Yote haya ni maisha yaliyopo ndani yako ambayo hujaanza kuyaishi.

2. Je umewahi kuanza kitu chochote ukashindwa kumaliza? Umewahi kupanga mipango mizuri ya maisha yako ukashindwa kuitekeleza? Umeshapanga kuyabadili maisha yako na kujiwekea malengo ila bado yanakushinda kutekeleza? Haya ni maisha mazuri yaliyoko ndani yako ambayo hujayaishi na kuyafurahia.

3. Je wewe ni mwandishi usiyeandika, mchoraji usiyechora, mwimbaji usiyeimba au mjasiriamali usiyeanzisha biashara? Kuna vipaji vingi viko ndani yako ambavyo kama ungeweza kuvitumia vizuri maisha yako yangekuwa bora sana.

  Kila mmoja wetu ana maisha yaliyopo ndani yake ambayo hajaanza kuyaishi. Sio kazi ngumu kuanza kuishi maisha hayo. Unachotakiwa kujua ni nini kinakuzuia wewe kuishi maisha yaliyoko ndani yako.

  Kati kati ya maisha unayoishi sasa na maisha yaliyoko ndani yako kuna ukinzani mkubwa. Ukinzani huu unajitokeza kwa njia mbalimbali kukuzuia wewe kuweza kuishi maisha yaliyopo ndani yako.

  Hakuna kinachoweza kuondoa ukinzani huu bila ya wewe mwenyewe kujitambua na kujua kwamba wewe ndio kiongozi mkuu wa maisha yako. (soma; uchaguzi mkuu muhimu kwako)

  Hutaweza kuondoa ukinzani huu kwa kulaumu wengine kwamba ndio waliosababisha wewe kufikia hapo ulipo.

  Utauondoa ukinzani huu kwa kushika hatamu ya maisha yako na kujijua kwamba wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa sana wa kufanya chochote unachofikiria kufanya.(soma; wewe ni wa pekee) 

  Ukianza kuishi maisha yaliyo ndani yako utayafurahia sana maisha. Inawezekana kuyaishi maisha hayo ila kwa sasa hujataka kuyaishi ndio maana nakuambia unayafisadi maisha yako.

maisha

  Umeificha sehemu kubwa na nzuri ya maisha yako, umejidhulumu furaha na mafanikio ambayo ungeyapata kwa kuyaishi maisha mazuri yaliyo ndani yako. Umekuwa fisadi wa maisha yako mwenyewe.

  Acha ufisadi na anza kuishi maisha yako. Utakuwa na furaha zaidi, ubunifu zaidi na mafanikio zaidi.