Watu wengi wanapokuwa wanaanza kufanya kitu kipya huwa wanakuwa na morali wa hali ya juu na shauku kubwa ya kutoa majibu mazuri. Inaweza kuwa ajira, biashara, sanaa au hata elimu. Mtu anaanza akiwa na mategemeo makubwa ya kufanya mambo mazuri na makubwa. Na pia wakati huo wa mwanzo unakuwa na furaha kubwa kwa kufanya unachofanya, na kama alikuwa anasubiri kwa muda mrefu kupata nafasi hiyo furaha huwa maradufu.

   Baada ya muda kupita(miaka mitatu mpaka mitano) mambo yanabadilika kwa kiasi kikubwa sana. Matarajio makubwa mtu aliyokuwa nayo yanayeyuka, uzalishaji unakuwa wa hali ya chini na ubunifu unapotea kabisa. Kama ni kazi inakuwa ni kwenda tu kwa sababu inabidi kwenda na maisha yako umeshayakabidhi kwenye kazi hiyo.

changamoto3

 

  Ni kitu gani kinasababisha mabadiliko haya makubwa?

  Kuna vitu vikuu viwili vinavyosababisha mabadiliko haya makubwa kutokea.

1. Kuzoea unachofanya. Binadamu tuna tabia ya kuzoea kitu kadiri muda unavyokwenda. Na jinsi tunavyozidi kuzoea ndivyo tunavyopunguza thamani na ufanisi.

2. Kukosa hamasa na kushindwa kujihamasisha. Mara nyingi tunapoanza jambo jipya huwa tunakuwa na hamasa kubwa kutoka ndani yetu na kwa wanaokuzunguka. Muda unavyozidi kwenda hakuna anaeonekana kujali tena na wewe mwenyewe unashindwa kujihamasisha.

  Tufanye nini ili kuondokana na tatizo hili la morali wa kufanya jambo kupungua jinsi muda unavyozidi kwenda?

   Dawa nzuri ya tatizo hili ni kujipa changamoto za mara kwa mara. Usikubali kufanya jambo hilo hilo kwa njia hiyo hiyo kila siku miaka nenda miaka rudi. Lazima tu utachoka na morali utaisha na kuona ni jambo la kawaida sana kwako.

changamoto changamoto2

  Jipe changamoto, jipe mitihani midogo midogo na ukiweza kuishinda jipongeze kwa kufanya hivyo. Kwa mfano unaweza kuamua kuongeza kazi unayofanya, kupunguza muda unaotumia kufanya kazi zako, kubuni njia mpya ya kufanya kazi unazofanya na pia kuweka malengo makubwa zaidi ya unavyofanya sasa. Kwa kujipa mitihani na kuweza kuishinda unapata nguvu fulani ndani yako inayokufanya ufurahie unachofanya na uwe na morali mkubwa wa kufanya.

  Badili mazingira ama njia unazifanyia kazi unayofanya. Hakuna kitu kinachochosha kama kuona mazingira yale yale kila siku na kufanya kitu kile kile kwa njia zile zile. Hakikisha kila baada ya muda kuna vitu unavibadilisha katika mazingira yako ya kazi ama njia unazotumia kufanyia kazi unazibadilisha mara kwa mara. Hata kama unafanya kazi ofisini tafuta njia ya kubadili mazingira ya kufanyia kazi ama njia unazofanyia kazi. Kwa mfano unaweza kubadili upande unaokaa, unaweza kubadili picha ama chochote kinachopendezesha ofisi, unaweza kuhama ofisi kabisa kama inawezekana na mengine mengi. Jaribu kufanya mabadiliko haya kidogo na utaona mabadiliko makubwa sana kwenye ufanyaji wako wa kazi.(soma; sio lazima kila siku iwe hivi)

 

  Kama unataka kuwa wapekee na kuwa bora zaidi hakikisha hufanyi kazi yoyote kwa mazoea. Kila unachofanya kifanye kama vile ndio unaanza kufanya kwa mara ya kwanza. Na ili uweze kufanya hivyo ni vizuri kujipa changamoto za mara kwa mara na kujaribu kubadili mazingira ya kazi kila baada ya muda.