Pamoja na ajira kuwa ngumu katika zama hizi bado tunahitaji sana watu wa kuajiriwa. Ajira zimekuwa ngumu kupatikana na pia mazingira ya kazi yamekuwa magumu sana kuliko kipindi cha nyuma kidogo. Pamoja na hayo yote bado ajira zina nafasi kubwa sana kwenye maisha yetu.
Japo kujiajiri ndio limekuwa kimbilio la wengi bado sio wote wanaweza kujiajiri na hata wote wangeweza bado kungetokea upungufu wa watendaji kwenye sekta mbalimbali. Lazima tupate watu wa kutoa huduma mbalimbali kama utawala, afya na elimu.
Kutokana na umuhimu huu wa ajira ni vyema walioko kwenye ajira kujua njia bora za kufanikiwa kwenye ajira.
Kuna kosa moja kubwa linafanywa na watu wengi sana walioko kwenye ajira bila ya kujua kosa hilo ama bila kujua athari za kosa hilo kwenye maisha yao.
Watu wengi walioko kwenye ajira wanafanya kazi chini ya viwango vyao. Na wengi walioajiriwa serikalini wanafanya kazi kwa kiwango kidogo mno. Watu wengi wanatega kazi wakifikiri wanamkomoa mwajiri wao.
Kosa kubwa waajiriwa wengi wanalifanya ni kufikiri kwamba wanamfanyia mtu mwingine kazi. Hakuna kosa kubwa kama kufikiri kwamba kazi unayofanya ni ya mtu mwingine na sio wewe. Ni kweli umeajiriwa na unalipwa kutokana na kazi uliyopangiwa kufanya. Ila kazi unayoifanya unajifanyia wewe na kama ni kuendelea kupitia kazi hiyo wewe ndio mwamuzi.
Kazi yoyote unayofanya haijalishi aliekuajiri ni nani, unajifanyia wewe mwenyewe. Kwa kutojua hili watu wengi wanajikuta hawapati maendeleo ya uhakika kupitia kazi zao.
Kwa mfano watu wengi wanaofanya kazi serikalini, mtu anaweza kwenda kazini na asifanye kazi yoyote ya maana mpaka siku inaisha. Kuna wengine hawaendi kazini kabisa na hata huo muda ambao hawapo kazini hakuna jambo lolote la maana wanalofanya.
Unaweza kuwa unafanya hivyo na ukaona uko sahihi kwa kuwa kazi siyo yako, ila mwisho wa siku wewe ndiye utakayeumia.
Utaumia kwa sababu kwa kutofanya kazi kwa kiwango chako hutoweza kutoa majibu mazuri. Na kutotoa majibu mazuri kunakufanya ushindwe kuwa na kitu cha kujivunia.
Moja ya chanzo kikubwa cha watu kukosa furaha ni kutokuwa wataalamu kwenye jambo wanalofanya. Kutofanya kazi kwa viwango vyako kutakufanya ujione wa chini na usiye na umuhimu wowote. Hali hii ndio inayopelekea kukosa furaha na wakati mwingine msongo wa mawazo.(soma; hii ndio sababu kuu ya wewe kukosa furaha)
Kama upo kwenye ajira hakikisha unafanya kazi zako kwa kiwango kikubwa sana. Unapokuwa unafanya kazi chukulia ile ni kazi yako binafsi hivyo juhudi na ubunifu wako ndivyo vitakavyokusaidia kupata kipato kikubwa zaidi. Kama unaona kazi yako inakupa vikwazo vinavyokusababisha uifanye kwa shingo upande(labda mshahara kidogo) achana nayo na ufanye kazi unayopenda kufanya.
Kumbuka ili ufanikiwe ni lazima upende unachofanya.(soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi) Ukishapenda unachofanya ni dhahiri utakifanya kwa juhudi na ubunifu mkubwa na hii itakuletea maendeleo makubwa kupitia kazi hiyo.