Leo ndio siku ambayo binadamu wa kipekee kuwahi kutokea duniani anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele. Binadamu huyu sio mwingine bali ni Nelson Mandela, raisi wa kwanza mweusi wa afrika kusini.
Kwa siku kumi tokea alipofariki tarehe 5/12/2013 mpaka leo anapokwenda kuzikwa tarehe 15/12/2013 mengi sana yamezungumzwa na kuandikwa juu ya binadamu huyu wa kipekee.
Viongozi mbalimbali wa dunia wamezungumza maneno mengi na mazuri juu ya Mandela. Nilipata muda wa kupitia hotuba ya rais wa marekani Barack Obama na leo nimepata muda wa kupitia hotuba ya raisi wa Tanzania Jakaya Kikwete, hakika Mandela ametuachia kazi kubwa ya kufanya.
Pamoja na kwamba leo Mandela anakwenda kupumzishwa ila bado ataendelea kuishi nasi kila siku. Mandela hajafa bali amepumzika kutoka kwenye maisha haya. Tutaendelea kumtamka na kumuishi kila siku kwenye maisha yetu.(soma; sio wote tunaowazika wamekufa)
Kwa nini Mandela amejizolea sifa kubwa duniani na kuonekana kuwa binadamu wa kipekee?
Pamoja na kuwa kiongozi na mwanaharakati wa kupigania haki za watu weusi, Mandela alionesha uwezo wa kipekee pale alipofungwa jela kwa miaka 27 na bado hakukata tamaa wala kubadili msimamo.
Ni binadamu wachache sana ambao wanaweza kukaa kifungoni miaka ishirini na saba na bado wakaendelea kuwa imara bila ya kutetereka.
Mandela anatufundisha kusimamia kile tunachoamini ni sahihi hata kama tunapitia nyakati ngumu. Anatufundisha kutumia nyakati ngumu kujifunza na kujiendeleza zaidi.
Mandela ameonesha mfano wa uwezo mkubwa ulio ndani ya kila binadamu. Hata wewe unao uwezo mkubwa na wakipekee wa kuweza kufanya mambo makubwa duniani.(soma; wewe ni wa pekee) Mandela ametuachia deni ambalo kila binadamu anatakiwa alitimize ili dunia iwe sehemu salama ya kuishi.
Moja ya misemo ya mandela ni “mara zote kitu kinaonekana hakiwezekani mpaka kitakapofanyika”. Mandela aliweza kufanya hivyo na sisi tunaweza kufanya pia.
Mandela amegusa maisha ya watu wengi sana hivyo kuondoka kwake kimwili ametuacha tukiishi fikra na falsafa zake. Tamani na wewe kugusa maisha ya wengine hata kwa kidogo ili utapoondoka watu waendelee kukuishi. Unaweza kufanya hivyo kwenye maisha yoyote unayoishi.(soma; nini kitatokea utakapokufa?)