Kuna usemi maarufu wa kiswahili unaosema “biashara asubuhi, jioni mahesabu”. Hii ina maana kwamba mwanzo wa jambo lolote ndipo kazi kubwa hufanyika na mwisho wa jambo hilo ndio tathmini hufanyika.
Tumefika ukingoni mwa mwaka 2013 na hivyo huu ndio muda wa kila mmoja wetu kufanya tathmini ya mwaka huu ulikwendaje kwa upande wake.![]()
Kila mmoja wetu aliweka malengo mbalimbali mwaka huu 2013, hata kama hukuyaandika ila kuna vitu ulipanga kuvifanya ndani ya mwaka huu. Itakuwa ni kosa kubwa sana kama utaingia mwaka 2014 na kuweka mipango mingine kama hutofanya tathmini ya mwaka 2013 ulivyokwenda kwa upande wako.
Chukua muda na ukae uyatafakari maisha yako kwa mwaka 2013. Yapitie malengo na mipango uliyojiwekea kwa mwaka huu.
Chukua kalamu na karatasi ama kitabu chako cha kumbukumbu kisha uandike na kujibu maswali yafuatayo. Kumbuka ni muhimu sana kuandika(soma; hivi ndivyo unavyopoteza mawazo yako mazuri). Yajibu maswali haya kwa kuwa muaminifi kwa nafsi yako ili ujue ni wapi ulipofanikiwa na ni wapi ulipokosea.
Katika malengo uliyojiwekea kuna malengo ambayo ulifanikiwa kuyatimiza. Kwa malengo uliyotimiza jiulize na ujibu maswali haya;
1. Je umefanikisha malengo yako kwa kiwango gani?
2. Ni malengo yapi uliyotimiza na ulipata nini baada ya kuyatimiza?
3. Ni changamoto gani ulizokutana nazo katika kutimiza malengo yako?
4. Ni watu gani waliokusaidia ama ulioshirikiana nao kutimiza malengo hayo?
Pia kuna malengo uliyojiwekea kwa mwaka huu na kwa sababu moja au nyingine ukashindwa kuyatimiza. Jiulize na kujibu maswali haya kwa malengo uliyoshindwa kutimiza;
1. Ni malengo yapi uliyoshindwa kuyatimiza mwaka 2013? 2. Ni vikwazo gani vilivyokuzuia kuyatimiza malengo hayo? 3. Ni watu gani waliochangia wewe kushindwa kufikia malengo hayo?
4. Ni vitu gani umekosa kwa kushindwa kuyatimiza malengo uliyojiwekea?
Ukiweza kujibu maswali hayo na kufanyia kazi majibu yako itakuweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kufanikiwa kwenye maisha.
Usijaribu kuweka malengo ya mwaka 2014 kabla hujajiuliza na kujibu maswali hayo. Maana utajikuta unarudia makosa uliyoyafanya 2013 na mwishowe utashindwa kufikia mafanikio unayostahili.
Umefanya nini 2013?