Kama wewe ni mtanzania ina maana nchi pekee ya asili yako ni Tanzania. Unaishi Tanzania, unapata mafanikio Tanzania na hata ukifa utazikwa Tanzania. Hata kama utapata nafasi ya kwenda nje ya Tanzania bado nchi hii itakuwa nyumbani kwako. Hata kama utaamua kubadili uraia na kuwa raia wa nchi nyingine bado kuna ndugu zako wengi wa damu kabisa utawaacha Tanzania. Hivyo Tanzania ni kitu muhimu sana kwetu sisi watanzania.![]()
Je ni kitu gani tunaweza kukifanya kwa nchi hii ambayo ni muhimu sana kwenye maisha yetu? Ni fadhila gani tunazoweza kuzilipa kwa kuishi kwenye nchi hii ambayo imejaliwa vitu vingi?
Kuna vitu vingi tunaweza kuvifanya kwa nchi hii ya kipekee kwetu. Moja ya vitu hivyo ni kuipenda Tanzania. Ni muhimu na lazima kwako kama mtanzania kuipenda Tanzania. Matatizo mengi tunayopitia kama taifa kwa kiasi kikubwa yanatokana na watu kupoteza upendo na nchi yao.
Kuna vitu vingi vinavyoendelea nchini ambavyo vinakatisha wananchi wengi tamaa. Watu wanaopewa nafasi za uongozi wanakuwa wezi na mafisadi, wanaingia mikataba ya kuihujumu nchi na wanaweka sera mbovu zinazoumiza wananchi. Pamoja na matatizo hayo yote bado ni muhimu na lazima kwa kila mtanzania kuipenda Tanzania. Huna sababu yoyote ya kushindwa kufanya hivyo.
Tumefika sehemu mbaya kama taifa kutokana na kila mwananchi kujiangalia yeye binafsi na kukosa mapenzi na nchi yetu. Watu wanafanya mambo ambayo kama yangefanywa miaka 50 iliyopita ni dhahiri leo hii tusingekuwa na nchi katika hali hii. Watu wanaishi kama vile wapo safarini, kama vile haya sio makazi yetu bali tunapita tu. Tunaishi kama vile hili taifa halina vizazi vinavyokuja baada yetu. Ni tatizo kubwa sana kwa taifa.
Kuipenda nchi kunaanza na wewe mwananchi mmoja na baadae kufikia taifa zima. Je wewe unaipenda nchi yako Tanzania? Kabla ya kuwanyooshea vidole viongozi wanaoihujumu nchi hii, wewe umefanya nini cha kuisaidia Tanzania? Je maisha unayoishi kama kila mtanzania angekuwa anayaishi nchi hii itakuwa wapi miaka 10, 20 na hata 50 ijayo?
Watu wengi hawaipendi nchi hii kwa maneno, vitendo hata maisha. Watu hawafanyi kazi, kila mtu anafikiria kupata njia ya mkato ya kufanikiwa. Hii ndio imesababisha watu wengi kujiingiza kwenye wizi na ufisadi.
Kama kweli tunataka maendeleo ya nchi yetu kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo ni lazima tuipende nchi yetu. Ni lazima tufanye kazi kwa juhudi na maarifa na ni lazima kila mmoja wetu awe mlinzi wa nchi yetu. Usiibe kwa sababu viongozi wanaiba, kwa sababu siku na wewe ukiwa kiongozi utaendelea kuiba na utawashawishi wengine kuiba. Na kama kizazi cha uongozi kilichopo kimeharibika kwa wizi na ufisadi basi tuwekeze kwenye kutengeneza vizazi vijavyo vya viongozi watakaokuwa wanaipenda nchi yao.
Sambaza ujumbe huu kwa watu wote wanaokuzunguka na hata kwa familia yako. Kila mtu aipende tanzania.
Maendeleo ya nchi yatapatikana kwa maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja ambayo yatapatikana kwa kufanya kazi halali kwa juhudi na maarifa na kuipenda nchi yake.
Tunakumbushwa hata kwenye wimbo wa taifa kuipenda Tanzania. Nayaweka mashairi ya wimbo wa taifa hapa ili mara kwa mara uwe unajiimbia na uongeze upendo kwa nchi yako.
Tanzania ni yetu sisi na vizazi vijavyo. Tuipende na kuilinda ili wanaokuja nao waifurahie kama sisi tulivyoifurahia.
Tanzania Nakupenda Kwa Moyo Wote
Tanzania Tanzania
Nakupenda kwa moyo wote
Nchi yangu Tanzania
Jina lako ni tamu sana
Nilalapo nakuota wewe
Niamkapo ni heri mama wee
Tanzania Tanzania
Nakupenda kwa moyo wote
Tanzania Tanzania, ninapokwenda safarini,
kutazama maajabu, biashara nayo makazi,
sitaweza kusahau mimi, mambo mema ya kwetu kabisa, Tanzania Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote.
Nchi yangu Tanzania, watu wako ni wema sana,
siasa yako na desturi, vilituletea uhuru,
hatuwezi kusahau sisi, mambo mema ya kwetu kabisaa Tanzania Tanzania, Mola awe nawe daima.