Maisha yamejaa changamoto nyingi na changamoto za maisha ndizo zinafanya maisha yaende. Lakini kutokana na kwamba binadamu tuna asili ya uvivu, imekuwa ni jambo la kawaida sana kutoroka changamoto za maisha yetu wenyewe.
Kuna matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha yetu. Bila kujali umri, rangi, kabila au hadhi kila binadamu kuna matatizo anakutana nayo kwenye maisha yake. Ndivyo maisha yalivyo na hatuwezi kukwepa hilo.
Pia maisha yetu tunakutana na vikwazo mbalimbali kwenye kazi au hata maisha ya kawaida ambayo inatubidi tufikiri sana ili kuweza kutatua.
Kwa kuwa matatizo na changamoto tunazokutana nazo zinahitaji kufikiri kwa kina ili kuzitatua, kumekuwa na tatizo moja kubwa sana kwetu binadamu. Kwa kuwa kufikiri ni kazi inayohitaji utulivu na busara kubwa wengi wetu tumekuwa tukitoroka inapofikia sehemu ya kufikiri.
Umekuwa ukitoroka matatizo na changamoto zako mara kwa mara ili kukwepa kukaa chini na kutatua. Tabia hii ya kutoroka imesababisha tatizo dogo kuwa kubwa na sugu na pia kuzaa matatizo mengine makubwa.
Mara nyingi tunapokutana na mambo magumu huwa tunatoroka kwa kufanya mambo ambayo yatatupatia furaha ya muda mfupi na kujiona tunafurahia maisha. Tatizo linakuwa kwamba pale furaha hii ya muda mfupi inapokwisha tunarudi pale pale kwenye tatizo la msingi.
Kuna njia nyingi ambazo watu wanatumia kutoroka changamoto zao, hapa nitazungumzia baadhi ya njia hizo. Zisome njia hizi na uone ni ipi unayopendelea kutorokea ili uweze kubadilika kwa sababu wengine hujikuta wanatoroka bila ya wao wenyewe kujua wanatoroka. Unaweza kuona unachofanya ni utaratibu wa kawaida wa maisha kumbe ni njia ambayo ubongo wako unakupumbaza na kukudanganya kwamba hiki ndio sahihi cha kufanya.
Njia ambazo wengi hutumia kutoroka ni hizi zifuatazo;
1. Utumiaji wa vileo.
Hii ni njia ambayo inatumiwa na watu wengi sana. Kuna mpaka usemi unatumika sana “kunywa pombe usahau shida zako”. Ni kweli unapotumia ulevi wowote utasahau shida zako ila ni kwa muda tu, tatizo la msingi bado liko pale pale. Na kupitia ulevi unazidi kuongeza matatizo mengi zaidi maana vileo vingi vinaleta hali ya uteja. Vileo vinavyotumika na wengi ni pombe, mihadarati na sigara.
2. Kutumia mitandao ya kijamii.
Kuna ulevi na uteja mpya umeingia duniani sasa hivi ambao ni mitandao ya kijamii. Mitandao hii hasa facebook na twitter imetoa njia rahisi sana ya kutoroka matatizo na changamoto. Kuna watu wanatumia mitandao hii kuripoti kila tatizo wanalokutana nalo kwenye maisha. Siku hizi hata makazini mtu akifanya kazi kidogo akakutana na changamoto inayohitaji kufikiri atakimbilia kwanza facebook au twitter kuona ni nini kinaendelea, watu wanasema nini, nini ni habari ya mujini. Kwa kuingia tu anajikuta anatoka baada ya saa moja kuisha na tatizo la msingi anakuwa amelisahau. Siku hizi hata wapenzi wakigombana wanakimbilia mitandao ya kijamii, utaona tu maandiko kama, “wanaume hawafai”, “wanawake hawajielewi” na kadhalika. Yote hii ni jitihada za kukimbia tatizo la msingi.
3. Kuangalia tv, sinema, filamu au tamthilia.
Kuna ulevi na uteja mkubwa sana ambao nao unakua kwa kasi sana. Kuna hizi tamthilia zinaitwa “series”. Mtu anaweza kutumia hata masaa sita kwa siku akiangalia series moja. Mara nyingi watu hukimbilia kuangalia series hizi wanapokutana na tatizo au changamoto inayowataka kufikiri. Baadae wanajikuta wametumbukia kwenye uteja wa series na kuzidi kutafuta series nyingi zaidi.
4. Kufanya jambo lolote ambalo litaleta mafanikio ya haraka.
Wakati mwingine mtu anapokutana na changamoto huishia kufanya jambo ambalo litaonesha mafanikio ya haraka ila jambo hilo linakuwa halina msaada wowote kwenye tatizo ama maisha yake. Mfano wa mambo hayo ni kupanga meza au vitabu, kufanya usafi au kuweka mipango zaidi.
Njia nyingine za kutoroka ni kupiga soga, kuzurura, kufanya mawasiliano ya simu au ujumbe mfupi yasiyo ya msingi na kulalamika.
Kuna moja kati ya njia hizo unapenda kuitumia kutorokea changamoto zako. Acha mara moja kutoroka changamoto na kaa chini ufikiri jinsi ya kuzitatua. Kutoroka changamoto sio kuikwepa bali ni kuisogeza mbele na kuikuza zaidi.