Katika maisha kila mtu anataka kuwa wa tofauti kwa kufanya mambo kwa utofauti na watu wengine. Kila mtu anataka kufanikiwa na hivyo tunatumia mbinu mbalimbali kufikia mafanikio yetu.
  Moja ya vitu tunavyovifanya ili kufikia mafanikio yetu ni kuweka
malengo na mipango. Na katika kuweka malengo ndipo tofauti kubwa inapoanzia kwenye jamii. Wale wanaoweka malengo inakuwa rahisi sana kwao kufikia malengo yao. Na wale wasioweka malengo wanajikuta wanakwenda tu na upepo wa matukio ya maisha.
  Hata kwa wanaoweka malengo, wale wanaoweka malengo makubwa wanafanikiwa zaidi kuliko wale wanaoweka malengo madogo na ya kawaida sana.
  Kama ndio rahisi hivi kufanikiwa kwa kuwa na malengo na mipango mikubwa kwa nini watu wengi kwenye jamii hawajafanikiwa?
         SEMINA
  Jibu ni rahisi sana, kwa sababu jamii haifanyi na hivyo yoyote anayefanya mambo haya anaonekana wa tofauti kwenye jamii na jamii inamshangaa. Watu wote waliofanikiwa kwa kiwango kikubwa waliweka malengo makubwa sana ambapo jamii iliwashangaa na kudhani wamechanganyikiwa. Lakini kwa kuwa walijua ni nini wanafanya na ni wapi wanataka kufika waliendelea kufuata malengo yao mpaka mwisho wakafanikiwa.
  Hata wewe kama hakuna anayekushangaa na kukuona umechanganyikiwa nasikitika kukuambia hakuna jambo kubwa unalofanya kwenye maisha yako. Hivyo utakuwa unafanya kila kitu sawa na kila mtu anavyofanya kwenye jamii, na kama unavyojua sehemu kubwa ya jamii inasukuma tu maisha hivyo na wewe utakuwa unasukuma tu maisha.
  Ili kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako ni lazima uwe na malengo makubwa na utambue uwezo mkubwa na vipaji vya kipekee vilivyo ndani yako. Ni lazima uishi kwa mipango yako na sio ile iliyowekwa na jamii. Kama njia unayotumia ni sahihi usiogope hata kama upo mwenyewe.
  Jamii itakucheka na kukudharau wakati unaanza na kupitia magumu ila utakapofanikiwa kila mtu atakuwa pale kukupongeza.
  Jamii itakuona kama umepotea na kuchanganyikiwa ila utakapofanikiwa itakutumia kama mfano wa kuigwa.
  Hivyo ukikata tamaa leo kwa sababu ya jamii kukuona umechanganyikiwa haikusaidii zaidi ya kukufanya kuwa mmoja wa wanajamii ambao hawana mipango mikubwa kwenye maisha yao.
  Ota ndoto kubwa, weka malengo makubwa, weka mipango madhubuti ya kufikia malengo yako kisha fanyia kazi mipango hiyo. Utakatishwa tamaa hata na watu unaowaheshimu sana, wengi watakucheka na kukuona umechanganyikiwa ila ukikomaa na kufanikiwa kila mtu atachekelea na kukupongeza.
  Fanya maamuzi leo, unafanya kile unachohitaji kufanya ili ufikie malengo uliyojiwekea au unafanya kile ambacho kila mtu kwenye jamii anafanya na mafanikio ni kidogo sana? Chaguo ni lako, maisha ni yako. Kumbuka wewe ni dereva wa maisha yako. Kama utawaachia wengine waendeshe maisha yako kila siku utakuwa na hofu, ila kama umeshikilia usukani wa maisha yako utakuwa na furaha kila siku.