Leo tutaangalia mahitaji matano ya msingi ya kila mwanadamu ambayo yanamsukuma kufanya maamuzi fulani. Kwa kujua mahitaji haya itakusaidia kukuza biashara yako kwa kutoa bidhaa au huduma ambazo zinatimiza mahitaji ya msingi ya watu. Mahitaji hayo ni;
1. Hitaji la kumiliki.
Kila mtu anapenda kuwa na umiliki wa vitu fulani ambavyo vinarahisisha maisha yake au vinafanya maisha yake kuwa bora. Umiliki wa vitu kama fedha, gari, nyumba na vingine vinawafanya watu kujisikia kwamba wana mafanikio kwenye maisha yao. Pia umiliki wa uwezo wa kufanya maamuzi, madaraja ya kijamii na nguvu ya ushawishi ni hitaji kubwa la watu. Biashara zinazoahidi kuwafanya watu kuwa matajiri, maarufu, wenye ushawishi na nguvu ya maamuzi zinapata mwitikio mkubwa sana wa watu.
2. Hitaji la kuonekana wa thamani.
Kila mtu anapenda kuonekana wa thamani kwa watu wengine. Tunapenda kupendwa na kuheshimiwa na watu wengine. Biashara kama za migahawa, mikutano mikubwa na hata biashara za kubadili muonekano wa mtu zinafanikiwa kwa kutumia hitaji hili.
3. Hitaji la kujifunza.
Watu wanapenda kujifunza vitu vipya ili kuboresha maisha yao au kupata madaraja fulani kwenye kazi au jamii. Pia watu wanapenda kujifunza vitu vipya ili kujibu maswali ambayo yamekuwa yakiwatatiza. Biashara za huduma za elimu, uchapishaji vitabu na semina za mafunzo zinapata wateja kutokana na hitaji hili la msingi la binadamu.
4. Hitaji la ulinzi.
Watu wanapenda kujilinda wao wenyewe na wale wanaowapenda. Pia watu wanapenda kulinda mali zao na hata haiba zao. Biashara kama bima, huduma za kisheria, ulinzi na mitambo ya kuzuia wezi zinapata wateja kutokana na hitaji hili la binadamu. Biashara zinazoahidi kuwaweka watu salama na kuepuka matatizo zinafanikiwa kupitia hitaji hili.
5. Hitaji la kupata hisia nzuri.
Watu wanapenda kupata hisia nzuri zitakazowafanya wafurahi na waone maisha yao yana maana. Watu wanapenda kuburudika na kustareheka. Biashara kama ya burudani, michezo, muziki, maonesho na tamthilia na filamu zinapata wateja wengi kutokana na hitaji hili la watu.
Mahali ambapo watu wanakosa mahitaji haya kuna soko la biashara inayoweza kutimiza hitaji linalokosekana. Kama biashara unayofanya inaweza kutimiza hitaji zaidi ya moja kwenye hayo ndivyo soko linavyozidi kuwa kubwa.
Biashara kubwa ambazo zimefanikiwa sana zimeweza kutimiza mahitaji hayo kwa watu. Kuna biashara ambazo zimeweza kutimiza mahitaji mengi kwa biadhaa au huduma moja. Mahitaji kama kupata fedha, umaarufu, ujuzi, ulinzi, hadhi, ushawishi, starehe na nguvu yameweza kufanya baadhi ya kampuni kufanikiwa sana.
Ufanye nini?
Kama unafanya biashara au unapanga kuingia kwenye biashara kuna mambo matatu muhimu unatakiwa kufanya juu ya mahitaji haya muhimu ya kila binadamu.
1. Jua biashara yako inatimiza hitaji lipi kati ya mahitaji hayo ya msingi. Kwa kujua hili ni rahisi kujua jinsi ya kuweza kuwafikia wateja wako vizuri na pia kuongeza soko.
2. Angalia ni hitaji gani jingine unaweza kutimiza kupitia biashara yako. Kama biashara yako inatimiza hitaji moja tu angalia jinsi unavyoweza kuiboresha na kutimiza hitaji zaidi ya moja, hii itakusaidia kukuza soko lako.
3. Weka mikakati ya kuboresha mahitaji unayotimiza ili kutengeneza wateja wapya na kubakiza wateja wa zamani.
Kwa kufanya hivi itakusaidia kukuza biashara yako na kufikia mafanikio.