Kila mmoja wetu anapenda kuwa na fedha zitakazomtosheleza mahitaji yake na kuweza kumuondoa kwenye umasikini. Pamoja na kupenda fedha na kuuchukia umasikini bado matendo yako hayaonyehi hivyo. Matendo yako yanakwenda kinyume kabisa na mapenzi au mawazo yako.

Matendo yako yanaonesha kwamba hupendi fedha na hutaki kuondoka kwenye umasikini. Ni vipi matendo yako yanaonesha hivi? Leo tutajadili tabia kumi zinazoonesha kwamba hupendi fedha na unataka kuendelea kuukumbatia umasikini.

Kwa wiki nne zilizopita haka kwenye KISIMA CHA MAARIFA tumemekuwa tunajadili kuhusu kujenga tabia ya matumizi mazuri ya fedha. Kama ulifuatilia makala zote kwa makini nina imani utakuwa umejifunza mambo mengi sana. Na kama umeanza kuyatumia mambo haya kwenye maisha yako utaona mabadiliko makubwa sana. Ila kama umeendelea kugoma na kuendelea kung’ang’ania tabia zako mbaya kuhusu fedha utaendelea kulalamika kila siku.

Hizi hapa ni tabia kumi mbaya kuhusu fedha zinazokurudisha nyuma kila siku, kukufanya uwe na maisha magumu na kuendelea kuwa masikini.

1. Kutumia fedha bila ya bajeti.

Kuna sababu kubwa sana kwa nini kila serikali, kampuni au taasisi duniani inakuwa na bajeti ya matumizi ya fedha. Ni kwa sababu inajulikana kwamba fedha yoyote ambayo haijapangiwa matumizi itatumika hovyo tu. Na wewe kwa kuwa huna mpango wa matumizi ya fedha zako unajikuta unazitumia hovyo na zikishakwisha unajiuliza zimekwenda wapi aua nani kakuibia. Kujua zaidi kuhusu tabia zako mbaya kifedha soma; tatizo sio fedha, tatizo ni wewe.

2. Kutokuweka akiba.

Tabia ya kutokujiwekea akiba ni moja ya tabia ambazo zinakufanya uendelee kuwa na maisha magumu na kushindwa kuondoka kwenye umasikini. Kushindwa kujiwekea akiba ni tabia yako mbaya tu kifedha na huna sababu nyingine ya msingi. Kama unafikiri unashindwa kujiwekea akiba kwa sababu kipato chako ni kidogo unajidanganya mwenyewe. Soma; Anza kujijengea tabia ya kujiwekea akiba na uone ni jinsi gani unavyoweza kuanza kuweka akiba hata kama kipato chako ni kidogo.

3. Kununu vitu bila ya mpangilio.

Ni mara ngapi umekutana na mtu njiani anauza kitu na ukashawishika kukinunua japo hukuwa na mahitaji ya kukinunua? Ni mara ngapi umenunua kitu cha aina hii na baadae ukawa huna matumizi nacho au kikawa sio muhimu kama ulivyofikiri? Hii ni tabia mbaya kwenye matumizi ya fedha na inakurudisha sana nyuma. Usinunue tu kitu kwa sababu anayeuza amekushawishi ununue, nunua kitu ambacho umepanga kununua na unamahitaji nacho kweli.

4. Kununua vitu vya bei rahisi.

Kununua vitu vya bei rahisi ni tabia mbaya kifedha na inachangia kwa kiasi kikubwa sana kukurudisha nyuma na kuendelea kubaki kwenye umasikini. Bado hujaelewa vizuri? Mara nyingi unafikiri kununua vitu vya bei rahisi ndio kutunza fedha, ila unapofikiri vizuri vitu vya bei rahisi vina ubora hafifu na hivyo kukufanya ununue mara nyingi. Kwa upande mwingine kuna vitu vinakuwa vinauzwa bei ghali ila vina ubora mkubwa na vinadumu kwa muda mrefu.  Kwa mfano mtu anayenunua gari kwa bei rahisi kutoka kwa mtu anaweza kupata usumbufu mkubwa sana baadae kwenye matengenezo au kuimudu gari hiyo. Ila yule anayenunua gari ambayo bado ni mpya au haijatumika sana ataitumia muda mrefu kabla ya kuanza kugharamia matengenezo.

5. Kutegemea chanzo kimoja cha mapato.

Kama unategemea chanzo kimoja tu cha mapato hasa kwa wale walioajiriwa unajijengea mazingira magumu sana. Unapokuwa na chanzo kimoja tu cha mapato ambacho ni ajira ni rahisi sana kwako kuendelea kubaki kwenye umasikini. Jijengee utaratibu wa kujiwekea akiba na tumia akiba hiyo kuwekeza sehemu mbalimbali ambapo unaweza kuwa na vipato vingine. Wiki zijazo tutajadili kwa kina kuhusu sehemu mbalimbali za kuwekeza hapa Tanzania, usikose kuwepo kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

6. Kukopa kwa ajili ya matumizi.

Mikopo ni mizuri sana ila kama mikopo hiyo ni ya kuzalisha, yaani unachukua mkopo na kuweka kwenye biashara ili ikue zaidi. Ila kama unachukua mkopo kwa ajili ya kwenda kula, hii ni tabia mbaya ambayo itaendelea kukudidimiza kwenye umasikini. Unapochukua mkopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida unajijengea tabia ya kutegemea mikopo na mwishowe kujikuta unaishi maisha ya kukopa na kulipa na kushindwa kufurahia kipato chako.

7. Kufanya matumizi kwa kuiga.

Kama kuna kitu unanunua kwa sababu wanaokuzunguka nao wamenunua au unataka uonekane na wewe unamiliki kitu hiko ni tabia mbaya kifedha. Nunua kitu ambacho unakihitaji na una matumizi nacho, usifanye manunuzi kwa kusukumwa na wengine. Huwezi kushindana na watu katika maswala ya fedha, utajikuta unaumia mwenyewe. Jua kipato chako na panga matumizi kutokana na mahitaji yako.

8. Kuendelea kununua mizigo.

Kama unapendelea kununua vitu ambavyo havizalishi hii ni mizigo na inaendelea kukurudisha nyuma. Badili mtazamo wako kutoka kupendelea kununua vitu ambavyo havizalishi na kuanza kununua vitu ambavyo vinakuzalishia hata kama ni fedha kidogo. Kwa mfano nusu ya nguo ulizonazo hujawahi kuzivaa miezi sita iliyopita ila bado unaendelea kununua nguo mara kwa mara, hii ni tabia mbaya kifedha.

9. Kuwekeza sehemu ambayo huijui vizuri.

Umeweka akiba yako na unataka kuwekeza anakuja mtu anakuambia kilimo cha mpunga kinalipa sana, njoo tufanye kilimo hiki. Huna uelewa wowote kuhusu kilimo hiki ila wewe unamuamini na kumkabidhi fedha ukiamini sasa umasikini unaanza kuaga. Baadae unakuja kukuta kuna changamoto nyingi kwenye kilimo hiko na hivyo kushindwa kupata faida uliyotarajia. Kila kitu kina changamoto zake, hivyo jiridhishe kabla hujaingia kwenye uwekezaji wowote ili usije ukaingia kwenye hasara.

10. Kuendekeza starehe.

Kuna wakati kweli unahitaji kujiburudisha ila kama kila siku unajiburudisha kwa gharama kubwa ni tabia mbaya kifedha. Haijalishi unapata kiasi gani cha fedha bado ni tabia mbaya kama kila siku unakaa baa na kunywa au kufanya starehe nyingine yoyote. Licha tu ya kutumia fedha vibaya, pia unapoteza muda wako mwingi kama kila siku unafanya starehe na hivyo kushindwa kufuatilia mambo yako kwa karibu.

Hizi ni baadhi ya tabia mbaya kifedha ambazo zinaendelea kukurudisha nyuma kila siku. Tabia hizi unaweza kuona ni mambo ya kawaida ila zina athari kubwa sana kwenye maendeleo yako.

Ni kwa tabia hizi unashindwa kujua fedha zako zinapotelea wapi na hivyo kuishia kulaumu kwamba kuna chuma ulete wanaokuibia fedha zako. Anza leo hii kuzifanyia kazi tabia hizi na nyingine ulizonazo na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii fanya zoezi moja, katika kitabu chako cha kuandika kuhusu mambo ya fedha orodhesha tabia zote za matumizi yako ya fedha ambazo zinakurudisha nyuma. Baada ya kuandika tabia hizi weka mkakati wa kuanza kuzitokomeza ili kuondokana na maisha magumu.

Usisahau kutushirikisha chochote unachojifunza kwenye kubadili kwako tabia kwenye FORUM-MAJADILIANO ili tuweze kujifunza kwa pamoja.

Nakutakia kila la kheri,

TUKO PAMOJA.