Kwa miezi miwili, kila wiki tumekuwa tukipata makala moja ya kujifunza jinsi ya kujenga tabia nzuri kwenye matumizi ya fedha. Pia tumejifunza jinsi ya kujenga tabia ya kujiwekea akiba na muhimu zaidi tumejifunza jinsi ya kuwekeza fedha ili kupata thamani zaidi.

Kama umefuatilia makala zote hizi kwa makini na kuanza kutekeleza yale uliyojifunza utakuwa kwenye hatua nzuri sana kwa sasa. Na kama bado hujaanza utekelezaji unasubiri nini? Huna sababu yoyote ya kusema kwamba unashindwa kutengeneza tabia ya matumizi mazuri ya fedha zako na kujiwekea akiba. Ukisema una kipato kidogo, sio sababu maana tulijadili sana ni jinsi gani unaweza kuweka akiba kama una kipato kidogo. Ukisema matumizi yako ni mengi sio sababu kwa sababu tulijadili ni jinsi gani ya kupunguza matumizi yasiyo ya msingi. Hivyo anza leo hii kutekeleza yale uliyojifunza.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala zote zinazohusiana na tabia za mafanikio hususani kwenye hii tabia ya fedha bonyeza maandishi haya na uanze kuzisoma makala zote.

Leo katika kuhitimisha tabia hii ya matumizi mazuri ya fedha tutaangalia aina mpya ya mawazo unayotakiwa kuwa nayo kwenye kichwa chako ili uweze kufikia uhuru wa kifedha. Mara nyingi nimekuwa naandika kwamba mafanikio yoyote yanaanzia kwenye kichwa chako, kushinda au kushindwa kunaanzia kwenye akili yako na ndio kunadhihirika kwenye maisha ya kawaida.

Hata matatizo yote ya fedha uliyonayo sasa yameanzia kwenye akili yako. Yanatokana na mtazamo ulioujenga na kujengewa kwenye kichwa chako kwamba kazi yako kubwa kwenye maisha ni kufanyia kazi fedha, yaani kuzikimbiza fedha. Na umejifunza hili vizuri sana na sasa unakazana kulitekeleza huku maisha yako yakiendelea kuwa magumu sana.

Leo tunafanya kazi moja ya kuondoa mtazamo huu unaokudidimiza na kupandikiza mtazamo mpya utakaokuinua na kukufikisha kwenye mafanikio makubwa sana.

Usiifanyie kazi fedha, wacha fedha ikufanyie wewe kazi.

Kwa maneno mengine naweza kusema usiikimbize fedha wacha fedha ikukimbize wewe.

Unawezaje kufikia hatua hii ambapo fedha inakufanyia kazi wewe? Ambapo fedha inakukimbiza wewe? Ambapo huna hofu tena juu ya fedha? Yote haya yanaanza na kuamua haya yote yatokee. Na yote haya yanaweza kutokea kama utatekeleza yale uliyojifunza humu kwenye KISIMA CHA MAARIFA na pia kwenye AMKA MTANZANIA. Kama unapata shida kwamba utaanzaje kuyatekeleza wacha hapa nikupatie muhtasari kidogo;

1. Kuwa na chanzo cha kipato.

Hatua ya kwanza kabisa ni kuwa na chanzo cha kipato, yaani shughuli yoyote ambayo unaifanya na kulipwa au kupata kipato. Usiniambie hujapata kazi au kazi uliyonayo hailipi. Kama huna kazi kuna fursa nyingi za kuweza kujiajiri au kufanya biashara.

2. Fanya kazi yako kwa viwango vya hali ya juu sana.

Kwa kazi hii ambayo unaifanya na kukuingizia kipato ifanye kwa viwango vya hali ya juu sana. Na ili uweze kuifanya kwa viwango vya hali ya juu inabidi uipende sana. Hata kama sio kazi uliyokuwa unatamani kuipata, kwa kuwa hii ndio itakuwa daraja lako kwa sasa ipende na ifanye kwa moyo mmoja na kwa viwango vya juu sana.

3. Weka malengo utaifanya kwa muda gani.

Baada ya kuwa na shughuli hii na kujitoa kuifanya kwa viwango vya juu sana, weka malengo utaifanya kazi hii kwa muda gani. Usifanye tu kazi kwa vile unalipwa na ukasahau kujipanga kwa mambo mengine. Hapa ndio wengi wanaishia kuwa watumwa wa fedha na kutumia maisha yao yote kufanyia kazi fedha.

4. Anza utaratibu wa kuweka akiba.

Baada ya kujua ni muda gani umejiwekea wa kufanya kazi hiyo, sasa anza utaratibu wa kujiwekea akiba. Kwa watu wa kawaida nimekuwa nikiwaambia waanze kwa asilimia 10 ya kipato chao, ila kwa wewe ambaye upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA sio wa kawaida, wewe ni zaidi ya wa kawaida, hivyo nitakuambia uanze na asilimia 30 na uende mpaka asilimia 50. Najua unaweza hili kwa sababu umejifunza mengi sana. Na kama kipato ulichonacho hakitoshi, tulishakubaliana kwamba unaongeza kipato na sio kupunguza akiba. Kama utaipenda kazi unayofanya, kama utaifanya kwa moyo mmoja na kwa viwango vya kimataifa, utashangaa fedha zitakuwa zinakufuata kila unapoelekea.

5. Anza kuwekeza.

Baada ya kuweka akiba kwa muda anza kuwekeza ili kuongeza thamani ya fedha zako. Tumezungumza mengi sana kuhusu uwekezaji na kama utapitia makala hizo za nyuma utaona njia zote za uwekezaji nilizopendekeza.

Hii ndio njia rahisi sana ambayo mtu yeyote, wa jinsia yeyote na kabila lolote, iwe ana shahada au hakumaliza elimu ya msingi anaweza kuitumia kufikia uhuru wa kifedha. Unaweza kujifunza zaidi kwa kusoma makala hii; Kuwa tajiri kwa kufuata sheria hii rahisi sana(bonyeza maandishi hayo kusoma)

Pia unaweza kuendelea kujifunza zaidi kuhusu matumizi mazuri ya fedha zako kwenye uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD unaoendelea hapa kwenye KISIMA. Kusoma makala za uchambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya.

Nakusihi sana uendelee kutumia haya unayojifunza kila siku, nina imani kwamba yatabadili maisha yako kama yalivyobadili maisha yangu na ya wengine wengi.

Nakutakia kila la kheri katika safari hii ya mafanikio.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.