Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.
Katika uchambuzi uliopita tuliona RICH DAD akiwaambia Mike na Robert kuhusu mbio za panya. Na aliwaambia mbio hizi zinachangiwa na hisia mbili ambazo zipo kwa kila binadamu, hofu na tamaa.
RICH DAD aliendelea kuwaambia kwamba lengo lake kubwa ni kuwafundisha jinsi ya kuepuka mtego ambao utawaingiza kwenye mbio hizo za panya na sio kuwafundisha tu kuwa matajiri. Aliwaambia kuwa tajiri hakutatui tatizo, bali ndio linazidi kuongezeka. Aliwaambia watu wengi wanapopata fedha wanaingiwa na tamaa ya kuitumia ili kupata raha na furaha na inavyozidi kuwa nyingi matumizi nayo yanazidi kuwa mengi. Hivyo wanajikuta wakitaka fedha nyingi zaidi na kuamini ndio zitawatoa kwenye tatizo hilo.
Alisema hata matajiri wengi wapo kwenye mtego huu wa mbio za panya. Anasema wanaanza na hofu ya kutokuwa na fedha na hivyo wanafanya kazi kwa bidii sana ili wapate fedha nyingi. Na wanapopata fedha nyingi na kuwa matajiri wanakuwa na hofu kubwa zaidi ya kupoteza fedha walizopata, hivyo kujikuta wakiishi katika utumwa wa fedha. Aliwaambia ana marafiki zake ambao bado wanafanya kazi sana wakati tayari wana fedha nyingi sana, na wanahofu kubwa sasa kuliko hata waliyokuwa nayo wakati hawana fedha nyingi.
RICH DAD aliwaambia anataka kuwafundisha nguvu ya kutawala fedha, na sio kuiogopa. Na aliwaambia elimu hii haifundishwi kwenye shule yoyote. Aliwaambia kama hawatajifunza elimu hiyo watakuwa watumwa wa fedha. Robert alianza kumuelewa RICH DAD na akaanza kuona jinsi baba yake anavyoteseka na fedha, mtazamo wake ulipanuka sana siku hiyo.
RICH DAD aliwaambia anataka kuwafundisha jinsi ya kuepuka mtego huo unaoletwa na hisia zile mbili na pia jinsi wanavyoweza kuzitumia hisia hizo kutawala fedha na sio kuwa watumwa wa fedha. Alisema kama atawafundisha tu kupata fedha nyingi bado haitawasaidia kwenye hisia mbili za hofu na tamaa na kama wakishindwa kutawala hisia hizo watakapokuwa watajiri watakuwa watumwa wanaolipwa fedha nyingi.
Robert aliuliza wanawezaje kuepuka mtego huo? Rich dad alijibu matatizo yote ya fedha yanaletwa na hofu na ujinga na sio uchumu, serikali au kitu kingine chochote. Hofu na ujinga wa kujitengenezea ndio unawafanya watu wengi kuingia kwenye mtego wa mbio za panya. Aliwambia waende shule na wajifunze ila yeye atawafunsisha jinsi ya kuepuka mbio za panya. Robert alianza kupata picha halisi ya tofauti kati ya baba zake hao wawili.
Kuzitawala hisia.
Rich dad aliendelea kuwaambia kwamba kila binadamu ana hisia mbili za hofu na tamaa, na aliwaambia ili kufikia mafanikio ni lazima waweze kuzitawala hisia hizo na kuzifanya ziwatumikie wao na sio wao kuzitumikia. Aliwaambia watu wengi wanatawaliwa na hisia hizo na ndio chanzo cha ujinga unaowaingiza kwenye matatizo ya fedha. Aliwaambia watu wengi wanaishi maisha yao kukimbiza fedha, mshahara na ongezeko la msahara bila ya kujua hasa hisia hizo mbili zinawapeleka wapi. Aliwaambia ni sawa na picha ya punda ambaye anavuta mkokoteni na mbele yake amewekewa chakula. Yule punda atakuwa anakaza mwendo akiamini atafikia chakula kile wakati anayemwendesha anajua ni wapi anakwenda. Hivi ndivyo watu wanavyokimbiza fedha bila ya kujua wanaelekea wapi.
Aliwaambia watu wanapata fedha na kuanza kununua vitu vya kujionesha kama magari, nyumba za kifahari na mengine. Hofu ya kutokuwa na fedha inawasukuma kwenda kazini na tamaa ya kuzitumia inawavuta zaidi kuendelea kuwa kwenye mtego.
Mike alimuuliza sasa jibu ni nini? Alijibu kinachofanya hofu hizi mbili kumtawala mtu ni ujinga. Aliwaambia mtu anapoacha kujifunza na kujiendeleza binafsi ndio ujinga unapoanza. Aliwaambia elimu ya shule ni muhimu sana, kila jamii inahitaji walimu, madaktari, wanasheria, mainjinia na kadhalika, ila kwa bahati mbaya wengi wanaacha kujifunza wanapohitimu. Elisema ujinga kwenye elimu ya fedha ndio unaoleta matatizo makubwa kwenye jamii zetu.
Aliwapa mfano kwamba daktari akitaka fedha nyingi anaongeza bei ya huduma zake, hii inapelekea watu kushindwa kupata huduma hizo, kutokana na daktari kuongeza mwanasheria naye anaongeza gharama zake, walimu nao wanataka kuongezwa mshahara. Yote haya yanafanya bei za bidhaa zinakuwa juu na hata kodi inakuwa juu. Hivi ndivyo ujinga wa fedha unavyoadhiri jamii nzima. Na aliwaambia tofauti ya wenye nacho na wasiokuwa nacho inapokuwa kubwa ndio hali huchafuka na kupelekea kuanguka kwa taifa. Robert aliuliza kwani gharama hazitakiwi kuongezeka? Alimjibu kwa jamii inayoongozwa na serikali bei hazitakiwi kupanda bali kushuka. Ila kwa vile watu hawana elimu ya fedha suluhisho pekee walilonalo ni kuongeza bei kitu ambacho kinakuwa na adhari kwa jamii nzima. Aliwaambia watu waliosomea elimu ya biashara wanajua kupunguza gharama na kuongeza bei kitu ambacho hakiwezi kuisaidia jamii. Aliwaambia wajifunze jinsi ya kutawala hisia zao na wataweza kuzitawala fedha. Aliwaambia matajiri wanatengeneza fedha na sio kufanyia kazi fedha.
Vitabu vya hadithi.
Rich dad alimaliza mazungumzo yake na kuanza kuondoka. Aliwaambia waache kufikiria kuhusu kuongezwa fedha na watumie vichwa vyao kufikiri jinsi ya kutengeneza fedha. Aliwambia wafanye kazi bure na wakati wanafikiria akili zao zitawaonesha fursa kubwa ya kutengeneza fedha kuliko zile ambazo angewalipa.
Mike na Robert waliondoka na kwenda kukaa sehemu nyingine huku wakifikiria yale waliyojifunz. Wiki iliyofuata kila walipokuwa shuleni waliendelea kufikiri na kuongea kuhusu kufanya kazi bure. Jumamosi iliyofuata walienda kazini kama kawaida na wakati yule mama aliyekuwa anasimamia anaondoka alionekana anakata vitabu vya hadithi ili kupata makava yake. Robert alimuuliza anapeleka wapi yale makava alimjibu anapeleka kwenye duka la vitabu na kupewa vingine. Robert na Mike walienda kwenye lile duka na kuuliza kama wanaweza kupata vitabu vile aliwakubalia ila aliwaambia wasiviuze. Walikubaliana na wakaenda kutumia chumba kimoja kwa kina Mike kuwa kama maktaba, waliweka vitabu pale na wakawa wanawalipisha watoto wengine wanapokuja kusoma vitabu vile. Walimuajiri dada yake Mike ndio awe mkutubi. Maktaba hiyo ilikuwa ikifunguliwa masaa mawili kwa siku baada ya muda wa shule. Waliweza kupata dola tisa kila wiki na yule dada walimlipa dola moja kwa wiki. Waliendelea kukusanya vile vitabu na walitaka kufungua tawi jingine la maktaba. Siku moja vijana wakorofi waliingia kwenye maktaba ile na kuleta fujo. Kitendo hiko kilipelekea maktaba ile kufungwa.
Kutokana na kutokulipwa kwenye kazi ya mwanzo kuliwasukuma kufikiria njia ya kutengeneza fedha na ndio wakaweza kufungua maktaba hii ambayo wao hawakufanya kazi moja kwa moja ila walipata kipato kizuri. RICH DAD aliwapongeza kwa hatua nzuri walizopiga, na alikuwa tayari kuwapa somo la pili. Somo hilo la pili litakujia kwenye uchambuzi ujao.
Tunajifunza nini hapa?
Kuna mengi ya kujifunza katika sehemu hii ya uchambuzi;
1. Binadamu wote tunaendeshwa na sishia mbili kwenye fedha, hofu na tamaa.
2. Hofu inatufanya tufanye kazi na tamaa inatufanya tuingie kwenye mbio za panya.
3. Matajiri wengi ni watumwa wanaolipwa vizuri kutokana na kushindwa kutawala hisia hizi mbili.
4. Tamaa na ujinga ndio vinaleta matatizo ya fedha kwenye jamii zetu.
5. Ni muhimu sana kuendelea kujifunza na kujiendeleza hata baada ya kumaliza masomo.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha,
TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.
Unagusa sana hisia zangu,
Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Nimeanza kuwa mwalimu wa uchumi bila kuingia darasani, nimeanza kufikiri mambo makubwa kuliko mwanzo sasa siwazi tena kuendelea kuwa mtumwa wa kazi za watu bali nawaza nianze kujiajiri mwenyewe.
Nimeanza kutafuta habari sahihi kwa kile ninachokihitaji kukipata, usomaji wa vitabu imeanza kuwa kama desturi yangu na najifunza mambo makubwa yaliyojificha ndani yake.
Nilichogundua ni kwamba maisha tunayofundishwa mashuleni na majumbani kwa asimilia kubwa tunaambiwa bila Elimu ya chuo kikuu huwezi kuwa tajiri na utaishia kuwa masikini.
Nimepata bahati ya kumsikiliza MZEE MFUGALE kwenye ushuhuda wake aliuzwa hivi; unajuta kwa kutosoma? Alisema sijawahi juta hata siku moja sababu niliosoma nao wakawa na elimu kubwa wengi ni maskini wakubwa.
Endelea kutuelimisha japo Mtanzania kwa kusoma vitu kama hivi ni vigumu sana maana tunapenda kufuatilia habari za udaku na mapenzi lakini habari njema hututaki tunaona ni ndefu na zinachosha.
LikeLike
Asante sana Samson kwa kuendelea kujifunza na kuanza kuchukua hatua. Ni kweli kabisa kwamba elimu hii ni muhimu ila sio wote wanaona umuhimu wake. Tuendelee kuwashirikisha wenzetu ili nao wapate mambo haya mazuri.
Karibu sana, TUENDELEE KUWA PAMOJA.
LikeLike
Usijali Tupo Pamoja.
LikeLike
Kweli amani hapa e mengi sana yanayogusa ndan mwangu kiakili tangu nijifunze kupitia kitabu hiki!ahsante sana kwa uchambuzi huu
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike
Asante sana upo sahihi
LikeLike
Karibu.
LikeLike