Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.

Kwa sababu wanafunzi wanamaliza masomo bila ya kupata mafunzo ya fedha, watu wengi wanafanya taaluma zao kwa ufanisi mkubwa lakini wanajikuta wakipata matatizo kwenye fedha. Wanafanya kazi kwa bidii ila hawaone wakiendelea. Kikubwa wanachokikosa kwenye elimu yao sio jinsi gani ya kutengeneza fedha ila ni jinsi gani ya kutumia fedha. Wafanye nini na fedha zao baada ya kuzipata.

Jinsi gani ya kuitumia fedha baada ya kuipata, jinsi gani ya kuzuia wengine wasiichukue kwako na ni jinsi gani ya kuifanya fedha ikufanyie wewe kazi ni mambo muhimu sana kujifunza.

Wtu wengi hawawezi kusema kwa nini wanateseka na fedha kwa sababu hawajui mzunguko wa fedha. Hawajui fedha yao inazungukaje kwanzia wanapoipata mpaka inapoondoka. Watu hawa wanakuwa na elimu na taaluma kubwa ila hawajui chochote kuhusu fedha. Watu  wanafanya kazi kwa bidii sana kwa sababu wanafikiri ndio suluhisho badala ya kuifanya fedha iwafanyie wao kazi kwa bidii.

Kwa mfano vijana wawili wanaoana na kuanza maisha pamoja kwenye nyumba ya kupanga ambayo sio ya hadhi sana kwa kuwa hawana fedha. Kwa kuwa gharama za maisha bado ni ndogo kwao wanaamua kuweka akiba ili wanunue au kujenga nyumba ya ndoto yao. Jinsi wanavyoendelea na maisha vipato vyao vinaongezeka na jinsi vipato vinavyoongezeka matumizi yao pia yanaongezeka na hivyo kujikuta wanakosa fedha ya kuwekeza kwenye mali zinazozalisha. Chanzo chao kikubwa cha mapato inakuwa mishahara yao na hapo mishahara hii imejaa makato mengi sana.

Baadae wanamua kujenga au kununua nyumba yao kwa fedha za mkopo na hivyo wanaednelea kuwa na matumizi makubwa. Baadae wananunua thamani za ndani, wananunua gari na vitu vingine ambavyo havizalishi. Baadae wanajikuta kwenye madeni makubwa na hivyo moja kwa moja wanaingia kwenye mbio za panya. Wakati hayo yakiendelea wanapata mtoto au watoto, hawa nao wanaleta gharama kubwa za maisha. Wanazidi kuingia kwenye madeni ili kuweza kupunguza ukali wa maisha.

Hivi ndivyo watu wengi wanavyoanza maisha na kujikuta katika madeni na mbio za panya za kuishi kwa kufanya kazi na kulipa madeni. Watu hawa huuliza ni nini siri ya kuondoka kwenye mbio hizi za panya, Robert anawaambia tatizo sio fedha wanazopata bali matumizi ya fedha hizo na hii inatokana na kutokuwa na elimu ya fedha.

Robert anasema kuna usemi mmoja rafiki yake anapenda kuutumua;

UKIJIKUTA KWENYE SHIMO ACHA KUENDELEA KUCHIMBA.

Nyumba yako sio mali inayozalisha.

Watu masikini na wa daraja la kati huruhusu nguvu ya fedha kuwatawala, kwa kuamka asubuhi kufanya kazi kwa bidii bila ya kujiuliza wanaelekea wapi. Kwa kuwa hawana elimu ya fedha, nguvu ya fedha inawatawala.

Robert anakumbuka wakati akiwa na miaka 16 yeye na Mike walianza kupata matatizo shuleni. Matatizo haya yalitokana na elimu ya shule waliyoipata kuwa tofauti na ile wambayo waliiopata kutoka kwa RICH DAD. Katika umri huu mdogo walikuwa wamepata bahati ya kukaa kwenye mikutano ya RICH DAD na hivyo kusikia mawazo ya washauri mbalimbali wa wahasibu, wanasheria na hata wafanyakazi wengine.

RICH DAD hakuwa na elimu ya shuleni ila alikuwa na elimu ya fedha. Mara kwa mara alikuwa anawaambia kwamba mtu mwenye akili siku zote anaajiri watu wenye akili zaidi yake. Robert na mike walipokuwa wanajaribu kumuuliza POOR DAD(baba mwenye elimu) kwa nini hawafunsishwi kuhusu fedha, aliwajibu fedha sio muhimu, wakishakuwa na taaluma nzuri fedha itafuata.

Katika umri wa miaka 16, Robert alikuwa na uelewa mkubwa wa fedha kuliko baba yake. Hali hii ilipelekea kuwepo kwa ubishani mkali mara kwa mara kati yake na baba yake ambaye alikuwa POOR DAD. Siku moja poor dad alikuwa namweleza Robert jinsi gani nyumba yao ni ASSET kubwa. Ubishani mkubwa sana ulitokea kati yao na Robert alijaribu kumchorea michoro kuonesha ni jinsi gani nyumba wanayoishi sio asset bali ni liability. Alimwonesha ni jinsi gani nyumba inavyozidi kuwa kubwa na gharama zinaendelea kua kubwa. Nyumba kubwa inakuwa na gharama kubwa za umeme, maji, samani, na hata kodi ya majengo.

Mpaka leo bado watu wengi sana wanampinga Robert anaposema kwamba nyumba sio asset. Watu wengi wana ndoto kubwa za kumiliki nyumba wakiamini hiyo ni asset. Kuwa na nyumba hakuna msaada mkubwa sana kwenye uzalishaji wako wa fedha. Robert anasema watu wengi wanaishi maisha yao kulipa mkopo wa nyumba waliyochukua na baadae wakiona nyumba hiyo ni ndogo au haiwafai wanaingia kwenye mkopo mwingine kununua nyumba nyingine.

Robert anasema kuna makosa makubwa matatu ya kuwekeza kwenye nyumba ambayo haizalishi;

1. Unaishi maisha yako yote kulipa deni la nyumba.

2. Nyumba haiongezeki thamani kwa kasi sana.

3. Unakosa fursa nyingi kwa kuwa umechimbia fedha yako kwenye nyumba.

Makosa haya matatu yanawafanya watu kuendelea kufanya kazi kwa nguvu sana na matatizo ya fedha kuendelea kuwepo. Anasema kama watu wangewekeza kwanza kwenye kununua asset, zingewawezesha kupata nyumba na mali nyingine bila ya kuteseka au kuingia kwenye mkopo.

Tunajifunza nini hapa?

Kuna mengi ya kujifunza katika sehemu hii ya uchambuzi;

1. Ukosefu wa elimu ya fedha unawafanya watu kuendelea kuwa watumwa wa fedha.

2. Matumizi mabaya ya fedha yanawapelekea watu kuingia kwenye madeni na hatimaye kujikuta kwenye mbio za panya.

3. Nyumba ya kuishi sio mali inayozalisha, ni mali inayokuingia wewe gharama na hivyo kuzidi kukuingiza kwenye matatizo ya kifedha.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.

TUKO PAMOJA.