Kuna watu wengi duniani ambao ni wagonjwa wa mawazo kuliko walivyo wagonjwa wa mwili. Magonjwa haya ya mawazo yanasababishwa na ukosefu wa virutubisho muhimu kwa akili. Virutubisho muhimu kwa akili ni mawazo mazuri na yenye kujenga.

Watu wenye ugonjwa wa mawazo ni watu ambao mara zote wanaingiza mawazo yenye sumu kwenye akili zao. Mawazo haya yanaharibu akili zao na hivyo kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Na tatizo kubwa la mawazo haya ya sumu ni kwamba yanaingizwa kwenye akili kila siku.

Je mawazo haya yenye sumu yanaingiaje kwenye akili yako? Unayaingiza wewe mwenyewe kwa kuyawaza. Yaani wewe mwenyewe unajitafutia ugonjwa wa mawazo kwa kufikiria mawazo hasi yenye sumu.

Mawazo yenye sumu yanaweza yasikuue moja kwa moja, pia yanaweza yasiue akili yako kabisa. Lakini mawazo haya yataua kabisa uwezo wako wa kufikia malengo makubwa na hivyo kukuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa. Mawazo haya yanapoua uwezo wako wa kufikia malengo makubwa unaanza kupelekwa tu na maoni ya kila mtu.

Aina za mawazo yenye sumu.

Kuna aina nyingi za mawazo yenye sumu ambayo yanakurudisha wewe nyuma. Hapa tutaangalia mawazo ya aina tano;

1. Vurugu.

Kila kukicha tunasikia habari nyingi kuhusu vurugu au fujo mbalimbali zinazoendelea duniani. Habari hizi huingia kwenye akili yako na kujenga mawazo ya vurugu au fujo. Hivyo mawazo haya hukufanya uone njia mojawapo ya kutaka kile unachopata ni kutumia nguvu au mabavu. Kwa mawazo haya inakuwa vigumu sana kwako kuweza kufikia mafanikio makubwa.

2. Chuki.

Mawazo ya chuki yamesambaa sana kwa watu wengi. Kupitia mawazo haya unaanza kuwachukia watu wengine ambao unawaona tofauti na wewe. Kupitia mawazo haya ya chuki unaweza kuwachukia wale unaoona wana mafanikio kuliko wewe na hivyo kushindwa kujifunza kutoka kwao. Pia mawazo haya ya chuki yanaweza kuwa kwako mwenyewe na hivyo kujichukia. Kama utajichukia sahau kabisa kuhusu kufikia mafanikio makubwa.

3. Hasira.

Hasira nayo ni mawazo yenye sumu ambayo yatakuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa. Unapata hasira pale unapohisi kwamba utu wako haujathaminiwa. Kama ukiendekeza mawazo hayo ya hasira yatakuzuia kuweza kupata au kutumia fursa nzuri zilizoko mbele yako.

4. Kutoroka.

Kila unapokutana na changamoto mbalimbali katika safari yako ya kufikia mafanikio, huwa unapata mawazo ya kuachana na kitu hicho kwa sababu huoni mafanikio. Haya ndio mawazo ya kutoroka na kutaka kufanya vitu ambavyo utaviona ni vizuri kwa wakati huo. Mawazo ya kutoroka ni sumu kubwa kwa akili yako kuweza kufikia mafanikio makubwa.

5. Kuacha.

Haya ni mawazo ambayo yanakutaka kuacha kabisa kufanya jambo fulani kwa sababu labda kwa wakati huu huoni mafanikio. Haya ni mawazo ambayo yanakukatisha tamaa mapema kabla hata ya kuanza. Kwa kuwa na mawazo haya utashindwa kabisa kuchukua hatua muhimu ya kuboresha maisha yako. Mawazo haya ya kuacha yanakufanya usiwe na malengo, usiwe na shauku na usiwe na kitu cha kukusukuma na hatimaye usiwe chochote.

Ni muhimu kutambua mawazo haya yenye sumu na kuanza kuyaepuka mara moja ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayotarajia. Kama una mawazo ya fujo au vurugu achana nayo, kama una hasira sana, chuki au mawazo ya kutoroka au kuacha anza kujirekebisha ili iwe rahisi kwako kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.