Kumbuka kwamba kila mmoja wetu ana hitaji kubwa la kukubalika kwa kile anachofanya au kile alichofanya. Kama hitaji hili la kukubalika lisipotimizwa, mtu hupata hisia za kutokuaminika, hofu ya kutokuweza na hatimaye kushindwa. Ni hisia hizi ambazo humfanya mtu kuamua kuacha kile anachofanya iwe ni elimu, kazi au hata maisha kwa ujumla.

Hisia hizi za kutokukubalika humfanya mtu kujiona ametengwa na familia, ndugu na hata watu wa karibu. Kutokana na haya mtu anaweza kufanya mambo yafuatayo;

1. Dhana ya NITAKUONESHA, ambapo mtu hujaribu kufanya jambo ili kuonesha kwamba yeye ni muhimu. Mara nyingi jambo linalofanyika huwa lina madhara makubwa kwa mtu mwenyewe au hata kwa wale ambao anataka kuwaonesha.

2. Kupoteza mtizamo chanya na msukumo wa kujenga ambapo inapelekea mtu kutoroka au kuacha kile anachofanya.

Wewe kama mtu ambaye unataka kufikia mafanikio makubwa ni lazima uweze kuijua tabia hii kwa watu na jinsi ya kuitumia vizuri ili uweze kupata ushirikiano wa kutosha. Kumbuka katika kufikia mafanikio ni lazima uweze kuwashawishi watu wakubaliane na kile unachotaka wao wafanye. Watu wa aina hii wanaweza kuwa ni wafanyakazi wako, washirika wako au hata wanafamilia wako.

Ili uweze kushawishi watu wa aina hii ni lazima uoneshe kujali hitaji lao la kukubalika kwa kile wanachofanya. Jua ni kitu gani mtu huyo anataka kukubalika nacho kisha angalia ni jinsi gani unaweza kumpa sifa bila yakudanganya.

Tumia njia ifuatayo kufanya hivyo;

1. Anza kwa kuonesha kukubali na kusifia kila kitu anachofanya au alichokamilisha, ila fanya hivyo kwa uaminifu mkubwa, usidanganye. Kila mara unapopata nafasi ya kuzungumza na mtu huyu onesha kujali na kukubali mafanikio yake.

2. Jali sana hisia za watu hawa na hizi ndio zitakazokuwezesha kujua ni sifa zipi ambazo mtu huyu anataka kukubalika nazo.

3. Jinsi ambavyo unaweza kujua sifa nyingi ambazo mtu huyu anataka kukubalika nazo na ukaweza kuzikubali kwa njia ambayo ataridhika, ndivyo nafasi yako ya mafanikio inazidi kuwa kubwa.

Kwa kuwa mafanikio yanakuja pale ambapo unaweza kuwasaidia watu wengi zaidi kupata kile wanachotaka, ni muhimu kujua jinsi ya kuwapatia watu wengi kile wanachotaka. Moja ya kitu ambacho kila mtu anataka ni kukubalika kwa kile anachofanya na pia kusifiwa kwamba anafanya vizuri. Lakini dunia ya sasa watu wengi hawaangalii sifa hizi kwa watu na hivyo watu kujiona kama wanadharaulika au hawakubaliki. Jukumu lako kwanzia leo ni kuangalia ni sifa gani unayoweza kuisifia kwa mtu yeyote unayekutana naye kwenye maisha yako ya kila siku. Iwe ni bosi wako, mwajiri wako, mfanyakazi wako, mwenza wako, mtoto wako, ndugu yako au hata mteja wako. Kuna kitu fulani mtu huyu anataka kikubalike na kama ukiweza kukijua na kutimiza utajenga urafiki mkubwa sana na mtu huyo na ukiweza kufanya kwa wengi zaidi utakubalika na watu wengi sana.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.