Kwa kuwa sasa umeshaamua kujiajiri mwenyewe au kufanya biashara kuna mambo ya msingi unahitaji kuyajua au kuyakamilisha ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Jiulize kama kuwa bosi wako mwenyewe ni kitu muhimu sana kwako, jiulize kama ni mtu ambaye unaweza kufikia mafanikio ukiwa unajifanyia kazi yako.

Jiulize ni yapi madhaifu yako na pia ni yapi mazuri yako katika kuendesha biashara yako mwenyewe. Je wewe ni kiongozi mzuri? Je wewe ni muandaaji mzuri? Je unaweza kuvumilia hata mambo yanapokuwa magumu? Je unaweza kukaa muda mrefu bila ya kutegemea mshahara?

Ni vyema kujiuliza maswali haya na kuyajibu kwa uaminifu kabla ya kuingia kwenye kujiajiri au kufanya biashara. Maana haya ndio yatakuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

Mambo ya kufanya na kutokufanya unapoanza biashara au kujiajiri.

1. Usiajiri ndugu kwenye biashara yako kama unaweza kukwepa hilo.

2. Kuwa muaminifu kwa tabia zako ili kujua udhaifu wako na uimara wako.

3. Pata ushauri wa kisheria, utakusaidia usije kuingia kwenye mambo yatakayokuletea hasara.

4. Kuwa mkweli kwa familia yako. Katika kujiajiri au kufanya biashara kuna wakati utafanya kazi zaidi ya kawaida, kuna wakati utakuwa mbali na familia yako. Hivyo familia yako inaweza kupata madhara fulani kwa wewe kujiajiri au kuwa kwenye biashara.

5. Weka mipango ya mbele. Ni vizuri kujua ni hatua gani inafuata mbele au ni kitu gani unategemea kitokee.

6. Usikatishwe tamaa mambo yanapokuwa magumu, uvumilivu ni muhimu.

Maswali muhimu ya kujua kama unavyo vinavyohitajika kuanzisha biashara au kujiajiri.

Jiulize maswali haya na kujipa majibu sahihi na ya uaminifu ili uweze kujua unaanzia wapi.

1. Je unaweza kuanzisha na kuendeleza biashara wewe mwenyewe?

2. Je upo tayari kufanya kazi kwa muda mrefu bila ya kuwa na uhakika ni kitu gani unapata?

3. Je unauzoefu wowote kwa biashara unayokwenda kufanya? Kama huna je upo tayari kujifunza kwa kupata mafunzo na kujifunza kwa wanaofanya?

4. Je unamtaji wa kutosha kufanya biashara ianze na pia uweze kuendelea na maisha mengine?

5. Ni fedha kiasi gani unaweza kuweka kwenye biashara kutoka kwenye mfuko wako mwenyewe? Ni fedha kiasi gani utahitaji kupata kama mkopo?

6. Je unajua sehemu ambayo unaweza kupata mkopo wa kuendeleza biashara yako? Na unajua vigezo na sifa za kupata mkopo?

7. Ni mapato kiasi gani unategemea kupata kwenye biashara yako kwa mwaka wa kwanza na hata baada ya hapo?

8. Je unaweza kuishi bila ya kutoa fedha yoyote kwenye biashara kwa matumizi kwenye miezi sita ya mwanzo?

9. Je unafikiria kufanya biashara hiyo na mtu mwingine au unapendeleakufanya mwenyewe? Kama utahitaji mshirika unafikiri awe na sifa gani ili muweze kwenda vizuri?

10. Je biashara unayotaka kuanzisha ina soko kwenye eneo unalotaka kufanyia?

11. Biashara nyingine kwenye eneo hilo zipo katika hali gani? Zina mafanikio au zinaelekea kushindwa?

12. Je unategemea biashara yako kutanuka zaidi na kuenda kwenye maeneo mengine kuacha hapo unapofanyia sasa?

13. Je wewe ni mtu unayejituma, unaweza kujiongoza mwenyewe na kupanga na kutekeleza mipango yako mwenyewe?

14. Je unaweza kuwahamasisha wateja na hata wafanyakazi wako kufanya kazi zaidi na vizuri?

15. Je unaweza kufanya maamuzi magumu na ukayasimamia?

16. Je wewe ni mtu unayeaminika? Watu wanakuamini kulingana na maneno na vitendo vyako?

17. Je afya yako inaruhusu wewe kuweza kukabiliana na mikiki mikiki ya biashara?

18. Je umeandaa mchanganuo wa biashara yako(business plan)? Je una mpangilio kamili wa biashara yako itakavyokwenda?

19. Vipi kuhusu ulinzi wa biashara yako? Je unafikiria kukatia bima ili ikitokea tatizo uweze kufidiwa?

20.Je unao mfumo mzuri wa kutunza mahesabu kwenye biashara yako? Je unayemtu wa kukuandalia mahesabu kwenye biashara yako?

Kwa nini baadhi ya biashara zinafanikiwa na nyingine zinashindwa?

Kumbuka kwamba biashara nyingi zinashindwa na kufa kwa sababu ya usimamizi mbaya. Wamiliki wengi wa biashara husingizia vitu vingine kama mtaji, ushindani, eneo baya au uchumi pale ambapo biashara zao zinaposhindwa. Sababu zote hizi sio za kweli.

Sababu ya kweli inayosababisha biashara nyingi kushindwa ni usimamizi mbovu wa wamiliki wa biashara. Mara nyingi wamiliki wanashindwa kujua ni aina gani hasa ya biashara wanayofanya na wanawezaje kuikuza zaidi. Wakati mwingine kushindwa kunasababisha na bidhaa au huduma inayotolewa kutokidhi mahitaji ya wateja.

Ukiweka pembeni sababu kama mtaji au nyingine ambazo watu wengi wanasingizia, biashara yoyote itashindwa ikiwa;

1. Usimamizi ni mbovu.

2. Matumizi mabaya ya fedha.

3. Kukosa wafanyakazi wenye uwezo.

4. Bidhaa au huduma inayotolewa kutokuwa na thamani inayotegemewa.

5. Kutokuijua vizuri biashara unayofanya.

6. Kushindwa kulifikia soko.

Anza maisha mapya ya utajiri na mafanikio.

Amua sasa ya kwamba biashara unayofanya au unayokwenda kufanya ndiyo itakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa. Amua kwamba utatumia uwezo wako mkubwa, vipaji na ubunifu ulionao na kwamba utavumilia mpaka pale ambapo utafikia mafanikio makubwa.

Utashangaa kuona ni jinsi gani mafanikio yatakavyokuja kwako na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisah yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.