Kwa kila hatua utakayochukua kwenye maisha yako itatengeneza nguvu na nguvu hiyo itakusukuma kuelekea kwenye mafanikio au kuelekea kwenye kushindwa. Kuna nguvu za asili ambazo zikitumiwa vizuri zinaleta mafanikio na zikitumiwa vibaya zinasababisha kushindwa.
Kuna nguvu nne zinazoweza kukuletea mafanikio kama ukizijua na kuzitumia vizuri.
Nguvu ya kwanza ya mafanikio; Mara zote kuwa muaminifu.
Uaminifu ni nguvu kubwa sana ya kufikia mafanikio. Watu wengi wanafikiri ili kufanikiwa kwenye biashara ni lazima udanganye, uibe, uchukue au kutoa rushwa na vitendo vinginje visivyo vya uaminifu. Japokuwa vitendo hivyo vinaweza kuleta mafanikio ya muda mfupi, mwishoni mtu hupata matatizo makubwa sana. Uaminifu utakupatia mafanikio makubwa, japo itakuchukua muda mrefu lakini mafanikio yako yatadumu kwa muda mrefu na utakuwa na amani na utulivu wa nafsi.
Kuna nguvu kubwa sana ya mafanikio inayotengenezwa na uaminifu. Kila unapochagua kuwa muaminifu unajiweka kwenye njia inayoelekea kwenye mafanikio. Kila unapochagua kutokuwa muaminifu unajitoa kwenye njia inayoelekea kwenye mafanikio.
Kuna baadhi ya watu sio waaminifu ila wanaonekana kuwa na mafanikio makubwa. Ndio inawezekana lakini ukiyachunguza maisha yao kwa ndani unakuta wana matatizo makubwa sana. Unaweza kuona wamefanikiwa sana kwenye biashara ila kwenye maisha ya familia wameshindwa, unakuta wana magonjwa makubwa, pia unaweza kukuta wana majuto makubwa na hivyo kushindwa kufurahia mafanikio yao.
Kuanzia leo fanya biashara zako au shughuli zako zote kwa uaminifu, sema ukweli na utajenga msingi imara sana wa kufikia mafanikio makubwa.
Nguvu ya pili ya mafanikio; Furahia kushindwa kwako.
Unaweza kushangaa lakini moja ya nguvu kubwa ya kufikia mafanikio ni kushindwa. Kila mara unaposhindwa unatengeneza nguvu ya kukupeleka kwenye mafanikio. Kuelewa hili vizuri chukua mfano wa mtoto mdogo ambaye anaanza kutembea. Mtoto anapoanza kutembea hupiga hatua chache na kisha kuanguka, je hubaki pale alipoanguka? Hapana, huinuka na kutembea tena. Hapo pia huanguka lakini anainuka na kujaribu tena na tena mpaka anaweza kutembea na hatimaye kukimbia. Hivyo ndivyo ilivyo kwa wewe kufikia mafanikio, mwanzoni utashindwa kama ukiendelea kujaribu bila ya kukata tamaa baadae utafanikiwa na kufikia mafanikio makubwa. Ila ukikubali pale unaposhindwa mara ya kwanza hutaweza kufikia chochote kwenye maisha yako.
Wengi wetu tunaogopa sana kushindwa na tuko tayari kufanya jambo lolote ili tusishindwe na moja ya mambo watu wanayofanya ili wasishindwe ni kutokujaribu kabisa. Tatizo jingine kubwa ni kwamba watu wengi hawajifunzi kutokana na kushindwa badala yake wanakata tamaa. Kwa kujifunza ni nini ambacho kimesababisha ukashindwa utaweza kujua ni kipi ambacho kitakufikisha kwenye mafanikio.
Tunaposema furahia kushindwa kwako hatumaanishi uchague ukishindwa ili uweze kufanikiwa. Badala yake tunamaanisha uelewe kwamba kushindwa ni sehemu ya mafanikio na hivyo inapotokea kwako usikate tamaa bali jifunze kupitia kushindwa huko.
Nguvu ya tatu ya mafanikio; Yatumie matatizo yako.
Matatizo unayopitia yanaweza kuwa moja ya nguvu kubwa sana ya kukufikisha wewe kwenye mafanikio. Kila tatizo lina fursa iliyojificha ndani yake. Hadithi kubwa za mafanikio zinatokana na watu waliotumia matatizo yao na kuyageuza kuwa fursa kubwa ya kufikia mafanikio.
Kwa tatizo lolote unalokutana nalo, kwanza kubali una tatizo halafu lichunguze tatizo hilo kwa makini na utaona fursa iliyojificha ndani ya tatizo hilo. Liangalie tatizo lako kwa mtizamo tofauti na utaona fursa nyingi unazoweza kuzitumia kwenye tatizo hilo.
Kama utaendelea kuona tatizo lako kama tatizo utashindwa, ila kama ukiliangalia tatizo kama fursa utafikia mafanikio makubwa sana.
Nguvu ya nne ya mafanikio; Kusanya nguvu zako.
Kama umewahi kuchukua lensi au kioo cha miwani na kukiweka kwenye jua, kama ukiweza kuikusanya miale ya jua kwenye sehemu moja unaweza kuwasha karatasi moto kwa kutumia miale hiyo iliyokusanywa. Hii ndio nguvu kubwa inayopatikana na kukusanya kitu. Hii pia inawezekana kwenye kufikia mafanikioa, unaweza kufikia mafanikio makubwa kama utachagua maeneo machache ambayo unaweza kuyafanyia kazi vizuri na kuelekeza nguvu zako zote kwenye maeneo hayo. Usijaribu kufanya kila kitu, utaishia kufanya juu juu na hutaweza kufikia mafanikio makubwa. Chagua mambo machache ambayo utayafanya kwa ufanisi mkubwa na yatakuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Usiyumbishwe na kutaka kufanya mambo mengine mazuri unayoyaona, yatakutoa kwenye njia ya mafanikio.
Amua leo ni mambo mangapi unataka kufanya na wekeza nguvu zako zote kwenye mambo haya na jizuie usiende kufanya mambo mengine. Kwa njia hii utaona jinsi gani unaweza kufikia mafanikio makubwa.
Falsafa za mafanikio.
Kuna falsafa za mafanikio ambazo zinakwenda zaidi ya nguvu hizi nne za mafanikio tulizojifunza. Kama ukijifunza falsafa hizi na kuzikumbuka kila mara kwenye maisha yako zitakusaidia kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kama ukichanganya falsafa hizi na nguvu hizo nne za mafanikio hakuna kitakachoweza kukuzuia kufikia mafanikio makubwa.
1. Usikubali ufahari wako uharibu biashara yako.
Kila mmoja wetu anaufahari fulani ambao anajichukulia(ego), ufahari huu humfanya mtu asikubali kuwa amefanya makosa. Kama usipoweza kutumia ufahari huu vizuri utakupelekea kufanya maamuzi ambayo yataumiza biashara yako. Moja ya matumizi mabaya ya ufahari wako ni kulipiza kisasi. Unapokuwa na mawazo ya kulipiza kisasi unakuwa na mawazo haribifu kwako na kwa yule unayetaka kumlipizia kisasi.
2. Kuwa mtaalamu uliyebobea.
Kwa chochote kile unachofanya kazana uwe mtaalamu uliyebobea. Jifunze kila kitu kinachohusiana na biashara au kazi unayofanya. Jinsi unavyojua sana ndivyo unavyoweza kufikia mafanikio makubwa. Kwa mfano kama una duka linalouza ngozi, kuwa mtaalamu wa ngozi. Jua viwanda vinavyotengeneza ngozi, jua ubora wa ngozi, jua hatua za kutengeneza ngozi na pia pata taarifa za teknolojia mpya inayoingia kwenye ngozi.
3. Usikate tamaa.
Maisha yana kila aina ya vikwazo , kushindwa na kukatishwa tamaa. Kama ukiweza kuvuka vikwazo hivi na kuendelea na safari ni lazima utafikia mafanikio makubwa. Kama ukikubali vikwazo hivyo na kukata tamaa huwezi kufikia mafanikio.
4. Maisha yanabadilika.
Kitu pekee ambacho hakibadiliki kwenye maisha ni mabadiliko, yaani kila kitu kinabadilika jinsi muda unavyokwenda. Na hata biashara yako nayo inabadilika. Ushindani, teknolojia, uchumi, wateja vyote vinabadilika kila wakati. Kujua mabadiliko haya na uelekeo wa mabadiliko utakuwezesha kuchukua hatua mapema ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.
5. Fanya kwa ubora wa hali ya juu.
Chochote unachofanya kwenye kazi au biashara yako fanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Toa majibu ambayo yana kiwango cha juu sana na kumnufaisha yule anayetumia. Kwa njia hii utaweza kushindwa ushindani wowote utakaoibuka kwako. Usikubali kufanya kazi ya kawaida tu kama wengine wanavyofanya. Kuwa bora zaidi na fanya kazi yenye ubora wa hali ya juu sana.
Kuna usemi mmoja unasema kama wewe sio namba moja au namba mbili kwenye biashara unayofanya, achana na biashara hiyo maana inakupotezea muda. Kwa biashara yoyote ambayo umeamua kufanya, wekeza kila kitu chako kuhakikisha kwamba unakuwa bora zaidi na inakuwa namba moja. Inawezekana, chukua hatua.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.