Katika maisha yako ya kila siku kuna maamuzi mengi sana ambayo unayafanya. Maamuzi unayoyafanya yanaweza kuwa na athari kubwa kwenye kufikia mafanikio makubwa.
Fikiria maamuzi makubwa mabayo umewahi kufanya kwenye maisha yako. Je ulipitia hatua gani kufanya maamuzi hayo? Je wakati unafanya maamuzi hayo ulikuwa katika hisia gani? Je unafikiri kuna maamuzi sahihi ambayo unatakiwa kuyajua au upo tayari kufanya maamuzi yoyote ukiamini mambo yatakuwa mazuri?
Katika kufanya maamuzi mara nyingi tunaongozwa na hisia mbili;
1. Hofu ya kupoteza. Hii ni hofu ambayo unaipata kwa kuhisi kwamba kama ukifanya maamuzi kuna kitu fulani utakipoteza. Hofu hii hukufanya uchelewe au uache kabisa kufanya maamuzi. Kwa mfano unaweza kuwa umepanga utaacha kazi na kwenda kujiajiri lakini kila ukifikiria unaona ukiacha kazi utapoteza mshahara na marupurupu mengine. Hivyo unaweza usifanye maamuzi hayo kabisa.
2. Tamaa ya kupata zaidi. Hii ni hisia ambayo inatokana na tamaa ya kupata zaidi. Kila mtu anapenda kupata zaidi ya alichonacho na katika kufanya maamuzi unaweza kuhisi kwamba utanufaika sana kwa kufanya maamuzi hayo. Hisia hii hukusukuma ufanye maamuzi haraka.
Ni vyema kuwa makini na hisia hizi mbili kwa sababu ukiendekeza hisia ya hofu utashindwa kufanya maamuzi na kukosa fursa na pia ukiendekeza hisia ya tamaa unaweza kufanya maamuzi mabovu na baadae ukajutia.
Maamuzi mabovu huwa yanafanyika katika hali zifuatazo;
1. Maamuzi ni makubwa au ya muhimu sana.
2. Madhara ya kufanya maamuzi hayo hayajulikani.
3. Maamuzi hayawezi kurudiwa yakishafanyika.
4. Maamuzi inabidi yafanyike haraka sana.
5. Maamuzi yanafanyika kwa hofu na wasiwasi mkubwa.
Epuka hali hizi wakati wa kufanya maamuzi ili uepuke kufanya maamuzi mabaya ambayo yatakufanya baadae ujutie.
Jinsi ya kufanya maamuzi sahihi.
Kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia wakati wa kufanya maamuzi na hivyo ukaweza kufikia maamuzi sahihi. Baadhi ya njia hizo ni;
1. Kubali uhalisia.
Kubali kwamba kuna mambo ambayo huwezi kuyabadili kwenye maisha. Hivyo hivyo wakati wa kufanya maamuzi jua ni mambo gani huwezi kubadilisha na kubaliana na hali halisi.
2. Jiangalie mwenyewe.
Jichunguze wewe mwenyewe na ujue ni kiasi gani tatizo lililopo mbele yako linaathiri maisha yako. Pia jua ni hisia gani zinazokusukuma au kuzuia kufanya maamuzi hayo ili uweze kufanya maamuzi mazuri.
3. Lichunguze tatizo zaidi.
Kumbuka kwamba tatizo unalolijua umeshalitatua nusu. Hivyo badala ya kukimbilia kufanya maamuzi wakati unakutana na tatizo fulani hebu kwanza lijue tatizo hilo vizuri ili uweze kufanya maamuzi sahihi.
4. Fikiri aina zote za masuluhisho.
Kabla ya kufanya maamuzi juu ya tatizo lolote fikiria kwanza aina mbalimbali za masuluhisho. Katika aina hizo mbalimbali zichanganue zote na kisha angalia moja ambayo ni bora ndio ufanye maamuzi.
5. Usiendeshwe na hisia.
Hakikisha wakati unafanya maamuzi hauendeshwi na hisia zozote. Huwezi kukwepa hisia, lazima zitakuja ila zitambue na kisha ziepuke wakati unafanya maamuzi. Fanya maamuzi yako kwa kuzingatia tatizo lenyewe, na aina za masuluhisho uliyofikia.
Usikimbilie kufanya maamuzi ambayo badae yanaweza kukugharimu. Tumia njia hizi kufanya maamuzi kwenye maisha yako ya kawaida na hata ya kazi au biashara.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.