Karibu msomaji kwenye kipengele hiki cha kujenga tabia za mafanikio ambapo mwezi huu wa tisa tunajifunza kuhusu nidhamu binafsi.

Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita nidhamu binafsi ni uweze wa kufanya jambo unalotaka kufanya bila ya kujali unajisikia kulifanya au la. Pia tuliona nidhamu binafsi ni muhimu sana kwako kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kama huna nidhamu binafsi unaweza tu kusahau kuhusu mafanikio kwa sababu nidhamu binafsi ndiyo inayokuwezesha kuendelea na malengo na mipango yako hata wakati mambo yamekuwa magumu.

Leo tutajifunza jinsi ya kujenga nidhamu binafsi na kama ukifuata hatua hizi utaanza kuona mabadiliko kwenye maisha yako. Kuna hatua sita muhimu za kufuata ili uweze kujijengea nidhamu binafsi. Hatua hizo ni;

1. Jijue wewe mwenyewe.

Hatua ya kwanza kabisa kwenye kujenga nidhamu binafsi ni kujijua wewe mwenyewe. Jua ni maeneo gani kwenye maisha yako ambayo umekosa nidhamu binafsi. Jiulize ni mambo gani ambayo sasa hivi huyafanyi au unayaahirisha kila mara ila kama ukiyafanya yatakuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Chukua kitabu chako cha kuandikia malengo na uandike mambo matatu makubwa ambayo kama ukiweza kuyafanya vizuri utafikia mafanikio unayotarajia. Pia andika ni sababu zipi zinazokufanya mpaka sasa hufanyi mambo hayo.

2. Kuwa na malengo ya muda mrefu.

Je ni kitu gani unataka kupata au kifikia kwenye maisha yako? Kwa kuwa na malengo ya muda mrefu na kujua faida utakayoipata ukifikia malengo hayo itakufanya uweze kuanza kufanyia kazi malengo yako. Kwa mfano kama unataka kufanya mazoezi, malengo yako yatakuwa kuwa na afya bora, kuishi muda mrefu na kuweza kufanya kazi ili kufikia malengo mengine. Kwa kuangalia faida hizi za muda mrefu kutakuwezesha kufanya mazoezi kila siku bila ya kukata tamaa. Yafanye malengo yako yakusukume kufanya kitu leo ili uweze kuyafikia.

3. Tenga muda maalumu wa kufanya jambo.

Katika mambo matatu uliyoandika ambayo ni muhimu kwako ili kufikia mafanikio yapangie muda maalumu wa kuyafanya kila siku na uhakikishe unafanya mambo hayo kwenye muda huo. Kwa mfano kama unataka kujifunza zaidi kwa kujisomea, weka utaratibu kwamba kila siku unaamka saa kumi na moja na nusu saa ya kwanza utajisomea. Fanya hivi kila siku angalau kwa miezi miwili na itakuwa tabia yako ya kudumu.

Muhimu sana ni kuweka ratiba ya kufanya jambo kila siku na katika muda ule ule na ikiwezekana ufanyie kwenye sehemu ile ile, hii itakurahisishia kujenga tabia husika. Kama huwezi kutumia muda mrefu, anza kidogo halafu utaendelea kuongeza muda kadiri siku zinavyokwenda.

4. Anza kutenda.

Ni rahisi sana kufanya mambo hayo tuliyojadili hapo juu, kila mtu anaweza kupanga na kila mtu anapanga, lakini ni wachache sana wanaoweza kufanya yale wanayopanga. Sasa wewe usiwe mmoja wao. Anza kufanya hayo uliyopanga kufanya mara moja. Kama hujui uanzie wapi anza kesho kwa kujisomea kitabu kitakachokuongezea ujuzi kulingana na shughuli unayofanya.

Vitendo ni muhimu saa, anza kufanya kidogo halafu ongeza kadiri siku zinavyozidi kwenda.

5. Jipe zawadi.

Kama ukiwea kufanya yale uliyopanga kufanya utaweza kufikia malengo yako, hii ni zawadi kubwa ila iko mbali sana. Ili kukuwezesha kuendelea kufanya jambo unalotaka kufanya jipe zawadi kila unapokamilisha hatua ndogo ndogo. Chagua kitu ambacho unapenda sana, halafu jinyime kitu hiko mpaka uwe umekamilisha mpango uliojiwekea. Kwa mfano kama unapenda kunywa soda, jiwekee mpango kwamba kama utaweza kusoma kwa saa moja kila siku ndio unaweza kunywa soda, ukishindwa basi hutakunywa soda. Hii itakuwezesha kujijengea nidhamu ya kufanya kile ulichopanga kufanya.

6. Pata ushirikiano kutoka kwa wengine.

Kama tulivyowahi kujifunza, maisha yako ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Hivyo tabia zako hazitofautiani sana na watu ambao unakuwa nao muda mrefu. Kama unataka kujenga tabia fulani au kufanya kitu fulani tafuta watu wanaofanya ili uweze kuenda nao pamoja. Hii itakufanya uweze kufanya jambo hilo hata kama hujisikii kwa sababu usipofanya utawaangusha wengine ambao unafanya nao. Kwa mfano kwa wanachama w GOLD kwenye KISIMA CHA MAARIFA kuna group la WHATSAAP ambapo inaweza kuwa sehemu nzuri sana ya kukutana na watu ambao wanafanya jambo ambalo na wewe unataka kulifanya na hivyo mkaweza kulifanya.

ZAWADI; Kwa mwanachama wa GOLD kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambaye anataka kujenga tabia ya kuamka mapema au kujisomea au kuandika awasiliane nami na tutafanya pamoja. Mimi huwa naamka saa kumi asubuhi, nasoma nusu saa au saa moja na ninaandika sio chini ya maneno elfu moja. Hii ni kila siku. Usiogope huna haja ya kufanya kwa kiasi kikubwa kama mimi, tayari nimezoea, kwa anayetaka ataanzia kuamka isiwe zaidi ya saa kumi na moja, kusoma isiwe chini ya nusu saa na kama unaandika isiwe chini ya maneno mia mbili. Natoa nafasi tano tu kwenye hili, kama unahitaji kupata nafasi hii wasiliana nami kwa 0717396253 au email amakirita@gmail.com

Kujenga nidhamu binafsi sio kazi rahisi ila inawezekana kama kweli una nia ya kufikia mafanikio. Anza kufanya mambo hayo sita na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Utakutana na changamoto nyingi sana kwenye kufanya mambo hayo, ukiweza kuzivuka ndio utafikia mafanikio.

Nakutakia kila la kheri kwenye kujenga tabia zitakazokufikisha kwenye mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.