Watu wengi wenye mafanikio makubwa kiuchumi  huwa ni watu wa kufanya mambo fulani ambayo huwa siyo rahisi kufanywa na watu wengine ambao hawana mafanikio. Kwa kufanya mambo hayo huweza kuwaongoza moja kwa moja kufikia mafanikio makubwa katika maisha yao.
Na mara nyingi watu hawa wenye mafanikio makubwa, kwao inakuwa ni vigumu kuweza kuacha kufanya mambo hayo. Huwa ni watu wa kufanya mambo hayo karibu kila siku na kila mara. Katika makala hii utajifunza mambo hayo muhimu ambayo yanafanywa na watu wenye mafanikio. Hata wewe unaweza ukayafanya ili yakusaidie kusonga mbele.
Fuatana nasi katika makala hii kuyajua mambo hayo zaidi:-
1. Kujifunza.
Hili ndilo hitaji la kwanza la watu wenye mafanikio. Maisha yao kwa sehemu kubwa yametawaliwa na kujifunza. Hawachoki kuchota maarifa sehemu tofauti tofauti ambayo wanaona yatasaidia kutimiza ndoto zao. Hiki ni kitu ambacho ukiwaambia waache siyo rahisi kukuelewa. Wamekeza sana katika kujifunza mambo muhimu ya kimafanikio. Ni tabia ambayo imewapelekea kuwafikisha kwenye mafanikio makubwa sana.
2. Kuweka vipumbele.
Siri nyingine ya watu wenye mafanikio ipo kwenye kuweka vipaumbele. Ni wawekaji wazuri wa mipango yao kwa kuzingatia vipaumbele zaidi. Na ni kitu ambacho kinawafanikisha katika kufikia malengo yao. Kwani watu hawa wamegundua kuwa bila kuweka vipaumbele ni wazi kabisa malengo yao mengi yatakuwa ni vigumu kufikiwa. Hili ni jambo pia ambalo linafanywa sana na watu wenye mafanikio makubwa.
3. Kujitoa mhanga.
Mafanikio yote waliyonayo yanategemea tabia hii ya kujitoa mhanga ambayo wanayo. Siku zote ni watu wa kujitoa mhanga na hawaogopi kitu chochote ambacho kinaweza kuwazuia katika safari yao ya kuelekea kwenye mafanikio. Ukiwachunguza vizuri utagundua kwamba kujitoa mhanga ni sehemu ya maisha yao na ni kitu ambacho lazima wakifanye.
4. Kujaribu.
Kujitoa kwao mhanga haitoshi, pia wanajipambanua kuwa ni watu wa kujaribu sana mambo mengi na kila wakati. Inapotokea wameshindwa katika jambo mojawapo si wepesi sana wa kukata tamaa zaidi hujipanga upya kwa ajili ya kufanya jambo jingine jipya litakalowaletea manufaa zaidi katika maisha yao. Kwa kifupi hawa ni watu wa kujaribu zaidi hadi kufanikiwa.
5. Kuuliza.
Watu wenye mafanikio siku zote hujiuliza sana watawezaje kutoka hapo walipo na kwenda ngazi nyingine kimafanikio. Huwa siyo tu wasikilizaji au wapokeaji wa moja kwa moja, pia hupata muda wa kuuliza. Kuuliza huku mara nyingi hujiuliza kichwani mwao na mwisho wa siku hupata majibu ya kile wanachokitaka na kuendelea na safari ya mafanikio.
6. Kutafuta msaada.
Kama unataka kupotea katika njia ya mafanikio, jifanye mjuaji. Watu wenye mafanikio katika maisha yao kwa sehemu kubwa wao si wajuaji. Ni watu wa kuheshimu na kupenda kujifunza kutoka kwa wengine na kutafuta msaada pale inapohitajika. Huwa siyo watu wakujifanya wanajua kila kitu. Na huwa hawachoki kutafuta msaada kila siku ambao wanaona  ni muhimu kwao.
7. Kutoa.
Watu wenye mafanikio siku zote hawachoki katika suala zima la utoaji. Ni watu ambao mara kwa mara hutoa kile wanachoona kinaweza kuwa msaada kwa wengine. Ni jambo ambalo hulifanya sana na wewe mwenyewe ni shahidi juu ya hili jinsi ambavyo huweza kutoa tena kwa sehemu kubwa. Kutoa ni sehemu muhimu katika maisha yao.
8. Ni watu wa shukrani.
Hiki ni kitu ambacho watu wenye mafanikio huwa hawachoki kukifanya. Pale wanapofanyiwa jambo zuri huwa ni wepesi sana wa kutoa shukrani kwa wale wote waliowafanyia hivyo. Ni moja ya tabia nzuri sana ambayo wamejijengea siku zote za maisha yao.
9. Kusamehe.
Inapotokea wamekosewa na wengine kwa namna moja ama nyingine, huwa ni watu wa kusamehe. Ndani ya mioyo yao ni watu wa kutolipa kisasi. Wamejijengea tabia ya kusamehe ambayo wanaiendeleza siku hadi siku katika maisha yao. Hivyo hujikuta wakiwa ni watu wa kuishi kwa uhuru sana.
10. Kumaliza kile wanachokianza.
Watu wenye mafanikio si waanzaji tu wa mambo mapya mengi, bali pia ni watu wa kumaliza kile walichokianza. Wanapopanga mipango yao ni lazima mwisho wa kumaliza wauone na ndicho kitu ambacho kinakuwa kinafanyiika mpaka kufikia ndoto zao.
Kwa kuhitimisha makala hii, mpaka hapo bila shaka umeshatambua, ili ufikie mafanikio makubwa ni muhimu kujifunza kufanya mambo kama wanayofanya watu wenye mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Tunakutakia safari njema ya mafanikio iwe ya ushindi kwako, endelea kutembelea AMKAMTANZANIA kujifunza kila siku.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,