Habari mpenzi msomaji wa makala hii. Na karibu tena leo uongeze maarifa katika ubongo wako na chakula cha ubongo ni maarifa, kama vile wewe unavyokula chakula kila siku na akili vivyo hivyo inahitaji maarifa kila siku ili iweze kukua. Leo tutajifunza tabia ambazo haziwezi kukufikisha wewe katika kilele cha mafanikio yoyote yale katika maisha.

UNAJIONDOA KWNEYE MAFANIKIO WEWE MWENYEWE.

 
Hizi ndizo tabia 4 (Nne) ambazo haziwezi kukufikisha katika kilele cha mafanikio yoyote yale;
1. Kuogopa Changamoto
Changamoto ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Sijawahi kuona mtu ambaye anapata kitu kiurahisi bila kukumbana na changamoto katika kile anachofanya. Changamoto zipo kila sehemu na hupaswi kuziogopa cha msingi ni kujipanga ili kukabiliana nazo katika maisha. Ata useme ujipange vizuri namna gani hazikwepeki. Kama wewe ni mtu ambaye unaogopa changamoto ni kazi kwako sana kufikia mafanikio. Unashindwa kujaribu kwa sababu ya kuogopa changamoto wapo watu ambao wana mawazo mazuri ya kuboresha maisha yao lakini wanaogopa changamoto utaendelea mpaka lini kujipanga na kuogopa changamoto katika maisha ya leo? Kama una ndoto yako ya kufanya jambo fulani ambalo litabadili maisha yako lifanye sasa na wala usiogope kujaribu endelea kuthubutu kila siku bila kuchoka na kukata tamaa bali chukua hatua stahiki ambazo zitafanya uwe na furaha siku zote. Kila binadamu ana matatizo yake hapa duniani na matatizo hayaishi hivyo basi simama imara katika kile unachofanya kipende ,weka juhudi na maarifa na fanya kwa ubora wote ili ufanikiwe.
SOMA; Sheria 6 Za Mafanikio Na Jinsi Zinavyoweza Kukuongoza Kufikia Mafanikio Makubwa.
2. Mtu Ambaye Haishiwi Sababu au Malalamiko
Kuna watu wao kazi yao ni kutoa sababu tu. Kila siku malalamiko hayaishi bila kuchukua hatua yoyote ile. Kuna watu hawataki kusikia mabadiliko yoyote katika maisha katika jambo lolote lile yeye lazima atoe sababu ya kutowezekana, watu wanajiwekea sababu na vikwazo vingi kabla hata ya kufanya jambo lolote lile anatafuta sababu hasi za kushindwa na siyo sababu chanya katika kushindwa. Je utawezaje kufanikiwa kama umeshaipa akili yako mawazo ya kushindwa? Muda mwingine usipoteze muda wako kumtafuta mchawi wa maisha yako mchawi wa maisha yako ni wewe mwenye na dereva wa maisha yako ni wewe mwenye jinsi unavyoendesha maisha na jinsi yalivyo ni matokeo yaliyosababishwa na wewe mwenye.
Kwa hiyo, ukitaka mabadiliko acha sababu na malalamiko kwanza. Fanya kazi kwa vitendo na siyo kwa mdomo acha kulalamika kila siku chukua hatua chanya leo ya kutatua matatizo au tatizo linalo kukabili. Kila siku unakuwa ni mtu wa sababu kuchelewa kufika eneo fulani ambalo ulipaswa kufika kwa muda fulani unaanza kutafuta sababu ya kutoa kwa nini ulichelewa badala ya kuchukua hatua kwa nini kila siku unachelewa kazini. Kama wewe ni mtu wa sababu ni ngumu kuleta mabadiliko katika maisha yako iwe ni katika familia yako, biashara, kazi yako na kadhalika. Toa thamani yako na wewe utalipwa kulingana na thamani unayotoa. Kila anayetoa hupokea na anayetafuta anapata na wahenga wanasema mkaa bure siyo sawa na mtembea bure.
3. Mtu Ambaye Anasikiliza Maneno ya kila Mtu
Kuna watu wanakosa raha sana kutokana na maneno ya watu kabla hujaanza kusikiliza maneno ya watu ambayo yanakukatisha tamaa jiulize kwanza maneno ya watu yana faida gani kwako? Yanakuingizia chochote kwa siku kama unapata faida katika kusikiliza maneno ya kila mtu endelea kama hupati faida acha kuwasiliza na wakimbie mara moja. Maneno ya watu ni sumu ndio na ukiyasikiliza huwezi kufika mbali. Unaogopa kufanya jambo fulani zuri la kubadili maisha yako kwa sababu ya maneno ya watu kuendelea kuishi maisha ya kutofanya mabadiliko na kuogopa jamii inayokuzunguka inasema nini ni hatari. Wako watu wanakatishwa tamaa kwa kila jambo analojaribu kufanya hii ni kwa sababu ya kumpa kila mtu nafasi ya kumsikiliza badala ya kuchagua watu wachache ambao wamefanikiwa katika kile ambacho unataka kufanya wewe na kuomba ushauri kutoka kwao na kujifunza kutoka kwao. Ukiruhusu kusikiliza maneno ya kila mtu utaishia pabaya. waswahili wanasema miluzi mingi humpoteza mbwa. Acha kuhangaika tafuta kweli, nayo kweli itakuweka huru.
Acha tabia ya kusikiliza maneno ya kila mtu utapotea njia.
SOMA; Anayetakiwa Kutafutwa Sana Kila Kona Kwa Dunia Ya Sasa Ni Nidhamu.
4. Mtu Ambaye Si Mwaminifu
Kwanza kabisa uaminifu unalipa hapa duniani. kukosa uaminifu ni ngumu kwako kufanikiwa unakosa uaminifu katika muda, katika kazi ,biashara ,familia yako nakadhalika. Kukosa uaminifu katika maisha ni kukosa nidhamu katika maisha. Nidhamu ni daraja katika mafanikio yoyote yale ya mwanadamu nidhamu binafsi ambayo unahitaji kujiongoza mwenyewe bila ya kusimamiwa na mtu. Wako watu hawawezi kufanya jambo peke yao mpaka wasimamiwe na mtu akumbushwe wajibu wake. Kama wewe umekosa uaminifu basi huna nidhamu acha tabia ya kujidanganya mwenyewe ishi maisha yako acha kuigiza maisha kuishi maisha yako yatakupa furaha na furaha itakuletea mafanikio. Watu wamekosa uaminifu siku hizi wametawaliwa na uongo tu na ukiwa mwongo uwe na kumbukumbu ya kukumbuka kama ulidanganya. Usitoe ahadi kama wewe huwezi kuitekeleza toa ahadi ambayo unaweza kuitekeleza kulingana na nafasi yako katika maisha. Kukosa uaminifu katika muda itakugharimu sana pale utakapofanya kazi na jamii ambayo inajali muda utakosa fursa nyingi kwa sababu ya kutokuwa mwaminifu.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com