Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.
Katika masomo sita ambayo Robert aliahidi kutufundisha katika kitabu hiki, somo la nne ni historia ya kodi na nguvu ya mashirika.
Robert anasema anakumbuka alipokuwa shuleni mwalimu alikuwa anawapa hadithi ya Robinhood, mtu ambaye alikuwa anawaibia matajiri na kuwapa masikini. Mwalimu wake alikuwa anamuona Robinhood kama shujaa ambaye aliwasaidia masikini. Rich dad hakumuona Robinhood kama shujaa, bali kibaka. Japokuwa Robinhood alishapita muda mrefu, bado wafuasi wake wanaendelea kuishi. Watu wengi wanafikiri na kusema matajiri inabidi walipe kodi nyingi. Ni mawazo haya ndio yamesababisha mpaka sasa masikini na tabaka la kati wanalipa kodi nyingi kuliko matajiri.
Kuelewa vizuri kinachoendelea tunatakiwa kujua historia ya kodi. Zamani sana hakukuwa na kodi ya moja kwa moja kwa wananchi. Wananchi walianza kutozwa kodi uingereza na marekani wakati wa vita ili kusaidia nchi kushinda vita. Baada ya muda kodi hizi zilifanywa kuwa sheria na mwanzoni kodi walikuwa wanalipa matajiri tu. Watu wengi walifurahia na kukubali sheria ya kodi kwa sababu waliambiwa itakuwa inawaumiza matajiri. Lakini baadae imekuwa kinyume chake, maana inawaumiza masikini na tabaka la kati kuliko inavyowaumiza matajiri.
Rich dad anasema serikali inapokua ndio matumizi yanaongezeka na hivyo kutafuta mbinu zaidi za kupata fedha na hivyo kuongeza kodi zaidi. Rich dad alimwambia Robert kwamba matajiri walielewa umuhimu wa mashirika kuanzia kipindi cha usafirishaji wa meli. Anasema mashirika hayo yaliwasaidia kuepuka kufilisika kwa sababu kama shirika likifa tajiri anakuwa amepoteza fedha alizowekeza tu na hivyo fedha zake binafsi kuwa salama. Katika hili la kodi, matajiri wamewazidi ujanja wasomi.
Matajiri wanawazidije ujanja wasomi?
Rich dad anasema wakati kodi inaanzishwa iliwalenga matajiri tu. Lakini serikali ilivyoendelea kukua, iliongeza kodi na kuchukua mpaka kwa masikini kabisa. Ni katika wakati huu ambapo matajiri waligundua na kuanza kutumia nguvu ya mashirika kuepuka kodi kubwa. Rich dad anasema mashirika yanawalinda matajiri, pia anasema shirika sio kitu kikubwa, ni faili tu lenye nyaraka za kisheria linalobeba usajili wa kitu fulani. Shirika linamlinda mmiliki asilipe kodi nyingi kwa sababu kiwango cha kodi kwa mashirika ni kidogo ukilinganisha na cha mtu binafsi.
Rich dad anasema vita hii ya kodi kati ya matajiri na masikini mara zote masikini wamekuwa wanashindwa ila hawajui kama wameshindwa. Hivyo huendelea kuamka asubuhi kwenda kazini na kufanya kazi kwa nguvu sana huku wakiendelea kulipa kodi kubwa sana. Hawajifunzi mbinu nzuri za kuwawezesha kufanya kazi kwa kiwango na kulipa kodi kidogo.
Rich dad anasema mara zote matajiri huangalia mbinu za kupunguza kodi. Huajiri wanasheria wazuri kuangalia sheria na jinsi ya kuzitumia kwa faida yao wenyewe. Anasema masikini wao wanaendelea kufanya kazi na huku wakilipa kodi zaidi, jinsi kipato kinavyoongezeka ndivyo kodi nayo inaongezeka. Rich dad anasema siri kubwa ya matajiri ni kumiliki mashirika au kampuni.
Robert anasema baba yake alikuwa anamshauri atafute kazi nzuri kwenye shirika kubwa na kisha aanze kupanda ngazi kuelekea nafasi za juu kwenye shirika hilo. Alipomwambia rich dad, alimwambia kuliko kutengemea kupanda ngazi kwa nini usimiliki ngazi yako mwenyewe? Alimwambia kutegemea kazi za kuajiriwa ni sawa na ng’ombe anayesubiri kukamuliwa.
Katika miaka ya ishirini Robert alianza kufanya kazi na ndipo elimu hii ilipoanza kumuingia vizuri. Kila alipofanya kazi na kipato chake kuongezeka ndivyo makato nayo yaliongezeka. Na hapa ndipo alipoanza kukumbuka alichoambiwa na rich dad na akajiuliza namfanya nani kuwa tajiri?
Mwaka 1974 akiwa bado ameajiriwa Robert alianzaisha kampuni yake ya kwanza. Na akaanza kujifunza na kuijua biashara yake vizuri. Japo alikuwa na ASSETS chache aliwekeza muda wake mwingi kuongeza assets na kukuza kampuni yake. Aliendelea kufanya kazi kwa nguvu sana, japo makato yaliendelea kuwa makubwa lakini aliweza kuongeza assets kwenye kampuni yake. Kampuni yake ilikuwa ya kuuza na kupangisha nyumba.
Chini ya miaka mitatu, Robert alikuwa anapata fedha nyingi kwenye kampuni yake kuliko aliyokuwa anapata kutoka kwenye ajira yake. Na hivyo fedha hizo zilikuwa zinatokana na fedha zake kumfanyia kazi na sio yeye kufanya kazi moja kwa moja. Aliweza kununua gari lake la kwanza kwa faida aliyopata kwenye kampuni hiyo. Robert anasema elimu ya fedha ndio ilimwezesha kufikia uhuru wa kifedha. Na amekuwa akiwafundisha watu mambo hayo kila anapopata nafasi ya kuongea na watu. Robert anasema kwamba elimu ya fedha inatokana na ujuzi wa maeneo makubwa manne;
1. Hesabu za fedha, ni muhimu sana kujua mapato na matumizi na mzunguko mzima wa fedha kwenye biashara. Kwa kuwa na ujuzi huu itakuwezesha kujua kama kampuni inakua au inakufa.
2.Uwekezaji, hii ni sayansi ya fedha kutengeneza fedha. Hii inahitaji ubunifu zaidi.
3. Kulijua vizuri soko, hapa unatakiwa kujua mahitaji na usambazaji.
4. Sheria. Hapa ni muhimu kujua sheria na jinsi ya kuzitumia kufanikiwa. Kwa mfano kwa kuwa na kampuni unakuwa na nafuu kubwa kwenye kodi kuliko mtu aliyeajiriwa.
Robert anasema kampuni/shirika linaweza kufanya mambo mengi sana ambayo mtu binafsi hawezi kufanya. Kwa mfano mtu aliyeajiriwa hukatwa kodi kabla hata hajapokea mshahara wake ila kampuni hulipa kodi baada ya kulipa gharama zake zote.
Tunajifunza nini hapa?
1. Kodi ilianzishwa ili kuwaadhibu matajiri ila kwa sasa inawaadhibu masikini.
2. Jinsi unavyofanya kazi zaidi na kipato kuongezeka ndivyo kodi nayo inaongezeka.
3. Kumiliki kampuni unakuwa kwenye unafuu wa kodi kuliko aliyeajiriwa.
4. Elimu ya fedha ni muhimu sana kwako ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha.
5. Katika elimu ya fedha kuna vitu vinne unatakiwa kuvijua vizuri; hesabu za fedha, soko, uwekezaji na sheria.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia uhuru wa kifedha.
TUKO PAMOJA.
Nitawezaje kutengeneza mfumo mzuri utakao nisaidia kwenye Hesabu za fedha,
kujua mapato na matumizi na mzunguko mzima wa fedha kwenye biashara yangu?
Ernest Lwilla.
LikeLike
Wapo watu wanatengeneza application za stock management, lakini gharama za wengi huwa juu, ambapo utakuta mpaka kila kitu kikamilike siyo chini ya milioni moja,
Sasa hiyo inaweza isiwe rafiki kama bado biashara ni ndogo.
Hivyo unaweza kutengeneza excel template ambayo utaweka bidhaa zako na kuweza kufuatilia vizuri.
Ukishakuwa vizuri unaweza kuwekeza kwenye app za stock management.
LikeLike