Katika sehemu hii tutajifunza mambo mawili muhimu;

1. Jinsi ya kuweka malengo ya fedha kwenye maisha.

2. Jinsi ya kuendeleza ujuzi ulionao ili kufikia malengo yako ya kifedha.

Kuweka malengo yako ya kifedha.

Kuna malengo manne ya kifedha unayoweza kujiwekea. Malengo hayo ni;

1. Malengo ya kipato. Haya ni malengo ya kipato ambacho unataka kupata kwa kipindi fulani. Kwa mfano unaweza kuweka lengo kwamba kwa mwaka unataka kutengeneza kipato ambacho ni tsh milioni 100. Unaweka malengo haya ukijua ya kwamba kwa kupata kiwango fulani cha fedha mipango yako mingine ya maisha itakwenda vizuri.

2. Malengo ya umiliki. Hapa unaweka malengo ya mali kiasi gani uwe unamiliki. Hapa unazungumzia mali zinazozalisha au zenye thamani kwa mfano biashara, uwekezaji, fedha ulizoweka akiba benki na kadhalika. Malengo ya umiliki unaweza kuanza kidogo na ukaongeza kadiri muda unavyokwenda.

3. Kipato kwenda kwenye uwekezaji. Haya ni malengo ambapo unatumia kipato chako cha ziada kuwekeza kwenye mali nyingine zaidi. Mtu anayeweka malengo haya hujikuta akipata faida kubwa kuliko kuweka tu fedha benki.

4. Mali kwenda kipato. Haya ni malengo ambapo unapata kipato kutoka kwenye mali zako au uwekezaji wako. Katika malengo haya unakuwa na uwekezaji ambao unakupatia kipato cha kukutosha wewe na kuendeleza uwekezaji wako. Ni katika hatua hii ambapo unaweza kuwa hufanyi kazi kubwa lakini unapata kipato kikubwa sana.

Jua ni aina ipi ya malengo ya kifedha unaweza kuanza nayo na kuanza kuelekea kwenye uhuru wa kifedha.

Kuendeleza ujuzi wako.

Kila binadamu anayeishi ana ujuzi fulani ambao watu wako tayari kumlipa kwa ujuzi huo. Hapo ulipo unao ujuzi au uzoefu fulani ambao kama ukiweza kuutumia vizuri utaweza kulipwa fedha nzuri na ukaanza safari yako ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha.

Chukua karatasi na uandike vitu vyote ambavyo unaweza kufanya. Kama umeajiriwa fikiria kazi ambazo unazifanya kwenye ajira yako. Pia fikiria vitu ambavyo unavipenda na hata vipaji vyako. Fikiria kitu chochote ambacho umewahi kumfanyia mtu na akafurahi sana kwa jinsi ulivyofanya vizuri. Inaweza kuwa ni kuuza, inaweza kuwa ni mipangilio, inaweza kuwa ni kuongoza au kingine chochote.

Katika vitu vyote ulivyoorodhesha anza kupitia kimoja kimoja. Angalia ni vitu gani ambavyo unahitaji elimu zaidi ili kuviendeleza. Pia angalia ujuzi ulioorodhesha na ujibu maswali yafuatayo;

1. Je unajionaje uwezo wako katika kila ujuzi? Mzuri sana, mzuri au kawaida?

2.Ni ujuzi upi ambao unahitaji kuendeleza kidogo tu?

3. Ni ujuzi gani ambao unajisikia ufahari kuwa nao?

4. Ni ujuzi gani ambao utakuletea mafanikio unayotazamia?

5. Ni aina gani ya elimu unayoweza kuipata kuendeleza ujuzi wako?

Katika kuendeleza ujuzi wako unaweza kupata elimu kutoka sehemu mbalimbali;

1. Uzoefu kutoka kwa waliokutangulia.

2. Kujiandikisha kwenye kozi inayofundishwa na taasisi fulani.

3. Kujisomea mwenyewe kwa kitafuta vitabu vinavyohusika na unachotaka kuendeleza na kujifunza.

Angalia muda wako na uwezo wako ili uweze kuchagua njia nzuri ya wewe kujiendeleza.

Ujuzi unaohitaji ili kufanikiwa.

Bila ya kujali unafanya nini na bila ya kujali malengo yako kwenye maisha ni nini, kuna ujuzi ambao kila mtu anayetaka kufanikiwa kwenye maisha anatakiwa kuwa nao. Ujuzi huo ni;

1. Kuweza kujiongoza na kujihamasisha mwenyewe.

2. Kupangilia muda na kazi zako.

3. Kufanya utafiti na kujaribu wazo lako.

4. Kupokea na kutumia taarifa za kifedha.

5. Kuwa na uhusiano mzuri na watu.

6. Kuwahamasisha wengine kukusaidia wewe.

7. Kufanya maamuzi.

8. Kuwashawishi wengine wafanye kile ambacho unataka wafanye.

Ujuzi huu ndio unaotakiwa kuuendeleza ili kuweza kutumia fursa ulizokonazo kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.