Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.

Katika masomo sita ambayo Robert aliahidi kutufundisha katika kitabu hiki, somo la tano ni matajiri wanavumbua fedha.

Robert anasema amekuwa anafundisha kwanzia mwaka 1984, anasema ni kazi nzuri sana ila pia imempa simanzi kubwa sana. Anasema simanzi hii anaipata kwa sababu katika maelfu ya watu aliofundisha kila mmoja ana uwezo mkubwa sana ndani yake ila bado wanashindwa kuutumia uwezo huo. Na wanashindwa kuutumia uwezo huo kwa sababu hawajiamini wao wenyewe.Robert anasema baada ya kumaliza somo, mtaani kinachopima mafanikio sio maksi za darasani bali udhubutu wa mtu kuchukua fursa na kuzitumia vizuri.

Anasema woga na kutojiamini ndio kinawafanya watu wengi kushindwa kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yao na hivyo kushindwa kufikia uhuru wa kifedha. Anasema watu wengi wanajua nini wanatakiwa kufanya ili wafanikiwe ila hawana udhubutu wa kuchukua hatua. Robert anasema kwenye madarasa aliyokuwa anafundisha alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake kujifunza kuishinda hofu, kuwa na udhubutu na kushukua mazingira hatarishi(risk). Anasema kwa watu wengi linapokuja swala la fedha watu wengi wako tayari kucheza salama(play safe).

Robert anasema watu wengi wameridhika na elimu walizo nazo na hawaoni umuhimu wa kujifunza elimu ya fedha. Kwa kukosa elimu hii ya fedha wanajikuta hawana machaguo mengi na hivyo fursa nyingi kuwapita. Anasema kwa wale ambao hawajiendelezi kwa elimu ya fedha wako katika wakati mbaya sana kwa sasa kwa sababu mambo yamebadilika sana. Miaka 300 iliyopita ardhi ilikuwa utajiri, na mwenye ardhi ndio alikuwa tajiri mkubwa. Baadae vikaja viwanda na hivyo waliokuwa na viwanda ndio wakawa matajiri wakubwa sana. Sasa hivi ni zama za taarifa, wenye taarifa sahihi na kwa muda sahihi ndio ambao wanakuwa matajiri sasa. Tatizo kubwa ni kwamba taarifa zinasambaa haraka sana na hivyo kwa wanaochelewa kuzipata wanakosa nafasi ya kunufaika nazo.

Robert anasema mawazo ya zamani ni mzigo mkubwa sana kwa anayeyatumia. Mambo ambayo yalikuwa yanalipa zamani sasa hivi hayalipi tena.Teknolojia imebadilika sana na hivyo wanaongangania mawazo ya zamani wanakosa nafasi nyingi za kuboresha maisha yao.

Katika kufundisha huku Robert alianzisha mchezo ambao wanafunz wake walikuwa wanaucheza huku wakijifunza elimu ya fedha. Mchezo huo uliitwa CASH FLOW BOARD GAME. Siku moja mwanafunzi wake mmoja alikuja na rafiki yake kwenye mafunzo na hivyo akapata nafasi ya kucheza mchezo ule. Kwa kuwa hakuwa na elimu ya fedha ilikuwa vigumu sana kwake kuelewa mchezo ule na hivyo alikasirika na kuondoka. Robert anasema hivi ndivyo inavyotokea kwenye maisha ya watu wengi, kwa kuwa hawana elimu ya fedha hujikuta wanachukua maamuzi ambayo yanawagharimu au yanawakosesha fursa nzuri.

Robert anasema kwanzia mwaka 1984 amekuwa akitengeneza fedha kwa kufanya kinyume na mfumo wa elimu. Anasema mfumo wa elimu mwalimu anamwelezea mwanafunzi lakini kwenye mafundisho yake mwanafunzi anajifunza mapungufu yake kwa kucheza mchezo. Anasema mchezo ule ulikuwa unawafanya watu kujua mapungufu yaliyopo ndani yao. Pia ulikuwa unawafundisha watu jinsi ya kuweza kuchukua na kutumia fursa zilizopo mbele yao.

Anasema kwenye maisha kuna watu ambao wanapata fedha sana ila hawaoni wakifikia maendeleo, hii ni kwa sababu hawajui jinsi ya kutumia fedha zao. Wanakuwa na chaguo moja tu na hivyo kukosa fursa nyingi. Pia kuna watu ambao wanaziona fursa nyingi ila wanalalamika hawana fedha. Hawa wanakuwa hawajui jinsi ya kutumia fedha za wengine kuweza kufikia malengo yao. Anasema watu wengi wanafursa zilizopo mbele yao ila hawazioni, baada e wanapokuja kuziona kila mtu anakuwa ameshaziona na hivyo kuwa hazina thamani kubwa tena. Robert anasema lengo la elimu ya fedha ni kukupa wewe machaguo zaidi ili uweze kuziona fursa nyingi zaidi na kuzifanyia kazi.

Matajiri wanatengeneza fedha.

Tokea wakiwa wadogo, rich dad alikuwa akimwambia Robert na Mike kwamba fedha sio kitu halisi. Aliwaambia masikini na tabaka la kati wanafanya kazi kupata fedha ila matajiri wanafanya kazi kutengeneza fedha. Jinsi mtu anavyoamini kwamba fedha ni kitu halisi ndivyo anavyozidi kufanya kazi ili kupata fedha nyingi zaidi. Na jinsi mtu anavyojua kwamba fedha sio kitu halisi ndivyo anavyoweza kuwa tajiri haraka.

Robert na mike walimuuliza rich dad kama fedha sio halisi ni kitu gani basi? Rich dad aliwaambia mali kubwa tunayomiliki ni uwezo wetu wa kufikiri. Uwezo wako wa kufikiri unaweza kutengeneza utajiri mkubwa sana. Robert anatoa mfano rahisi wa jinsi ya kutengeneza fedha; anasema mwaka 1990 uchumi ulikuwa mgumu sana na watu wengi walikuwa wanashauriwa kuweka akiba kwa muda mrefu. Yeye aliamua kutumia fedha aliyokuwa anayo kuizungusha na kupata fedha nyingi zaidi. Alinunua nyumba zilizokuwa zinauzwa kwa bei rahisi, kuzirekebisha na kuuza kwa bei kubwa. Wakati mwingine alikuwa anakopa fedha anakwenda kununua nyumba, halafu anaiuza na kurudisha deni na hivyo kubaki na faida kubwa. Robert ansema hivi ndivyo alivyoweza kutengeneza fedha kwa kutumia akili yake.

Robert anasema kwa kutumia akili mtu yeyote anaweza kuzitumia fursa nyingi zinazopatikana pale alipo.

Tunajifunza nini hapa?

1. Kila mtu ana uwezo mkubwa sana ndani yake ila hofu na kutokujiamini ndio kunawazuia watu wengi kutumia uwezo wao.

2. Baada ya kuhitimu masomo, mafanikio kwenye maisha hayapimwi kwa ufaulu wa darasani.

3. Kulikuwa na zama za ardh, zikaja zama za viwanda na sasa ni zama za taarifa.

4. Wenye taarifa sahihi na kwa wakati sahihi ndio wanaokuwa matajiri.

5. Fedha sio kitu halisi, masikini wanafanyia kazi fedha wakati matajiri wanatengeneza fedha.

6. Kila mtu anaweza kutengeneza kama atatumia akili yake na kufikiri vizuri.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.