Katika tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa watu matajiri na wenye mafanikio makubwa imeonekana kwamba karibu kila mmoja ambaye amefikia mafanikio makubwa ametumia siri saba kufikia mafanikio hayo.
Leo tutajifunza siri hizo saba na kama ukianza kuzitumia hakuna kitakachoweza kukuzuia kufikia mafanikio makubwa.
1. Malengo na maono makubwa.
Watu wote waliofanikiwa walikuwa na malengo makubwa ya kufikia hatua fulani. Watu hawa waliangalia mazingira yaliyowazunguka na kujiuliza wanawezaje kuyabadili na kishakuweka malengo ya kuyabadili. Ni kwa njia hii tumeweza kupata uvumbuzi mkubwa sana duniani.
Tumeshajadili sana kuhusu malengo, na mpaka sasa nina hakika kwamba tayari unayo malengo ya maisha yako. Kama huna au kama hujayaandiaka mahali popote nikupe pole.
2. Rasilimali/kujiendeleza.
Watu wote waliofikia mafanikio makubwa waliweza kujiendeleza na kujiweka katika hatua ya kuweza kutumia vizuri fursa zilizokuwa mbele yao. Watu hawa waliweza kufikia mafanikio licha ya kuwepo kwa hali ngumu au kukatishwa tamaa. Hawakusubiri mtu aje awaoneshi jinsi ya kutumia fursa walizoziona, walijaribu wenyewe na kila waliposhindwa walitumia kama njia ya kujifunza zaidi.
Anza sasa kujiendeleza na kujifunza zaidi juu ya kile unachofanya au unachotaka kufanya ili kusifikia mafanikio yako. Kama ni biashara hakikisha unaijua vizuri na unaifanya kwa viwango vya juu sana.
3. Kuwa na imani kwao wenyewe.
Watu waliofikia mafanikio makubwa walikuwa wanajiamini sana na hawakuwa na shaka yoyote kwamba wanaweza kushindwa. Ni watu ambao wanaamini wanaweza kufanya na kufikia malengo waliyojiwekea. Imani hii isiyotetereka ndio inawawezesha kuvuka nyakati ngumu na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.
Amini kwamba unaweza kufikia mafanikio makubwa sana. Amini kwamba wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa sana. Usianze kujishukua u kuhisi kwamba huwezi kufikia kule unakotaka kufika. Amini bila ya kuyumbishwa na imani yako itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
4. Nguvu ya taswira.
Watu waliofikia mafanikio makubwa waliweza kupata taswira ya kile ambacho wanakitaka. Waliweza kujiona tayari wanamiliki vitu walivyotaka kumiliki au tayari wana nafasi ambazo walikuwa wanataka kuzifikia. Kwa kujijengea taswira hizi kwenye akili zao iliwawezesha kufikia malengo yao.
Anza kutengeneza taswira ya kile unachotaka kwenye maisha yako. Kama unataka kuwa na gari fulani jione tayari upo kwenye gari hiyo. Kama ni mafanikio makubwa kwenye biashara jione tayari upo kwenye biashara hiyo. Inashauriwa kila siku upate muda wa kukaa kimya na kisha kupitisha picha hiyo kwenye akili yako. Kwa kufanya hivi unatengeneza mazingira ya kukufikisha kwenye malengo unayotaka kufikia.
5. Kukusanya nguvu.
Watu waliofanikiwa sana waliweza kukusanya nguvu zao na kuzielekeza kwenye mambo machache. Kwa kufanya hivi waliweza kutumia nguvu zao kukamilisha mambo hayo na hatimaye kufikia mafanikio makubwa. Kama tulivyoona kwenye mfano wa lensi na jua, ukiukusanya mwanga wa jua kwa kutumia lensi unaweza kuunguza karatasi. Huu ni mwanga ule ule ambao ulikuwa hafifu ila ulipokusanywa umekuwa na nguvu kubwa.
Kusanya nguvu zako kwenye malengo yako machache ambayo unataka kuyafikia. Usijaribu kufanya vitu vingi au usifanye kila kitu. Fanya vitu vichache ambavyo vitakuletea mafanikio makubwa sana, vingine ajiri watu wengine wa kuvifanya.
6. Hamu kubwa.
Watu waliofikia mafanikio makubwa walikuwa na hamu kubwa sana ya kufikia mafanikio hayo. Hamu hii iliweza kuwasukuma na kuwajengea shauku kubwa iliyowawezesha kuvuka vikwazo na kufikia mafanikio makubwa. Hamu kubwa ya kutaka kurahisisha usafiri ndio iliyowafanya watu kugundua ndege.
Tengeneza hamu kubwa ya kufikia malengo uliyojiwekea. Hamu hiyo ikusukume na kukujengea shauku kubwa ya kutaka kufikia kile unachotaka. Hamu hiyo iwe kama inakuunguza na kukufanya ujitume zaidi.
7. Nia njema.
Watu waliofikia mafanikio makubwa walikuwa na nia njema sana ya kuleta mabadiliko mazuri kwenye jamii zao. Hawakusukumwa na sababu binafsi au tamaa ya kunufaika wao wenyewe, walitaka kuona maisha yanakuwa rahisi kwa watu wengine na hii ikawawezesha kufikia mafanikio makubwa sana.
Kuwa na nia njema ya wewe kufikia malengo yako. Usitake tu fedha ili uishi kifahari, taka kuleta mabadiliko makubwa kwa watu wanaokuzunguka na dunia kwa ujumla. Kwa njia hii utaweza kufikia mafanikio makubwa sana.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.