Kujenga nidhamu binafsi sio kazi rahisi. Kuna changamoto nyingi sana ambazo utakutana nazo na kama hujajipanga vizuri unaweza kukata tamaa na kuacha kabisa. Wiki iliyopita tulijadili jinsi ya kujenga nidhamu binafsi. Baada ya kujua hayo leo tutajifunza mambo muhimu ya kuazingatia wakati wa kujenga nidhamu binafsi.

Hapa kuna mambo matano muhimu sana ya kuzingatia wakati wa kujenga nidhamu binafsi ili uweze kufikia malengo yako.

1. Jielewe wewe mwenyewe.

Kujaribu kujenga nidhamu binafsi kabla hujajielewa mwenyewe ni sawa na kufanya kazi bure. Hii ni kwa sababu utajiona kama unajitesa na hivyo kushindwa kuendelea. Ni lazima uelewe ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Na pia ni lazima uweze kuweka uhusiano kati ya nidhamu binafsi unayotaka kujenga na mafanikio unayotaka kufikia. Kwa njia hii utaweza kuendelea hata pale mambo yanapokuwa magumu.

2. Jifuatilie wewe mwenyewe.

Wakati unajenga nidhamu binafsi mara kwa mara utakuwa unashindwa na kujikuta unarudia tabia ulizopanga kuacha. Ni vizuri sana kama utaweka utaratibu wa kujifuatilia mwenyewe kwa sababu hii itakuwezesha kujua wakati ambapo unarudia kufanya yale uliyopanga kuacha. Ukishajigundua kwamba unarudi nyuma ndio unaweza kujirekebisha.

3. Jitoe kwa ajili ya nidhamu binafsi.

Unapopanga kwamba unajenga nidhamu binafsi unatakiwa kujitoa kweli ili kuweza kufikia nidhamu binafsi. Kwa mfano unapopanga utaamka saa kumi asubuhi, inabidi ukubaliane na maamuzi yako kisha uwe tayari kuamka muda huo. Na unapoamka muda huo usione kama ni mzigo bali ufurahie kwa sababu itakusaidia kufikia ndoto zako.

4. Kuwa na uthubutu.

Kama tulivyoona kujenga nidhamu binafsi sio kazi rahisi hata kidogo. Utakutan na vikwazo na vishawishi vingi sana. Ni muhimu sana kuwa na uthubutu ili kuweza kujenga na kuendeleza nidhamu binafsi. Ni lazima uwe na uthubutu wa kukataa raha ya muda mfupi ili kuweza kufikia furaha ya milele. Ni lazima uwe na uthubutu wa kuvumilia mateso ya muda mfupi ili kuwa na maisha bora baadae.

5. Jiongoze mwenyewe.

Katika safari yako ya kujenga nidhamu binafsi unahitaji kuongozwa na kushikwa mkono. Lakini katika jamii zetu ni vigumu sana kupata mtu wa kukuongoza. Hivyo inakubidi uweze kujiongoza mwenyewe. Ongea na nafsi yako na jipe moyo kwamba mambo yatakwenda vizuri sana. Jikumbushe malengo yako na umuhimu wa wewe kuwa na nidhamu binafsi na pia jitengenezee ujasiri.

Haya ndio mambo matano ya kuzingatia wakati wa kujenga nidhamu binafsi. Yafanye kila siku na utaweza kujenga nidhamu binafsi itakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri kwenye kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.