Mwaka 1995 Robert alikuwa kwenye mahojiano na mwandishi wa habari. Mwandishi huyo alimwambia Robert angependa kuwa mwandishi mzuri na anayeuza kama yeye. Robert anasema kwa kuangalia makala alizokuwa anaandika zilikuwa nzuri sana. Robert alimwambia una staili nzuri ya kuandika, nini kinakuzuia kufikia malengo yako? Mwandishi alimjibu kazi yake haikuonekana kumfikisha kwenye malengo yake. Alimuiliza Robert kama ana ushauri wowote.

Robert alimshauri mwandishi yule ajifunze kozi ya masoko na uuzaji(sales and marketing), na alimuelekeza sehemu nzuri ya kujifunza hayo. Mwandishi yule alimuuliza Robert kwa mshangao, unamaanisha nikasome sales? Robert akamwambia ndio. Mwandishi yule alimwambia Robert kwamba yeye ana mastars degree ya english na ni mtaalamu wa lugha hiyo, kwa nini aende kusomea kuhusu kuuza(sales)? Robert alimuonesha kitabu chake akamwambia soma kimeandikwaje? Kimeandikwa Robert Kiyosaki, Best Selling Author, akamwambia kwa nini hakikuandiwka best writing author? Robert alimwambia kwamba yeye sio mwandishi mzuri sana ila anajua jinsi ya kuuza na hiyo ndio imewezesha kufikia mafanikio makubwa. Mwandishi yule alisema hawezi kujifunza kuwa muuzaji na hivyo akaondoka.

Dunia imejaa watu ambao wana akili na vipaji vya hali ya juu. Lakini licha ya vipaji hivyo bado vipato vyao ni vidogo sana. Robert anasema mshauri mmoja wa biashara aliyebobea kwenye maswala ya afya alikuwa anamwambia jinsi gani madaktari na watu wengine wa afya wanavyoteseka na fedha. Anasema wako karibu sana na fedha ila hawajui jinsi ya kuzifanya ziwe zao.

Kama tulivyoona kwenye sura zilizopita, elimu ya fedha inaunda na vitu vinne muhimu, hesabu za fedha, uwekezaji, soko na sheria. Ukijifunza vitu hivi vinne unaweza kufikia uhuru wa kifedha kupitia chochote unachofanya. Linapokuja swala la fedha, kitu pekee ambacho wengi wanakijua ni kufanya kazi kwa nguvu.

Kwa mfano yule mwandishi angejifunza kuhusu soko na uuzaji angeweza kunufaika zaidi na uandishi wake. Robert anashauri njia nyingine nzuri ya kujifunza ni kuchukua kazi kwenye kile unachopenda na kisha kufanya kazi hiyo kujifunza. Kujufunza kupitia kazi unaelewa haraka na unakuwa mtaalamu mzuri. Hivyo kwa yeyote ambaye anataka kujua vitu vingi vitakavyomwezesha kufikia mafanikio, afanye kazi ili kujifunza na sio kupata tu fedha.

Tatizo la Utaalamu na Kubobea.

Robert anasema mfumo wa elimu unatukuza utaalamu ili kufikia mafanikio. Yaani ili mtu afikie mafanikio makubwa inabidi atafute eneo ambalo atabobea. Ndio maana madaktari husoma udaktari kwa ujumla na baadae kubobea kwa mfano madaktari wa wanawake, watoto n.k Robert anasema mfumo wa elimu unawafanya watu kujifunza zaidi na zaidi kwenye vitu vichache sana. Rich dad alimshauri yeye kufanya kinyume, yaani asijifunze vitu vichache, bali ajifunze vitu vingi. Alimwambia unatakiwa kujifunza vichache kwenye vitu vingi sana. Alimwambia ajifunze kuhusu benk, masoko, uuzaji, uongozi, biashara za kimataifa na kadhalika.

Robert anasema wakati wanafunzi wenzake walikuwa mapumziko ya likizo, yeye alikuwa anajifunza biashara, watu na tamaduni mbalimbali. Anasema hii ilimfanya kukua sana kiufahamu. Rich dad alimwambia kazi ngumu kwenye kuendesha kampuni ni kuweza kuwaongoza watu. Alimwambia ni muhimu sana kujifunza mbinu za uongozi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Hii ilimfanya Robert kuomba kazi kazi ya kuwa wakala wa mauzo(salesman) wa kampuni ya Zerox, ambapo alikuwa akizunguka sehemu mbalimbali kutafuta wateja wa bidhaa. Rich dad alifurahia hatua hiyo, ila baba yake alikasirishwa sana kwa sababu anafikiria kazi ya uuzaji ni ya watu ambao hawana elimu.

Robert anasema kazi mbalimbali alizofanya zilimpa elimu na uzoefu mkubwa ambao mpaka sasa annautumia kwenye kuendesha biashara zake.

Tunajifunza nini hapa?

1. Watu wengi wana ujuzi wa taaluma yao ila hawana ujuzi wa biashara hivyo wanashindwa kufanikiwa.

2. Ni muhimu sana kujifuza masoko na mauzo(sales and marketing) bila ya kujali ni kazi au biashara gani unafanya.

3. Usifanye kazi ili kupata tu fedha, fanya kazi kujifunza na tumia elimu uliyoipata kwenye biashara zako.

4. Badaya ya kubobea kwenye vitu vichache, jifunze vitu vingi sana.

5. Kuendesha kampuni au biashara ni lazima uwe kiongozi mzuri ndio utaweza kufanikiwa.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.