Kila mtu anapenda kufanikiwa kwenye maisha yake. Na hata kwa wanafunzi, unapokuwa masomoni unapenda kufanikiwa kufikia viwango fulani ulivyojipangia. Unapenda kupata ufaulu mzuri katika masomo na pia unapenda kupata kazi nzuri baada ya kumaliza masomo yako. Yote haya yanawezekana kwako na kwa kila mwanafunzi kama ataijua misingi muhimu ya kufikia mafanikio kwa wanafunzi.

Leo tutajadili misingi muhimu ya kufikia mafanikio kwa wanafunzi. Kupitia misingi hii mwanafunzi yeyote anaweza kufurahia maisha yake ya elimu na baadae kupata mafanikio makubwa kwenye maisha pia.

Elimu ni nzuri sana, ipate na jifunze vizuri. Pia maisha yako ya kwenye elimu ni muhimu sana. Hapa ndio utakapojifunza kuishi na watu, kujifunza uvumilivu na hata kujifunza jinsi ya kufikia mafanikio. Kwa vyovyote vile pata elimu, hata kama hutaitumia kwenye kazi zako kuna vingi utakuwa umevifaidi.

Hatua za mafanikio kwa wanafunzi.

1. Weka malengo na mipango.

Ni muhimu sana kwa mwanafunzi kuwa na malengo na mipango ya maisha yake. Malengo hayo yawe ya muda mfupi na muda mrefu. muda mfupi yatahusu masomo yaliyoko mbele yako na muda mrefu yatahusu maisha yako na kazi utakazofanya. Kama unapenda kuwa daktari ni lazima uandike kwenye malengo yako na ujue unatakiwa kufanya nini ili uweze kuwa daktari.

2. Jenga shauku kubwa.

Baada ya kuweka malengo, ni muhimu kujenga shauku ambayo itakusukuma kufikia malengo hayo. Ni lazima uwe na shauku kubwa itakayokufanya uone kufikia malengo yako ni kitu muhimu sana kwenye maisha yako.

3. Fikiri kwa usahihi.

Jifunze kutumia akili yako vizuri na kufanya maamuzi sahihi kwako na kwa maisha yako ya shule na ya baadae. Wanafunzi wengi wanashindwa kufanya vizuri kwenye masomo kwa sababu wanashindwa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi. Jua ni kipi unataka kwenye masomo yako kisha hakikisha unakilinda kila unapofanya maamuzi yako.

4. Tengeneza haiba chanya.

Kuwa chanya kuanzia mawazo yako, maneno yako na hata matendo yako. Unapokuwa chanya unaweza kutengeneza marafiki wengi na kukubalika na wengi pia. Kwa kuwa na mtizamo chanya utaona kila kitu kinawezekana na utaweza kufikia mafanikio makubwa sana.

5. Chagua marafiki zako kwa uangalifu.

Kuna usemi unaosema ndege wanaofanana huruka pamoja. Marafiki zako ambao unakuwa nao muda mwingi wana ushawishi mkubwa sana kwako. Hivyo kama marafiki zako ni watu ambao hawana mipango mikubwa kwenye maisha yao, watakurudisha wewe nyuma. Kama marafiki zako hawana shauku kubwa ya kusoma na wewe utakuwa hivyo hivyo. Angalia marafiki zako, je ni watu ambao wanaelekea kule unakotaka kuelekea wewe? Kama ndio endelea kuwa nao, kama sio acha kukaa nao kwa kuda mwingi.

6. Jiamini unaweza.

Pamoja na kwamba unahitaji kuweka malengo na mipango, pamoja na kuwa na shauku kubwa na hata mtizamo chanya, kama hujiamini wewe mwenyewe ni kazi bure. Kama hujiamini kwamba unaweza tayari umeshachagua kushindwa, hata ukijaribu kwa kiasi gani bado utaendelea kushindwa. Hivyo kuwa na imani kubwa ndani yako mwenyewe kwamba unaweza kufikia malengo makubwa uliyojiwekea na hii itakuwezesha kuyafikia.

7. Tatua matatizo yako binafsi.

Ni vigumu sana kuzingatia masomo kama una matatizo binafsi yanayokusumbua. Kila mtu anakutana na matatizo mbalimbali. Lakini kama wewe utakwepa matatizo yako yatakufanya uendelee kuyafikiria na hivyo ushindwe kuzingatia masomo. Yatatue matatizo yako binafsi na baada ya hapo achana nayo na upate muda wa kuzingatia masomo na malengo yako mengine.

8. Kuwa mvumilivu.

Sio kila malengo uliyoweka utayafikia, sio kila mipango uliyopanga utaikamilisha. Na wakati mwingine unaweza kufanya kila ulichoweza kufanya lakini bado mambo yakaenda tofauti na ulivyotegemea. Unahitaji kuwa mvumilivu sana ili uweze kufikia malengo na mipango yako. Hata pale inapotokea umeshindwa usikate tamaa, jaribu tena na tena na tena na kama ukifanya hivi ni lazima utafikia malengo yako.

Hizo ndio hatua muhimu za kufuata wewe mwanafunzi ili uweze kufikia mafanikio kwenye masomo na hata kwenye maisha kwa ujumla. Jinsi unavyoanza mapema kujijengea nidhamu nzuri na tabia hizi muhimu za mafanikio ndivyo unavyoweza kufikia mafanikio makubwa mapema zaidi.

Nakutakia kila la kheri kwenye masomo yako na maisha kwa ujumla.

TUPO PAMOJA.