Habari za leo mwana mafanikio? Karibu kwenye kipengele cha tabia za mafanikio na mwezi huu tunaendelea na kujijengea tabia ya kujiamini. Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita, kujiamini ni muhimu sana ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Kama utakosa kujiamini utakuwa umejiwekea kikwazo kikubwa sana kuweza kufikia mafanikio.

Leo tutajadili madhara ya kujiamini na pia kutokujiamini. Unapokuwa unajiamini kuna mambo yatabadilika kwenye maisha yako. Na pia unapokuwa hujiamini kuna mambo yanabadilika kwenye maisha yako.

Madhara ya kujiamini mwenyewe.

Watu ambao wanajiamini mwenyewe huona mabadiliko haya kwenye maisha yako;

1. Wanakutana na watu wageni ambao wanaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha yao.

2. Hawaogopi kuhusu watu wengine wanavyowafikiria na hivyo kutokujizuia kufanya wanachotaka kufanya.

3. Wana ujasiri wa kujieleza na kutoa mawazo yao na hivyo kuonekana uwezo wao.

4. Wanazungukwa na watu ambao wanapenda kuwa karibu zao.

5. Mawazo yao yanapokelewa na watu wengi kwa sababu watu wengi wanapenda kuwa karibu nao.

6. Wanakuwa viongozi wazuri katika jambo lolote wanalofanya.

7. Wanayapenda na kuyafurahia maisha na hivyo huweza kujaribu vitu vingi vipya na hii kuwafanya kukutana na fursa nyingi.

8. Wana uwezekano mdogo sana wa kupata magonjwa ya akili.

Watu ambao wanajiamini wana mtizamo wa NAWEZA.

Madhara ya kutokujiamini.

Watu ambao hawajiamini wanakuwa na tabia zifuatazo.

1. Hawajiamini wao wenyewe na hawaamini kama wanaweza kufanya jambo kubwa.

2. Wanajiona wameshashindwa kabla hata ya kuanza, na hii huwakatisha tamaa hata wasianze kabisa.

3. Hawawezi kujisamehe makosa yao na hivyo kujutia kwa maisha yao yote.

4. Wanaamini hawawezi kuwa bora zaidi ya walivyo sasa au kama walivyo wengine.

5. Wanaogopa kuonesha ubunifu wao kwa sababu wanaogopa kupingwa au kufikiriwa  vibaya na wengine.

6. Hawatoshelezwi na maisha yao na hivyo hawawezi kuyafurahia.

7. Muda mwingi wanakuwa wenyewe, watu wengi hawapendi kuwa karibu nao.

8. Hutumia muda mwingi kulalamika, kulaumu na kuhukumu wengine.

9. Wanahofia kila kitu na mwishowe wanashindwa kufanya chochote.

10. Wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya akili kama sonona(depression), msongo wa mawazo(stress) na hata hofu iliyozidi(anxiety).

Watu wasiojiamini wana mtizamo wa SIWEZI.

Hayo ndio madhara ya kujiamini na kutokujiamini. Ni dhahiri kwamba kujiamini kuna manufaa makubwa kuliko kutokujiamini. Endelea kujijengea tabia ya kujiamini ili uweze kufikia mafanikio unayotegemea.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.

TUPO PAMOJA.