Wajasiriamali wengi ambao pia ni wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakifanya biashara zao kwa mazoea. Kwa kuwa mtu anawazo zuri linaloweza kutatua matatizo ya watu na wapo tayari kulipia bidhaa au huduma inayotokana na wazo hilo, mjasiriamali anaingia moja kwa moja kwenye biashara bila ya kujali mambo mengine. Ukiwa unafanya hivi unaweza kuona ni rahisi na hakuna tatizo lolote ila unakosa fursa nyingi sana kwa kushindwa kuifanya biashara yako kuwa rasmi.
Unaweza kuianza biashara yako kidogo bila ya kuirasimisha, ila kuna wakati ikifika ni muhimu sana kuifanya kuwa rasmi. Tunaposema kuirasimisha biashara tunamaanisha kufanya biashara hiyo kwa taratibu zinazokubalika, kuisajili, kupata namba ya mlipa kodi, kuwa na leseni na hata kufanyiwa ukaguzi wa mahesabu na mtaalamu wa hesabu za fedha. Ndio kurasimisha biashara yako kutakuongezea gharama zaidi ila pia itakupatia nafasi yawe we kukua zaidi.
Leo tutajadili kwa nini ni muhimu sana wewe kurasimisha biashara yako ndogo.
1. Itakusaidia kupata msaada wa kifedha kwa ajili ya kukuza mtaji. Moja ya sababu kubwa zinazowafanya watu wahangaike kusajili biashara zao ni pale ambapo wanataka kuomba mkopo. Kwa sababu kipindi hiki taasisi inayotaka kukupa mkopo lazima ijihakikishie kwamba biashara yako imeshaweza kudumu angalau kwa miezi sita. Kwa wewe kuirasimisha biashara yako mapema utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata mkopo na hata msaada mwingine wa mtaji. Kwa kuwa utakuwa umeisajili mapema na unafanyiwa mahesabu na mtaalamu unaweza kuionesha taasisi yoyote mchanganuo na mzunguko wako wa fedha kwa kipindi husika. Hii itakufanya uaminike na watu waweze kushirikiana na wewe na hatimaye ukakuza biashara yako zaidi.
2. Utalipa kodi sahihi kulingana na biashara unayofanya na faida unayopata. Mfumo wetu wa kodi kwa sasa hasa kwa wafanya biashara wadogo ni wa kukadiria. Yaani kwenye kodi utakadiriwa ni kodi kiasi gani unatakiwa kulipa kwa mwaka na itabidi uilipe iwe umepata faida au la. Lakini unapokuwa unafanya biashara yako rasmi, na ukawa na mtaalamu wa kukupigia mahesabu na akaunti ya benki ya biashara yako, unaweza kupeleka mahesabu yako ya mwaka kwa mamlaka ya mapato na wao wakakutoza kodi kulingana na faida uliyopata kwenye biashara kwa kipindi hiko. Hivyo unaporasimisha biashara yako unalipa kodi kulingana na faida unayotengeneza.
3. Kupata ulinzi wa biashara yako. Unaporasimisha biashara yako inakuwa rahisi sana kuilinda kwa kuilipia bima. Kuna majanga mengo yanaweza kuikumba biashara yako na hatimaye ukajikuta umebaki bila ya chochote. Unapoamua kufanya biashara yako kitaalamu unaweza kuikatia biashara yako bima au kukatia mali za biashara yako bima. Hii itakulinda pale linapotokea jambo linalokufanya upoteze mali hizo au biashara hiyo. Unaweza kuona hili halina umuhimu ila siku unayojikuta kwenye matatizo ndio unaona umuhimu wa vitu kama bima ni nini.
4. Kuongeza ushirikiano zaidi. Unaporasimisha biashara yako unatoa nafasi yaw ewe kushirikiana na wafanya biashara wengine ambao wanafanya biashara kama unayofanya wewe au wanafanyia biashara zao kwenye eneo ambalo hata wewe unafanyia biashara yako. Ushirikiano huu unaweza kuwasaidia mambo mengi kuanzia kubadili baadhi ya taratibu ambazo zinakuwa kikwazo kwa biashara zenu. Ila kama kila mmoja anafanya biashara yake kwa mazoea ni vigumu sana kukaa pamoja na kutetea au kusimamia jambo linalohusu maslahi na maendeleo yenu kupitia biashara mnazofanya.
Unapokuwa unafanyabiashara kwa mazoea unaweza usione umuhimu wa vitu kama kulipa kodi au kuwa na bima ya biashara yako. Ila vitu hivi haviepukiki, ukikwepa kulipa kodi leo kuna siku watakupata na watakusumbua sana. Ukiona kulipia bima leo ni kupoteza hela, kuna siku utaamka uambiwe biashara yako yote imekubwa na janga kubwa na umebaki mtupu. Kurasimisha biashara yako hata kama ni ndogo itakufanya uweze kuona manufaa makubwa ya biashara hiyo.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.