Napenda kuchukua nafasi hii kuwatakia wajasiriamali wenzangu wote heri ya mwaka mpya 2015. Mwaka huu bado ni mpya kabisa na hivyo una miezi kumi na mbili iliyopo mbele yako. Katika miezi hii inayokuja unayo nafasi ya kukua zaidi kama mjasiriamali na pia katika miezi hii unaweza kubaki hivyo ulivyo au hata biashara yako kufa kabisa.
Katika mwaka huu 2015 kuna biashara nyingi zitakazoanzishwa, huenda na wewe ni mmoja wa watu ambao unapanga kuanza biashara mwaka huu. Na pia kwenye mwaka huu 2015 kuna biashara nyingi ambazo zitakufa, yaani mtu atapata hasara na itampelekea kufunga biashara yake. Swali kubwa la kila mjasiriamali kujiuliza ni kwamba mwaka huu mpya una maana gani kwako? Je unakwenda kukuza biashara yako, unakwenda kubali ulivyo au unakwenda kufunga biashara?
Unahitaji kukaa chini na kufanya tathmini muhimu sana kabla hujaendelea na mwaka huu. Bila ya kufanya tathmini hii muhimu unaweza kujikuta unabaki ulivyo au unafunga biashara yako huku ukisingizia eneo halina biashara au umechezewa mchezo mchafu.
Tathmini muhimu kwa kila mjasiriamali kufanya.
Kwanza kabisa chukua muda wako na pitia mwaka ulioisha. Pitia mwaka huo na uandike ni mambo gani makubwa matano uliyofanikiwa kwenye mwaka huo 2014. Andika ni nini kilikuwezesha kufanikisha mambo hayo na ni kitu gani ulichojifunza katika kufanikisha mambo hayo. Huenda uliweza kufikia kiwango kikubwa cha mauzo, huenda uliongeza biashara nyingine, huenda ulinunua vitendea kazi kwenye biashara yako. Yale mazuri ambayo yamekuwezesha kupata mafanikio yaendeleze mwaka 2015.
Baada ya hapo andika mambo makubwa matano ambayo ulishindwa kukamilisha kwa mwaka 2014. Pia katika mambo haya unaweza kuweka changamoto au matatizo uliyopitia katika kipindi hiko kilichopita. Inawezekana ulipata hasara kubwa, inawezekana kuna watu ulifanya nao biashara wakakutapeli na pia inawezekana ulipata ushindani mkubwa ulioifanya biashara yako iyumbe. Jiulize ni vitu gani vilichangia wewe kushindwa kukamilisha au kuingia kwenye matatizo hayo. Na pia jiulize na mambo gani umejifunza kutokana na matatizo hayo ambayo umepitia kwa mwaka ulioisha 2015. Kumbuka kwamba kama hujajifunza kutokana na matatizo uliyopata au makosa uliyofanya unajiweka kwenye nafasi ya kuyarudia tena kwenye mwaka huu mpya 2015.
Baada ya kufanya tathmini ya mwaka ulioisha sasa tumia muda wako kuuangalia mwaka huu mpya 2015. Muhimu kabisa usianze mwaka huu kama ambavyo watu wengi wamekuwa wanauanza. Usianze kwa kuimba tu mwaka mpya mambo mapya, lazima ujue ni nini unakitaka kwenye biashara yako kwa mwaka huu mpya.
Chagua maeneo matano kwenye biashara yako ambayo unajua kama ukiyafanyia kazi vizuri basi biashara yako itakua kwa kiasi kikubwa sana. Kwenye makala za nyuma niliwahi kuandika kwamba asilimia 20 ya juhudi zako inakuletea asilimia 80 ya mafanikio. Hivyo angalia yale maeneo muhimu kwenye biashara yako na mwaka huu yawekee mkazo. Inaweza kuwa ni mauzo, angalau hii ni kwa kila biashara. Mambo kama huduma nzuri kwa wateja ni muhimu sana kwa kila mjasiriamali na mfanya biashara.
Weka mipango itakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara yako kwa mwaka 2015. Weka vipaumbele na vifanyie kazi, mambo mengine ambayo sio kipaumbele tafuta mtu anayeweza kuyafanya ili wewe upate muda mzuri wa kukuza biashara yako. Huwezi kufanya kila kitu, ila unaweza kufanya vitu vichache kwa ufanisi mkubwa sana. Hakikisha vitu hivi ndio muhimu zaidi kwenye biashara yako.
Kushinda au kushindwa kwenye ujasiriamali kunaanza na wewe mwenyewe. Sababu yoyote itakayokamilisha kushindwa huko ndio unaweza kuilaumu ila kila kitu kinaanza na wewe. Ufanye mwaka 2015 kuwa mwaka wa kushinda na weka malengo na mipango itakayokuwezesha kushinda. Hakuna kitu kinachotokea kwa ajali, kila kitu kinasababishwa, sababisha mafanikio ya biashara yako kwa kujipanga vizuri.
Nakutakia kila la kheri kwa mwaka huu 2015,
TUPO PAMOJA.