Kama isingekuwa tabia ya kuahirisha mambo maisha yako yangekuwa tofauti sana na yalivyo leo. Maisha yako yangekuwa bora sana na huenda ungeshatekeleza baadhi ya ndoto zako. Lakini sisi ni binadamu na mara kwa mara tunaanguka kwenye udhaifu wetu.

Tabia ya kuahirisha mambo inamuathiri karibu kila mtu. Ni rahisi sana kupanga mipango yako halafu wakati wa utekelezaji ukajiambia kwamba utafanya kesho. Na kwa bahati mbaya sana hiyo kesho huwa haifiki. Na kama ni mtu ambaye unafanya biashara au umejiajiri inakuumiza zaidi maana unashindwa kufikia malengo yako. Angalau mtu aliyeajiriwa anaweza kusukumwa na tarahe ya mwisho iliyopangwa kwa yeye kutekeleza jukumu fulani.

Ni kutokana na hali hii ndio maana ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kujua chanzo cha tabia hii ni nini na ni jinsi gani ya kuondokana nayo. Tulishajadili hasara za tabia hii na pia tukajadili jinsi ya kuondokana na tabia hii kwenye makala hizi za tabia za mafanikio.

Leo tutajadili vitu vinavyochochea tabia ya kuahirisha mambo na jinsi ya kuviepuka. Kama ilivyo kwa tabia nyingine, kuna baadhi ya vitu ambavyo vinachochea tabia ya kuahirisha mambo. Yaani kuwepo kwa vitu hivyo inakuwa rahisi sana kwako kushawishika kuacha kufanya kitu ambacho ulikuwa umepanga kufanya. Baadhi ya vitu hivyo ni;

1. Jukumu usilolipenda.

Moja ya vitu ambavyo vinachochea tabia ya kuahirisha mambo ni pale unapojaribu kufanya jukumu usilolipenda au lisilokuvutia. Ili kufikia mafanikio kuna baadhi ya mambo inatulazimu kufanya japokuwa tunaweza kuwa hatuyapendeleo kufanya.

Ili kuepuka kuahirisha jambo kutokana na kutolipenda ni vyema ukalipanga jambo hilo asubuhi na mapema. Yaani hakikisha kitu cha kwanza kufanya kwenye siku ndio hiko, hii itakulazimu kulifanya na kuacha kuzunguka nalo kwenye akili kwa siku nzima.

2. Jukumu halina msaada kwako.

Kuna wakati ambao unajikuta umepewa jukumu la kufanya ambalo halina msaada wowote kwako. Yaani halikusaidii kufikia malengo yako ya muda mfupi au ya muda mrefu. Huenda jukumu hili tunapangiwa na wengine au tunakubali baada ya kuombwa na wengine.

kuepuka majukumu ya aina hii jifunze kusema HAPANA kwenye jambo lolote ambalo unaona haliwezi kuwa na msaada kwako. Kwa kufanya hivi utajipunguzia nafasi ya kuahirisha mambo na pia hutawaangusha wengine ambao watakuwa wanakutegemea wewe utekeleze jukumu fulani.

3. Kukosa muelekeo, uchaguzi.

Kuna wakati ambapo mtu unakosa muelekeo na kujikuta umeshindwa kuchagua mambo machache ambayo utayafanyia kazi. Unakubali kuchukua majukumu mengi ambayo yanakuchosha na hivyo kujikuta huna budi kuahirisha baadhi ya majukumu. Kama unafanyia kazi majukumu mawili kwa wakati mmoja ni vigumu sana kukamilisha hata moja na hivyo kujikuta unaahirisha yote. Kumbuka mtu anayekimbiza sungura wawili hawezi kukamata hata mmoja.

Ili kuepuka kukosa muelekeo chagua majukumu machache ambayo unaweza kuyafanyia kazi na fanyia kazi kitu kimoja kwa wakati. Ukishakamilisha jukumu moja ndio uende kwenye jukumu jingine.

4. Kuhisi kuzidiwa.

Kuna wakati ambao unaangalia jukumu lililopo mbele yako na kukosa nguvu kabisa. Unaona jukumu ni kubwa sana na hujui hata uanzie wapi hivyo inakuwa rahisi kwako kuahirisha. Majukumu ya aina hii ni kama kumla ng’ombe, ni ngumu lakini inawezekana.

Ili kuepuka majukumu makubwa kukushawishi kuyaahirisha kawa jukumu kubwa katika sehemu ndogo ndogo unazoweza kuzifanyia kazi. Jua ni sehemu ipi unaweza kuifanyia kazi, ni sehemu ipi unaweza kuwapa wengine na ni hatua ipi ya kwanza na ipi itafuata. Kama ilivyo kwenye kumla ng’ombe, unamchinja kisha unakula vipande vya nyama.

5. Hofu.

Hofu ni moja ya vitu vinavyochangia tabia ya kuahirisha mambo. Wakati wowote ambapo unapanga kufanya jambo kubwa kwenye maisha yako mara nyingi huwa unapatwa na hofu kama kweli utaweza mara nyingine unapatwa na hofu je ukishindwa. Hivyo inakuwa rahisi kwako kuahirisha kile ulichopanga kufanya.

Kuondokana na hofu hii ambayo inakufanya uahirishe mambo jaribu kuangalia hofu hii inaahsiria nini. Kama inaashiria kwamba unaweza kushindwa rejea mikakati yako ya jinsi gani utafanya ikiwa utashindwa.

6. Matumizi mabaya ya muda.

Matumizi mabaya ya muda ni chanzo kikubwa cha tabia ya kuahirisha mambo. Kama unafanya jukumu la msingi huku unatumia simu au mtandao ni vigumu sana kulikamilisha na utaishia kuliahirisha. Kama unaanza siku yako kw akufanya majukumu rahisi kila siku utajikuta unaahirisha majukumu magumu ambayo ndio ya msingi sana kwenye maisha yako.

Kuepuka tabia hii ya matumizi mabaya ya muda weka vipaumbele, na panga ratiba zako ambazo utaziheshimu. Pia tenga muda ambao hupati usumbufu wa aina yoyote ambapo utaweza kufanya majukumu yako makubwa. Kwa mfano mimi huwa nafanya kazi ya kuandika kila siku asubuhi na mapema, nikisema nifanye kitu kingine asubuhi halafu niandike baadae inakuwa vigumu sana kufanikiwa kuandika.

7. Kutokuwa na maamuzi.

Kuna wakati ambao mtu unajikuta unakosa maamuzi, badala yake unaanza kuruka ruka na maswali ambayo huna majibu yake. Unaanza kujiuliza nifanye hiki au kile, nianzie wapi, kipi ni muhimu zaidi n.k

Ili kuepuka hali kama hii weka mipango yote kabla ya kuanza kutekeleza jukumu lako. Hivyo unapoanza ni moja kwa moja hakuna tena kukwama kwa maswali ambayo yanaweza kukushawishi uahirishe kuendelea na jukumu lako.

Yajue mambo haya saba na jinsi yanavyoweza kukushawishi wewe uahirishe jukumu ulilopanga kufanya. Fanyia kazi mapendekezo haya ili uweze kuondokana na tabia hii ambayo inakunyima mafanikio.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kuboresha maisha yako.

TUPO PAMOJA.