Mchanganuo wa biashara ni muhimu sana kama kweli unataka biashara yako ikue na upate faida kubwa. Lakini wajasiriamali na wafanyabiashara wengi wadogo huwa hawaoni umuhimu wa kuandaa michanganuo ya biashara zao. Wengi huandaa pale wanapohitaji mkopo na kuambiwa ili wapewe mkopo lazima waoneshe mchanganuo wa biashara yao. Tofauti na hapo watu wengi wamekuwa wakifanya biashara zao kwa mazoea tu hivyo kukosa mipango na mikakati mizuri ya kuwawezesha kukua zaidi kibiashara.
Leo tutajadili jinsi ambavyo unaweza wewe mwenyewe kuandaa mchanganuo rahisi wa biashara yako. Mchanganuo huu utakuwezesha kujipima kama unasonga mbele au unapotea. Na kwa kuwa huu bado ni mwanzo wa mwaka utaweza kutumia vizuri mchanganuo wako ili mwaka utakapoisha uweze kujitathmini. Njia hii ya kuanda amchanganuo rahisi itafaa kutumika kwa wote, yaani wale wanaopanga kuanza biashara zao na hata wale ambao tayari wapi kwenye biashara zao lakini hawajawahi kufanya zoezi hili.
Kuwa na kalamu na karatasi, ikiwezekana kitabu na uandike na kujibu maswali haya ambayo yatakupa mwanga wa kujua biashara yako inaelekea wapi.
1. Biashara yako ni nini na una malengo gani?
Kitu cha kwanza kabisa kwenye mchanganuo wa biashara ni kujua aina ya biashara unayofanya. Ni lazima ujue aina ya biashara unayofanya ili usije kuingia kwenye mtego wa kujaribu kufanya kila kitu kinachotokea mbele yako. Ukishajua biashara yako ni nini unakazania hiyo na kuachana na mambo mengine. Pia baada ya kujua biashara yako ni nini weka malengo ya muda mfupi(miezi mitatu, sita na mwaka) na pia weka malengo ya muda mrefu, miaka miwili, mitano mpaka hata kumi. Weka malengo ambayo yatakusukuma kufanya kazi zaidi ili uweze kufanikiwa.
2. Nani ni wateja wako na utawafikiaje.
Baada ya kujua biashara unayofanya ni nini sasa unatakiwa kujua wateja wa biashara yako na jinsi ya kuwafikia. Kwenye kuwajua wateja wa biashara yako kwanza ni lazima ujue upo kwenye muundo upi wa biashara. Unaweza kuwa kwenye biashara ya kuuzia kampuni, au kuuzia wafanyabiashara wengine au kuuzia walaji moja kwa moja. Baada ya kujua muundo wako mfikirie mteja unayemlenga hasa wewe ni yupi, mfikirie kwa umri, aina ya maisha, kipato na hata vitu anavyopendelea. Pia jua mteja wako yuko wapi na unawezaje kumfikia ili ajue biashara yako ipo na inaweza kumtatulia matatizo yake.
3. Uongozi na usimamizi wa biashara/kampuni.
Ni muhimu kwenye mchanganuo wako uandike kuhusu uongozi na usimamizi wa biashara yako. Kwanza kabisa ni muhimu kusajili biashara yako kama kampuni kama bado hujafanya hivyo. Tutaona faida za kuwa na kampuni kwenye makala zijazo. Ni muhimu kuwa na uongozi mzuri ambao utahakikisha ukuaji wa biashara hiyo hata pale ambapo wewe utapata matatizo na kushindwa kusimamia biashara. Hapa ndio sehemu muhimu ya kujua ni watu gani unashirikiana nao kwenye biashara unayofanya.
4. Ni bidhaa au huduma ngapi unazotoa.
Ni muhimu pia kujua na kuandika kwenye mchanganuo wa biashara yako aina na idadi ya bidhaa au huduma utakazotoa. Kama ndio unaingia kwenye biashara kuwa makini sana usikimbilie kuingiza bidhaa au huduma nyingi sokoni halafu zikakushinda kusimamia na hatimaye ukapata hasara. Ni bora kuanza na bidhaa au huduma chache ambazo unaweza kuzisimamia vizuri.
5. Chanzo cha fedha.
Kama ndio unaanza biashara ni muhimu kuainisha kwenye mchanganuo wako ni kipi kitakuwa chanzo chako cha fedha. Je itakuwa ni akiba zako mwenyewe, zuruku kutoka kwenye taasisi au ndugu wa karibu au mkopo. Kama tayari upo kwenye biashara pia ainisha kama utahitaji fedha za kukuza biashara yako zaidi utatumia njia gani kuzipata.
6. Makisio ya faida.
Kitu cha mwisho na cha muhimu kuzingatia kwenye mchanganuo rahisi wa biashara yako ni makisio ya faida. Ni lazima ufanye makisio ya faida utakayokuwa unatengeneza baada ya miezi mitatu, miezi sita na mwaka mmoja. Hii itakufanya uongeze juhudi hasa pale ambapo unashindwa kufikia malengo.
Mchanganuo tuliojadili hapa ni wa kukuwezesha wewe kujua biashara yako inaelekea wapi. Kama utahitaji mchanganuo wa kitaalamu tafadhali pata onana na mshauri wa biashara aliyepo karibu na wewe akuandalie mchanganuo wa kitaalamu zaidi.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.