Moja ya maeneo muhimu sana kwenye biashara yako wewe kama mjasiriamali ni upangaji wa bei za bidhaa au huduma unazotoa. Hili ni eneo muhimu kwa sababu ukikosea kupanga bei unaweza kuiathiri biashara yako kwa kiasi kikubwa sana. Unaweza kukosa wateja au hata kupoteza wateja uliokuwa nao awali.
Katika makala ya leo tutajadili mchakato mzima wa kupanga bei kwa bidhaa au huduma zako na pia nini cha kufanya pale unapotaka kubadili bei. Jambo muhimu la kuzingatia hapa ni kwamba mambo tutakayojadili hapa yanaweza yasiwezekane kwenye biashara ua uchuuzi. Kama unauza vitu vya reja reja ambavyo bei tayari inajulikana mbinu hizi unaweza ukashindwa kuzitumia, ila kujifunza na kuzijua zitakusaidia katika maeneo mengine.
Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kupanga bei.
Wewe kama mjasiriamali tayari una wazo lako la kuzalisha bidhaa au huduma itakayowez akutatua matatizo ya watu. Au tayari unayo bidhaa au huduma ambayo unataka kuifikisha sokoni ili watu wanufaike na wewe upate faida. Kabla ya kuingia sokoni ni lazima ujue bei ya bidhaa au huduma hiyo ni kiasi gani. Kuna mambo muhimu ya kuzingatia katika kupanga bei, haya hapa ni baadhi ya mambo hayo;
1. Jua gharama zako za uzalishaji.
Kabla ya kupanga bei ya bidhaa ni muhimu sana kujua mpaka inamfikia mteja itakuwa imekugharimu kiasi gani. Hapa weka gharama za uzalishaji, gharama za usafirishaji, gharama za matangazo(kama umefanya). Utachukua gharama zote kisha ugawe kwa idadi ya bidhaa au huduma unazotoa. Ukishajua gharama halisi za wewe kuifikisha bidhaa au huduma mikononi mwa mteja hapo unaanza kupata picha kwamba bei isiwe chini ya hapo maana utapata hasara.
2. Jua uwezo wa mteja wako na kiwango anachoweza kumudu.
Kabla ya kuamua kuingia kwenye biashara hiyo uliyoingia, tayari ulishafanya utafiti kidogo kuhusu uwepo wa soko la biashara hiyo. Katika utafiti huu, pia ulipanga ni aina gani ya wateja ambao utafanya nao biashara. Sasa kaa chini na uangalie uwezo wa wateja wako kuweza kumudu bidhaa au huduma unayowapatia. Ukiweka bei kubwa sana utapoteza wateja, na pia ukiweka ndogo sana unaweza kupoteza wateja muhimu.
3. Jiridhishe na ubora wa bidhaa yako.
Jambo la tatu na muhimu sana kuzingatia wakati wa upangaji wa bei ni ubora wa bidhaa au huduma unayotoa. Bei unayotoa ni lazima iendane na ubora wa kitu unachotoa. Ukiweka bei kubwa huku bidhaa au huduma yako ina ubora mdogo utakosa imani kwa wateja na biashara yako itakufa.
4. Jua kiwango cha chini unachotakiwa kuuza ili kuweza kupata faida.
Baada ya kuangalia gharama zako za uzalishaji, kujua uwezo wa wateja wako na kujua ubora wa bidhaa yako sasa unaweza kufanya majaribio ya bei mbalimbali. Weka bei halafu angalia kwa vigezo hivyo vitatu hapo juu, utaweza kuuza bidhaa yako kwa urahisi kiasi gani na utahitaji kuuza kiasi gani kwa mwezi ili uweze kupata faida. Unaweza kupanga bei kubwa, ukauza kwa watu wachache na ukapata faida ya kukutosha. Na pia unaweza kuweka bei ndogo, ukauza kwa watu wengi na ukapata faida ya kukutosha pia. Wewe angalia kwa soko lako na ubora wa bidhaa yako ni ipi unaweza kwenda nayo ambayo pia itakujengea uaminifu kwa wateja wako.
Mabadiliko ya bei.
Baada ya kupanga bei na kuanza kufanya biashara, inaweza kufika kipindi ambapo utahitaji kubadili bei. Kuna mambo mawili muhimu ya kuzingatia wakati w akubadili bei;
Jambo la kwanza kabisa la kuzingatia kwenye kubadili bei ni kwamba hakikisha pia unafanya mabadiliko kwenye bidhaa au huduma yako yanayoweza kuendana na bei yako.
Jambo la pili ni unapobadili bei, ni bora kuongeza bei kuliko kupunguza bei. Hii ni muhimu sana hawa kama unafanya biashara ambayo unataka kuenda na wateja wako kwa muda mrefu. Unapopunguza bei, wateja wako wa mwanzo wanaweza kuona kama wao uliwaibia na hawatajisikia vizuri kuendelea kufanya biashara na wewe. Hivyo kuliko kupunguza bei ili kuvutia wateja wapya, ni bora kuacha bei ile ile ila kuongeza ubora wa bidhaa au huduma yako. Kama utaongeza bei pia pitia vigezo tulivyojadili hapo juu ili usipoteze wateja ambao wataona bei yako imekuwa kubwa sana.
Haya ndio mambo muhimu ya kuzingatia kwenye upangaji wako wa bei. Wajasiriamali wengi wanafikiri bei ndogo ndio inavutia wateja wengi, ila sio ukweli. Kinachovutia wateja ni ubora wa biadhaa au huduma unayotoa, hivyo kazana kuhakikisha unachotoa ni bora sana na kinamsaidia mtu kutatua matatizo yake.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.