Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu THINK AND GROW RICH kama umekosa uchambuzi wa nyuma bonyeza hayo maandishi.
Tuko kwenye uchambuzi wa hatua ya nne ya kufikia utajiri ambayo ni kupata maarifa, uzoefu na hata kufanya uchunguzi wako binafsi.
Kuna udhaifu mkubwa sana kwa watu ambao hauna dawa. Udhaifu huu ni kukosa matarajio makubwa kwenye maisha yao. Udhaifu huu ndio unaowafanya wengi kukubaliana na hali walizonazo na kutofanya jitihada za kuboresha maisha yao.
Kukosa matarajio makubwa kwenye maisha kumefanya watu kuendelea kufanya kazi ambazo hawazipendi kwa sababu tu hawaoni maisha mengine. Hatua nzuri ya mtu yeyote kuboresha maisha yake ni kujifunza zaidi. Kuongez amaarifa yanayohusiana na kile mtu anachofanya iwe ni kazi au biashara.
Watu wengi husingizia kwamba hawana muda wa kujifunza, hawawezi kwenda shule kwa sababu hawana fedha, wana majukumu ya kifamilia na kadhalika. Ila ukiangalia vizuri kuna nafasi nyingi sana ambazo mtu anaweza kuzutumia kujifunza na kuboresha kile anachofanya na hii ikapelekea kuboresha maisha yake.
Watu wengi wanaoanzia chini iwe kwenye kazi au biashara wanashindwa kukua zaidi. Hii inatokana na hali halisi iliyopo kwa wale wanaoanzia chini. Mtu yeyote anayeanzia chini anakuwa anatumia nguvu nyingi sana kwenye kazi zake tofauti na anayeanzia juu. Kazi hizi zinazotumia nguvu nyingi zinamfanya ashindwe kukazania mambo ya msingi yatakayomwezesha kukua zaidi.
Dawa pekee ya mtu kuweza kutoka chini na kwenda juu ni kujifunza na kuongeza maarifa. Hapa mtu ataweza kufanya mabadiliko kwenye kile anachofanya na hivyo kuongeza thamani yake.
Kufanikiwa na kushindwa kote kunatokana na tabia. Kama ukijijengea tabia ya kupenda kujiongezea maarifa na kuzitafuta fursa na kuzifanyia kazi ni lazima utafanikiwa. Ukiwa na tabia ya kutokupenda kujiongezea maarifa na kufanya kile tu ambacho unafanya kila siku unafunga njia yako ya mafanikio.
Unachohitaji ili kuweza kufikia utajiri ni WAZO ambalo utalifanyia kazi. Kwa kuwa na wazo ambalo utajifunza zaidi na kuliboresha kila siku utaweza kuzitumia vizuri fursa ambazo zitakuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
Kujifunza kupitia uzoefu wa wengine ni njia bora sana ya wewe kuweza kuongeza thamani ya kazi au biashara unayofanya.
Kuna makosa mengi sana ambayo unahitaji kuyafanya ili ujifunze, lakini kufanya makosa yote hayo wewe mwenyewe utachelewa sana kufikia utajiri ambao unakusubiri. Hivyo njia bora ya kujifunza ni kuangalia makosa gani ambayo wengine wameyafanya yakawagharimu hivyo kuepuka kuyafanya.
Pia unaweza kujifunza mbinu walizotumia wao kufikia mafanikio na wewe ukazitumia ili kufikia mafanikio zaidi kwa kile unachofanya. Njia bora ya wewe kujifunza kupitia uzoefu wa wengine ni kuwa na MASTERMIND GROUP ambapo unakuwa na watu ambao wanaelekea kwenye mafanikio makubwa kama wewe. MATERMIND GROUP itakufanya wewe uweze kufuata malengo na mipango uliyojiwekea hata kama unakutana na changamoto zinazoweza kukufanya ukate tamaa.
Uchunguzi pia utakuwezesha wewe kuziona fursa mbalimbali na jinsi unavyoweza kuzitumia kuboresha maisha yako na kuw atajiri. Ni muhimu sana wewe kuwa mchunguzi, kujua kila kinachoendelea kwenye kazi au biashara unayofanya ili uwe tayari kuchukua hatua. Kuna mabadiliko mengi sana yanayoendelea hivyo usipokuwa mchunguzi utashangaa unaachwa nyuma wakati wenzako wanasonga mbele.
Maarifa sio nguvu, bali maarifa yanayoweza kutumika vizuri ndio nguvu. Endelea kujipatia maarifa ambayo utayatumia kuboresha kazi au biashara unazofanya ili uweze kufikia utajeri.
Nakutakia kila la kheri kwenye maisha yako ya kitajiri.
TUPO PAMOJA.