Kuna kitu kimoja ambacho sina hakika sana kama nimewahi kukuambia. Kama sijawahi kukuambia ni kwamba kwa nyakati ambazo tunaishi ni lazima kila mtu awe mjasiriamali. Hata kama una ajira inayokulipa kiasi gani, kutegemea chanzo kimoja tu cha mapato ambacho ni mshahara ni hatari kubwa sana unayoweza kucheza kwenye maisha yako.

Mambo yamebadilika sana na kama bado hujayaona mabadiliko haya unajiandaa kukutana na hali ngumu zaidi. Hata jinsi unavyofanya kazi zako hata iwe umeajiriwa, unahitaji kuzifanya kw afikra za kijasiriamali, hii itakuwezesha kuwa mbunifu zaidi na kuweza kutoa matokeo mazuri.

Habari njema ni kwamba, ulazima wa kila mtu kuw amjasiriamali sio kitu kigeni, miaka mingi iliyopita kila mtu alikuwa mjasiriamali. Ni miaka michache iliyopita ajira hisi rasmi zilianzishwa lakini kama tunavyoshuhudia ni kwamba zinakufa na zinapotea kabisa, hivyo tunarudi tulikotoka.

Ili kuweza kuingia kwenye ujasiriamali na kujiajiri, kuna vitu vingi sana unavyohitaji kuvivuka kwa sababu jamii yetu imetupandikiza vitu vingi sana vya kuona ujasiriamali kama ni kitu hatari sana. Leo hapa utajifunza sababu 16 zinazokuzuia wewe kuingia kwenye ujasiriamali na jinsi ya kuzishinda ili uanze kufurahia maisha yako.

1. Umri wangu bado ni mdogo.

Kwa dunia ya sasa hakuna umri mdogo wa kuingia kwenye biashara au ujasiriamali. Na kipimo cha umri sahihi wa kuingia kwenye ujasiriamali sio miaka bali ukomavu wa akili. Ukishakuwa na akili komavu ya kuweza kufanya maamuzi na kuasimamia unaweza kufanikiwa kwenye ujasiriamali bila kujali umri wako ni miaka mingapi.

2. Sina uzoefu.

Kwa bahati nzuri au mbaya ni kwamba hakuna mtu aliyezaliwa akiwa na uzoefu wowote. Ila watu wanajifunza, watu wanafanya na hatimaye wanakuwa wazoefu, wanabobea na kuwa bora. Njia pekee ya wewe kuwa na uzoefu ni kuanza kufanya kile ambacho unataka kuwa na uzoefu nacho. Ndio utapata changamoto kati kati, lakini si ndio uzoefu wenyewe?

3. Sijaamua vya kutosha.

Sawa maamuzi yana nafasi kubwa, ila huwezi kuzijua hesabu kw akuamua. Unazijua hesabu kwakuamua, unajifunza hesabu kwa kujua kanuni na kufuata kanuni. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kuajiri na ujasiriamali, unatengeneza kanuni zako mwenyewe na unazifuata.

4. Sijawahi kufanya biashara.

Ndio uzoefu wa biashara ni muhimu sana kwenye kufikia mafanikio katika kujiajiri au ujasiriamali. Sawa hujawahi kufanya biashara, kwa hiyo kutokuanza kunakusaidiaje? Anza na endelea kujifunza kwa kile ambacho hukijui.

5. Siwezi kuhimili mambo yote mwenyewe.

Ujasiriamali unaweza kuwa na mambo mengi sana ambayo kama ukitaka kuyafanya mwenyewe utaishia kuchoka huku huoni kikubwa ulichofanya. Kama unaona mambo yanakuwa mengi sana kwako, tafuta mtu wa kwenda nae kwenye safari hiyo. Mtasaidiana na kupeana moyo katika nyakati ngumu.

6. Sina wazo zuri.

Anza na wazo lolote ambalo unalo kichwani, anza na kitu unachopenda kufanya na kama mambo yasipokwenda vizuri utabadili mbele ya safari. Ukisema usubiri mpaka upate wazo zuri, utaendelea kupoteza muda na hata ukianza na wazo zuri kiasi gani, kuna wakati utahitaji kufanya mabadiliko kwenye wazo lako.

7. Kila mtu anafanya ujasiriamali.

Au kuna watu wengi wanaofanya ninachotaka kufanya. Vizuri sana, hii inaonesha kwamba unachotaka kufanya tayari kina soko na watu wanakihitaji. Sasa unachohitaji kufanya wewe ni kuwa mbunifu na kuangalia ni jinsi gani unavyoweza kupenyeza na kuingia kwenye soko hilo. Usiige.

8. Nina familia inayonitegemea.

Hii isiwe sababu ya wewe kutoingia kabisa kwenye ujasiriamali, maana hakuna siku ambayo familia itaacha kukutegemea. Badala yake andaa akiba itakayoiwezesha familia yako kuishi miezi sita hata kama huna kipato chochote na jitoe miezi hiyo sita kufanyia kazi kile ulichoamua kufanya. Au kama hiyo huna uhakika nayo, anza kufanya kidogo kidogo, ukiwa bado umeajiriwa na ukishaona umefika mahali pazuri ndio unaweza kuingia moja kwa moja.

9. Sitaki kuwa na fedha nyingi sana, ni matatizo.

Kuingia kwenye ujasiriamali sio tu msukumo wa fedha, bali kuisaidia jamii zaidi. Kwa wewe kujiajiri kwanza utatoa nafasi wka wengine kuajiriwa unakotoka na pia utatengeneza ajira kwa wengine. Na kizuri zaidi utawasaidia watu kutatua matatizo yao.

10. Nitakosa uhuru wangu.

Kuingia kwenye ujasiriamali kunaweza kuwa ndio mwisho wa uhuru. Ndio hasa mwanzoni ambapo unaweza kuwa unafanya kazi masaa 24 kwa siku na siku 7 kwa wiki. Kama ni kitu unachojali hakuna tatizo kubwa, na pia kumbuka unawez akujipanga vizuri na ukatumia muda wako vizuri ili kujitengenezea uhuru. Ukilinganisha kujiajiri na kuajiriwa, unakosa uhuru mkubwa sana kwenye kuajiriwa.

11. Sina uhakika wa kufanikiwa.

Ni kweli, wengi wanaoingia kwenye ujasiriamali wanashindwa tena vibaya. Wengi wanaoanzisha biashara wanapata hasara. Lakini pia kuna wanaofanikiwa. Hivyo kuna nafasi ya wewe kufanikiwa pia, lakini jiandae vizuri ukijua kuna hatari iliyopo mbele yako. Na hivi ni jambo gani ambalo tuna uhakika nalo kwenye maisha?

12. Wazazi wangu wanataka niwe daktari.

Ni kweli wazazi na hata jamii inayotuzunguka inapenda kutuona tukiw akwneye ajira rasmi. Ukiwa daktari, msandishi, mwanasheria, mhasibu n.k unaonekana wa maana zaidi ya anayesema ni mjasiriamali. Usihofu kuhusu hili maana maisha unayotaka kuishi ni ya kwako na ukitaka kumfurahisha kila mtu utaishia kuwa na maisha magumu sana.

13. Sina akili sana.

Kama unaweza kuwa na wasi wasi kwamba una akili za kutosha kuwa mjasiriamali, basi hiyo ni akili tosha ya kuwa mjasiriamali. Huhitaji uwezo mkubwa sana wa kufikiri ndio uweze kuwa mjasiriamali. Unahitaji kujali, kuvumilia, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kuwa mwaminifu na kuwa tayari kubadilika.

14. Ajira inanitosha.

Kama ndio umeamua hivyo, basi na usilalamike tena kuhusu kipato, kutokupenda kazi unayofanya na hata kazi kukuchosha. Maana kwa kulalamika hakutakusaidia, ni bora kuchukua hatua ambayo tayari unaijua.

15. Nitaanza, kesho, mwaka ujao, watoto wakimaliza shule.

Kama unataka kuanza, anza leo, chochote unachosubiri hakitakupa nafasi ya kuanza kesho. Anza leo au hutaanza kabisa. Usijidanganye kesho au mwaka ujao.

Chukua hatua ya kuboresha kipato chako kwa kufanya kile unachopenda kukifanya na kukifanya kw aubora wa hali ya juu sana. Kujiajiri na ujasiriamali ndio njia mpya ambayo kila mtu anaweza kuingia, kama ataamua kufanya hivyo.

Nakutakia kila la kheri.

TUPO PAMOJA.