Hakuna kitu kizuri kwenye maisha ya sasa kama kuwa mjasiriamali. Kwa nini? Sababu zipo wazi na tumekuwa tunazijadili kwenye kona hii mara kwa mara. Na faida kubwa kabisa katika faida nyingi za kuwa mjasiriamali ni kuwa na uhuru wa maisha yako. Unapokuwa mjasiriamali unakuwa na uhuru ufanye nini ambacho kitakuwa na manufaa kwako, tofauti na mwajiriwa ambaye analazimika kufanya kila anachopangiwa hata kama hakina mchango mkubwa kwake.

Pamoja uhuru kuwa faidia kubwa ya ujasiriamali, hali haiku hivyo kwa wajasiriamali wengi wa kitanzania. Hali ipo tofauti kabisa, ujasiriamali umekuwa gereza ambalo linawafunga watu zaidi na wanashindwa kuishi yale maisha waliyotarajia kuishi wakati wanaingia kwenye ujasiriamali.

Unapoingia kwenye ujasiriamali na kuwa kwenye biashara kuna njia mbili. Njia ya kwanz ani biashara kukumiliki, hii inatokea kwa kila mtu hasa mwanzoni mwa ujasiriamali. Na njia ya pili ni wewe kuimiliki biashara, hii hutokea kwa wachache sana ambao wanajua maana hasa ya ujasiriamali. Sasa leo hapa nataka wewe utoke kwenye kundi la kumilikiwa, ambapo ndio wajasiriamali wengi wapo na biashara na kuingia kwenye kundi la kumiliki biashara, ambapo kuna wajasiriamali wachache na wenye mafanikio makubwa.

Kumilikiwa na biashara maana yake nini?

Tunaposema unamilikiwa na biashara maana yake biashara yako inakutegemea wewe kwa kila kitu. Katika hali hii wewe ukikosekana kwenye biashara yako mambo karibu yote yanashindikana. Hii ni hali ya hatari sana kwani hakuna aliye na uhakika wa kuweza kuwa vizuri kila wakati na kuweza kusimamia biashara yake vizuri. Hali hii ya kumilikiwa na biashara kila mjasiriamali anaipitia mwanzoni mwa biashara.

Maana ya kumiliki biashara.

Kumiliki biashara ni pale wewe mjasiriamali unapokuza biashara yako kiasi kwamba inaweza kujiendesha yenyewe bila yaw ewe kuwepo moja kwa moja. Biashara inaweza kuenda vizuri na wewe kuona ukuaji huo kupitia ripoti mbalimbali. Hii ni hali ambayo inafikiwa na wajasiriamali wachache ambao walifanya jitihada za kukua zaidi na wakaweza kuzifikia. Katika hali hii mjasiriamali anapopata matatizo yoyote anakuwa hana wasi wasi na biashara zake kwa sababu zinaweza kujiendesha mwenyewe.

Unawezaje kujitengenezea uhuru wa kumiliki biashara?

Kwa kuwa lengo lako la kuingia kwenye ujasiriamali lilikuwa kujijengea uhuru wa maisha yako sasa leo utajifunza jinsi unavyoweza kuifanya biashara yako isikutegemee.

1. Tengeneza mfumo.

Kabla hata hujafikiria kuajiri mtu kwenye biashara yako, tengeneza mfumo wa biashara yako. Katika mfumo huu yaangalie maeneo muhimu kwenye biashara yako na angalia kama ukimuajiri mtu majukumu yake yatakuwa yapi. Andika nafasi hiyo ya kazi na majukumu ambayo mtu atayafanya kwenye nafasi hiyo. Hii itakuwa rahisi kwa biashara yako kujiendesha kwa uhuru badala ya kutegemea watu. Kama ukiajiri watu halafu wao ndio waone nini cha kufanya, wakiondoka biashara yako itaumia sana.

2. Ajiri watu wa kukusaidia kazi.

Haijalishi ujasiriamali wako ni mdogo kiasi gani, hatua namba moja ya kupata uhuru na kukua zaidi kama mjasiriamali ni kuajiri watu wakusaidie kazi. Wewe mtu mmoja huwezi kufanya kila kitu, tafuta watu wenye sifa nzuri ambao unaweza kuwaajiri na wakatekeleza majukumu hayo vizuri. Katika kuajiri sio lazima uende haraka na wewe kubaki bila jukumu lolote. Ni vizuri kwenda taratibu ili pia uijue biashara yako vizuri na hata watu unaowaajiri upate nafasi ya kufanya nao kazi na kuwajua vizuri zaidi.

Kama kikwazo cha wewe kushindwa kuajiri ni kipato kidogo basi naweza kukuambia kwamba biashara yako haitengeneze faida ya kutosha. Hivyo unahitaji kufanya mabadiliko ya haraka sana la sivyo utaendelea kuwa mtumwa wa biashara hiyo ambayo pia haiwezi kukupatia kipato cha kuridhisha.

3. Fikiria mbali zaidi ya matatizo ya biashara.

Unapoingia kwenye biashara ni rahisi sana kumezwa na matatizo madogo madogo ya kuendesha biashara kila siku. Ukishamezwa na matatizo haya ni rahisi sana kwako kusahau lengo kubwa ambalo ni kukuza biashara yako zaidi ili kupata uhuru. Endelea kuangalia mbali zaidi na mara zote fanya kazi kufikia umbali huo. Ukishaingia kwenye biashara za kuendesha biashara ni rahisi sana kupotea.

Ni wakati sasa wa kuchukua uhuru ambao uliufuata kwenye ujasiriamali. Anza kutengeneza mfumo na ajiri watu wenye sifa na watakaokusaidia kukuza biashara yako. Kadiri utakavyokuwa na muda mwingi wa kufikiriakuhusu biashara yako, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kuikuza zaidi na kupata uhuru zaidi.

TUPO PAMOJA.