Ili kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yaani WORLD CLASS unahitaji kuchagua maisha ambayo utataka kuishi mwenyewe, kuchagua kitu ambacho unapendakukifanya na kuwa na mbinu nyingi za kukuwezesha kuwa bora sana kwa chochote unachoamua kufanya.

Kwa upande wako mpaka sasa umeshachagua kitu ambacho unapenda kukifanya kwenye maisha yako na kama ungekuwa umabakiza siku moja tu ya kuishi ungefurahia kufanya kitu hiko. Kama bado hujachagua kitu hiki unahitaji kufikiria mara mbili kama kweli upo tayari kwa ajili ya kuyapata mafanikio makubwa.

Kwa upande wa pili, hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA unajifunza mbinu mbalimbali zitakazokuwezesha kufikia mafanikio hayo makubwa unayotazamia. Mbinu zote bora unazohitaji unajifunza hapa na kama ukizitumia maisha yako yatabadilika kwa kiasi kikubwa sana.

Katika kusoma na kujifunza kwangu kupitia mtandao wa intaneti nimekutana na makala moja ya mtu anayeitwa John Romaniello. Mtu huyu ameandika makala yenye sheria zake 65 za mafanikio, furaha na maisha mazuri. Nimeisoma na nikaona kuna vitu vizuri tunavyoweza kujifunza na hata kuchagua vichache vya kuongeza kwenye orodha zetu. Nimewashirikisha makala hii ili na nyie muone ni vitu gani mnaweza kuchukua hapa.

Sehemu kubwa ya sheria hizi nimechukua kama alivyoandika yeye hivyo katika kuzitumia unaweza kuzibadili ili ziendane na mazingira yako. Hapa nimekushirikisha sheria 32 kati ya hizo 65 alizoandika wewe, kusoma nyingine zaidi utapata kiungo mwisho wa makala hii.

Sheria zenyewe hizi hapa;

1. Kamwe usilale zaidi ya masaa 9 na usilale pungufu ya masaa 3. Ni muhimu kupumzika, lakini kulala sana ni kupoteza muda ambao ungeweza kuutumia kujiendeleza au kutawala dunia.

2. Ni bora kuomba msamaha kuliko kuomba ruhusa.

3. Unapopata wazo lolote liandike mahali, usiamini kumbukumbu zako.

4. Shona nguo zako. Suti ya laki mbili inayokutosha itakupa muonekano mzuri kuliko suti ya laki tano ambayo ni kubwa kwako.

5. Onesha upendo. Mara zote kuwa na neno zuri la kuongea, la kumpa mtu moyo, la kuonesha upendo. Watu watakupenda kwa hilo.

6. Toa shukrani. Usitumie kazi au wazo la mwingine bila ya kumtambua na kutoa shukrani.

7. Hakuna mtu anayejali kuhusu matokeo yako ya shule, kuhusu GPA yako. Au hata mafanikio yoyote uliyopata zaidi ya miaka miwili iliyopita. Watu wanataka kujua ni kipi umefanikisha sasa.

8. Unaruhusiwa kusema hapana kwa vitu ambavyo huvitaki. Hata kama hali au jamii inakulazimisha kwa kiasi gani, kama hupendi au husukumwi kufanya sema hapana, baadae watakuheshimu kwa hilo.

9. Fanya kitu unachokichukia, kifanye kila siku kwa siku 30, halafu usikifanye tena.

10. Usipinge wazo kama huna wazo mbadala. Kama huna njia bora au wazo zuri zaidi ni bora kukaa kimya.

11. Usitake kufuatilia sana maisha ya watu na ni vitu gani wanafanya na maisha yao binafsi. Kama hawavunji sheria, hayakuhusu.

12. Jitahidi usitengeneze maadui. Kama kuna mtu analazimisha kuwa adui yako, hakikisha unammaliza nguvu.

13. Jua linapochomoza uwe tayari kwenye uwanja wa mapambano.

14. Usiwe na urafiki na mtu ambaye hana vitabu, hakuna kikubwa utakachojifunza kwake.

15. Angalau mara moja kwenye maisha yako vurugwa.

16. Kuwa mtu wa kwanza kutaka kusaidia.

17. Juana na watu wengi sana uwezavyo. Jinsi unavyojuana na watu wengi, ndivyo unavyoongeza nafasi zako za kufikia mafanikio.

18. Jaribu kila kitu unachofikiria kuwa kwenye maisha yako, jaribu kwa kujitoa na kuna vitu utavipenda na vingine hutavipenda.

19. Jibu matusi yote kwa tabasamu. Sio kila mtu atakupenda au kukubaliana na wewe, na kujibu tusi kwa tusi hutakuwa na tofauti yoyote na yule anayekutukana.

20. Soma vitabu vingi sana uwezavyo. Kusoma kunakufanya unakuwa na akili zaidi, unakuwa mjanja na unakuwa na mawazo mazuri. Na pia unakuwa mtu bora zaidi.

21.Kuna vitu vingi sana ambavyo haviwezi kufundishwa ila hakuna kitu ambacho huwezi kujifunza. Tafuta watu wa kukufundisha na wakati mwingine jifunze kutokana na uzoefu.

22. Kinachohesabika sio miaka uliyoishi kwenye maisha yako, bali maisha uliyoishi kwenye miaka yako. Kuwa bora kila siku na furahia maisha yako.

23. Yakubali makosa yako kwa uaminifu.

24. Kuwa bora sana kwa kile unachofanya, kuliko mtu yeyote alivyowaki kukifanya dunia nzima.

25. Popote unapokuwa hakikisha una kiasi cha fedha kama tahadhari, huwezi kujua nini kitakachotokea.

26. Kama unaogopa kupoteza fedha, hutokaa upate fedha. Kama unaogopa kuchukua mazingira ya hatari(risk) utakosa fursa nyingi za kukuwezesha kupata fedha zaidi. Na utakufa masikini.

27. Jifunze jinsi ya kupika. Kama ni mtu mzima lazima uweze kujihudumia mwenyewe, ndio lengo kuu la maisha.

28. Kila kitu kwenye maisha yako kiwe kwenye marekebisho, hata marekebisho yenyewe. Kila siku kuwa bora kuliko ulivyokuwa jana.

29. Tatua migogoro haraka, kwa siri na bila ya hasira. Kuwa na hasira au kutafuta wa kulaumu hakutakusaidia zaidi ya kuongeza tatizo.

30. Jifunze jinsi ya kuomba kile unachotaka. Watu hawawezi kusoma mawazo yako, iwe ni kwenye mahusiano, kazi au biashara, hakuna mtu anayeweza kutabiri unataka nini. Uliza au omba kile unachotaka na hakika utapewa.

31. Usimiliki vitu vingi sana, isipokuwa vitabu.

32. Maliza mazungumzo yoyote kwa kutumia kauli hii… “Hebu niambie; nawezaje kukusaidia?” Sema hivi ukimaanisha, saidia vyovyote uwezavyo,  hii ndio sheria muhimu sana kuliko zote.

Hizo ni baadhi ya sheria za mafanikio nilizoweza kukushirikisha kutoka kwa John Romaniello. Unaweza kusoma sheria nyingine kwenye makala yake kwa kubonyeza hapa. Nyingi sijazichukua kwa sababu naona hazina uhusiano hasa kwenye mazingira yetu.

Chagua sheria chache za kuongeza kwenye sheria zako za mafanikio. Au unaweza kuchukua zote. Kumbuka mafanikio yako yapo mikononi mwako, ni wewe kuyafanyia kazi na kuanza kuyaona kwenye maisha yako.

Nakutakia kila la kheri.

TUPO PAMOJA.