Dunia imebadilika sana kwa siku hizi. Mambo ambayo yalikuwa yanafanyika miaka ya nyuma sasa hivi ni kama hayana faida tena au hayaendani na mazingira tuliyopo. Moja ya mabadiliko makubwa yaliyotokea duniani ni kusambaa kwa mtandao wa intaneti.
Miaka 20 iliyopita mtandao wa intaneti ulikuwa unatumika na watu wachache sana na waliokuwa wakifanya kazi kwenye ofisi muhimu. Ila sasa hivi mtandao wa intaneti unatumika karibu na kila mtu anayeweza kutumia simu ya mkononi.
Takwimu za mamlaka ya mawasiliano Tanzania(TCRA) zinaonesha kwamba mpaka kufikia desemba mwaka 2014 tanzania ilikuwa na watumiaji wa intaneti wasiopungua milioni kumi na moja(11,000). Hili ni ongezeko kubwa sana kutoka watumiaji milioni tatu mwaka 2008. Kwa takwimu hizi na hata kw akuangalia maisha ya kawaida idadi ya watumiaji wa mtandao wa intaneti inaongezeka kwa kasi sana.
Ukuaji huu wa watumiaji wa intaneti unamaanisha kwamba wateja wako wengi sasa hivi una uhakika wa kuwapata kwenye mtandao. Watu wengi ambao wanahitaji huduma au bidhaa zako ni rahisi sana kuwafikia kwenye mtandao kutokana na ongezeko la matumizi ya simu zenye uwezo wa kutumia mtandao?
Je wewe kama mjasiriamali una mbinu gani za kuwafikia wateja hawa?
Leo nakushirikisha mbinu mbili zitakazokuwezesha kutumia mtandao wa intaneti kuwafikia wateja wako na hata kukuza biashara yako. Huenda umekuwa unatumia mbinu hizi ila ukawa huzitumii vizuri.
Mbinu ya kwanza; kuwa na tovuti na blogu.
Tovuti hii ni sehemu ambapo wateja wako wanajua wewe ni nani, uko wapi na unafanya nini. Kwenye tovuti ya biashara yako kunakuwa na maelezo ya kila kitu unachofanya. Hii inakuwa rahisi kwa mteja kujua anafikaje pale ulipo na akifika anapata nini kinachoweza kumsaidia.
Pia unahitaji kuwa na blogu ambayo unaandika mambo yanahusiana na biashara unayofanya. Blogu ni sehemu ndogo ya tovuti ambayo unaweza kuwa unaandika mambo mbalimbali kwa lengo la kuelimisha, kutoa taarifa au kutangaza. Kupitoa blogu ya biashara yako utakuwa ukiandika mambo yanahohusiana na wateja wako na jinsi ambavyo biashara yako inaweza kuwasaidia.
Kumbuka kwamba siku hizi watu wanapopata tatizo lolote wanaingia kwenye mtandao wa google na kutafuta suluhisho. Sasa kama wewe una tovuti na blogu inayoelezea kile unachofanya na jinsi kinavyoweza kuwasaidia, tovuti au blogu yako itaonekana mwanzo kabisa kwenye ukurasa wa google na mtu atakuja moja kwa moja kwenye tovuti au blogu yako.
Mbinu ya pili ni kuwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hivi sasa kuna mitandao mingi sana ya kijamii na watu wengi wapo kwenye mitandao hii. Kabla kabisa ya kuingia kwenye mitandao hii kwa ajili ya kutangaza biashara yako ni lazima ujue wateja wako wanapatikana kwa wingi kwenye mitandao ipi. Kwa hapa Tanzania watu wengi wapo kwenye mitandao ya facebook, instagram, twitter na hata linkedin. Mitandao hii inatofautiana kwa jinsi unavyoweza kuitumia kutangaza biashara yako. Kuna mitandao ambayo inatumia sana picha na mingine inatumia sana maelezo.
Baada ya kujua mtandao unaoweza kutumia, kuwa na muda ambao unaweka habari zinazohusiana na biashara unayofanya. Muda huo uwe unaendana na muda ambao watu wengi wanakuwa wanatumia mitandao hii. Kama wakati wa asubuhi, machana na hata jioni.
Kwa mitandao ya kijamii hakikisha unategeneza ukurasa wa mashabiki facebook ambapo unaweza kujenga nao mahusiano mazuri kupitia mtandao. Toa elimu muhimu inayohusiana na biashara unayofanya na jibu maswali na maoni ya wateja wako wanaowasiliana na wewe kupitia mitandao hii.
Usiache wateja wanaopatikana kirahisi kwenye mtandao wa intaneti. Japokuwa wateja hawa wanapatikana kirahisi haimaanishi kuwapata ni kazi rahisi. Unahitaji kujipanga vizuri ili uweze kuwafikia wateja wako vizuri kupitia mitandao huu. Kama utahitaji kutengenezewa tovuti au blogu tafadhali wasiliana nami kwa email(amakirita@gmail.com) au namba ya simu(0717396253/0755953887)