Tunaishi kwenye dunia ambayo kuna vitu vingi sana vya kufanya lakini muda ni mfupi. Labda tusiseme muda ni mfupi, bali muda umekuwa ni ule ule tokea zamani ila siku hizi mambo ya kufanya yamekuwa mengi sana.
Kadiri maendeleo ya teknolojia yanavyotokea, tunapata vitu vingi sana vya kufanya. Kwa mfano ukianza na simu yako, kwa nafasi kubwa sana unatumia simu yenye uwezi mkubwa, simu ambayo imeunganishwa na mitandao ya kijamii, pabua pepe na bado kupiga na kupokea simu na ujumbe mfupi.
Hii ina maana kwamba kwa simu yako tu, unaweza kuwa na mambo mengi sana ya kufanya. Kuingia facebook kuona kama kuna mtu kaweka jambo zuri au kuweka jambo lako mwenyewe. Kuingia instagram na kuangalia picha mbili tatu, kuingia kwenye email na kusoma au kujibu na bado kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno. mambo yasingekuw amabaya sana kama kazi yako ingekuwa ni kuingia tu kwa muda ambao unapanga wewe. Mambo yanaharibika zaidi pale ambapo kifaa hiki kimoja tu kinawez akukukatisha kwenye kazi yako kwa ujumbe wowote unaoingia kwenye mitandao ya kijamii au kwenye simu yenyewe.
Kutokana na changamoto nyingi ambazo tnakutana nazo kwenye maisha ya sasa, kuweka kipaumbele kwenye maisha yako ni muhimu sana.
Zifuatazo ni baadhi ya faida za kujiwekea kipaumbele kwenye maisha yako.
1. Kuwa mmiliki wa maisha yako mwenyewe.
Hakuna jambo zuri kwenye maisha kama pale unapojua wkamba wewe ndio unayemiliki maisha yako, wewe ndiye unayepanga ufanye nini na kwa wakati gani. Sasa kama huna kipaumbele utajikuta unafanya kila kinachotokea mbele yako. Na mara nyingi hayo utakayokuwa unafanya sio uliyopanga wewe na hivyo kujikuta unakosa nguvu kwenye maisha yako. Anza kuweka kipaumbele kwenye maisha yako na utakuwa na uhuru na maisha yako.
2. Kukamilisha mipango yako ya siku.
Katika siku yoyote ile kuna vitu ambavyo unakuw aumepanga kufanya. Kama utaanza tu kufanya vitu hivyo bila ya kuwa na kipaumbele, utajikuta umemaliza siku huku umechoka lakini huoni kipi umekamilisha. Ni rahisi sana kupotez amuda kama huna kitu kimoja cha kufanya ambacho unaweza kukiangalia na kusema leo nimekamilisha hiki. Nafikiri una uzoefu kwa baadhi ya siku kujikuta umefanya mambo mengi ila hakuna hata moja ambalo umelikamilisha. Hii ni kwa sababu hukuw ana kipaumbele na hivyo kujikuta unajaribu kila kitu.
3. Kupata muda wa kupumzika.
Tunaishi kwenye dunia ambayo ina usumbufu masaa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki. Yaani hata muda wa kulala, kuna mambo mengine mazuri yanayoendelea ambayo ungependa kuyafuatailia. Ndio maana siku hizi watu wengi wanakosa hata muda wa kulala huku hakuna jambo la maana wanalokuwa wanafanya. Kwa mfano mtu anakaa mpaka usiku wa manane akizunguka kwenye mitandao, au akiangalia tamthilia, au akiangalia michezo mbalimbali. Kama utakosa kipaumbele kwenye maisha yako ni rahisi kwako kujikuta unafanya kitu ambacho kinakukosesha muda wa kupumzika.
4. Kupata muda wa kukaa na wale unaowapenda.
Kama kuna changamoto kubwa ni kupata muda wa kukaa na wale ambao tunawapenda. Vifaa vya kisasa vimeharibu sana hali hii ya kukaa pamoja na wale unaowapenda. Siku hizi ni vigumu watu kuzungumza dakika kumi bila ya kuangalia simu zao. Kama watu unaowapenda ndio kipaumbele kwako itakuwa rahisi kwako kuweka simu pembeni na kuwa na mazungumzo mazuri ambayo yatajenga uhusiano wenu zaidi.
5. Kufanikiwa.
Hakuna mafanikio kama huna kipaumbele.
Kuna mtu mmoja alikuwa anakimbiza sungura wawili, unajua alikamata wangapi? Hakukamata hata mmoja, maana alifikiri anaweza kupata wote mwishowe akakosa wote. Kama huna kipaumbele kwenye maisha yako ni sawa na mtu anayekimbiza sungura wawili. Utajikuta unakazana kufanya kila kitu ila mwisho wa siku huoni ukisonga mbele.
Maisha ni kipaumbele, chochote unachofikiria kufanya kiweke kuw akipaumbele. Chagua kufanya kitu kimoja tu kwa wakati na kikiisha ndio ufanye kitu kingine. Hii ndio njia ya uhakika ya kuweza kufanya zaidi na kwa ubora zaidi.
Nakutakia kila la kheri katika kuweka kipaumbele kwenye maisha yako.
TUPO PAMOJA.