Jambo kubwa la kushangaza kuhusu maisha ni kwamba kuna watu wengi sana ambao wamejaribu kutafuta mafanikio kwenye maisha yao ila wameshindwa. Cha kushangaza ziadi ni kwamba wanaoshindwa ni wengi sana kuliko wale wanaofanikiwa. Asilimia 98 ya watu wanaojaribu kupata mafanikio wanaishia kushindwa.
Kuna tatizo kubwa sana kwenye mfumo wa maisha ambao unachangia sehemu kubwa ya watu kuishia kushindwa. Kuna tatizo kubwa pia kwenye mfumo wa elimu ambao unaandaa watu wengi kwenda kushindwa. Mwandishi anasema alipata bahati ya kuhoji watu waliofanikiwa na watu walishindwa pia. Na aliweza kupata sababu 30 ambazo zinawafanya watu wengi kushindwa.
Hapa tutaziona sababu hizo.
1. Matatizo ya kuzaliwa nayo. Hili ni tatizo dogo ila linaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwa mtu kuweza kufikia mafanikio. Kwa mfano kwa mtu ambaye anazaliwa na matatizo ya akili, yaani ana uwezo mdogo sana wa kiakili, ni vigumu sana kuweza kufanya mambo mengi tuliyojadili yanayomwezesha mtu kufikia mafanikio.
2. Kukosa lengo linaloeleweka kwenye maisha. Hakuna matumaini ya mafanikio kwa mtu ambaye hajui ni kitu gani anachotaka kwenye maisha, atakipataje? Mwandishi anasema watu 98 kati ya 100 aliowahoji hawakuwa na lengo kubwa kwenye maisha yao.
3. Kukosa shauku kubwa ya kuwa tofauti. Mtu yeyote ambaye hayupo tayari kuwa tofauti hana nafasi ya kuweza kufanikiwa.
4. Kukosa elimu ya kutosha. Hiki ni kikwazo ambacho kinawazuia wengi kufikia mafanikio ila kinaweza kuondolewa. Na elimu tunayozungumzia hapa sio ya darasani tu, bali elimu ya kukuwezesha kujua vizuri kile unachofanya.
5. Kukosa nidhamu binafsi. Kama huwezi kujisimamia mwenyewe, huwezi kumsimamia yeyote. Nidhamu binafsi inatokana na kuweza kujisimamia mwenyewe. Kabla hujaweza kuidhibiti hali yoyote unahitaji kujidhibiti wewe kwanza.
6. Afya mbovu. Hakuna mtu anayeweza kufikia mafanikio na kuyafurahia kama hana afya nzuri. Mambo mengi yanayochangua kuwa na afya mbovu unaweza kuyadhibiti.
7. Kukulia kwenye mazingira ambayo sio mazuri. Tabia nyingi ambazo watu wanazo wamejijengea tokea wakiwa wadogo. Kama mtu amekulia mazingira yenye uhalifu sana, ni rahisi na yeye kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu, na hakuna mhalifu anayeweza kufikia mafanikio.
8. Kuahirisha mambo. Hii ndio sumu kubwa sana ya mafanikio. Watu wengi hupend akusubiri mpaka mambo yawe vizuri ndio waanze kufanya kitu, yote hii inakuzuia kufikia mafanikio. Anzia ulipo, anza na ulichonacho na baadae utapata njia bora zaidi.
9. Kukosa uvumilivu. Wengi wetu ni waanzilishi wazuri ila wamaliziaji wabovu sana kwenye jambo lolote tunalofanya. Ni rahisi sana kuanz akufanya kitu, ila unapokutana na changamoto, ni vigumu kuendelea. Unahitaji uvumilivu ili kufikia mafanikio. Kushindwa hakuwezi kuvumilia uvumulivu.
10. Haiba Hasi. Mafanikio hayawezi kuja kwa mtu ambaye ana haiba hasi ambayo inawafanya watu wasiwe karibu naye. Mafanikio yanakuja wka ushirikiano, hivyo kama haiba yako haiwavutii watu kushirikiana na wewe ni vigumu sana kufikia mafanikio.
11. Kushindwa kudhibiti hamu ya kufanya mapenzi. Nguvu inayotumika kwenye kufanya mapenzi ni nguvu kubwa sana unayoweza kuitumia kufanya mambo makubwa. Kwa kuweza kutumia nguvu hii na kuibadilihsa kuipeleka kwenye vitu vitakavyokufikisha kwenye mafanikio utaweza kufikia mafanikio makubwa.
12. Kutaka kitu pasipo kutoa kitu. Mawazo ya kamari yamewafanya watu wengi sana kushindwa. Pale unapofikiria kwamba unaweza kupata kitu bila ya kuweka juhudu na maarifa jua kabisa kwamba unajiandaa kushindwa. Hakuna mafanikio yanayopatikana kwa njia hiyo.
13. Kukosa nguvu ya kufanya maamuzi. Watu waliofanikiwa wanafanya maamuzi haraka na kama ni kuyabadili wanayabadili taratibu sana. Watu wanaoshindwa wanafanya maamuzi taratibu sana na kama ni kuyabadili wanayabadili haraka sana. Kukosa maamuzi na kuahirisha mambo ni ndugu wawili ambao unatakiwa kuwaua haraka sana kabla hawajakumaliza.
14. Hofu. Kuna hofu kuu sita ambazo zinawazuia wengi kufikia mafanikio. Tutajifunza hofu hizi kwenye sura nyingine za kitabu hiki.
15. Uchaguzi mbovu wa mwenzi wa maisha. Hii ndio sababu kubwa ya wengi kushindwa. Mahusiano ya ndoa yanawaleta watu wawili karibu sana. Kama ukaribu huu hautakuwa mzuri na ukawa wa migogoro unaua ndoto zote za kufikia mafanikio.
16. Kuwa mwangalifu sana. Hakuna mafanikio kwa watu ambao hawapo tayari kuchukua hali za hatari. Kuwa mwangalifu sana ni tatizo kama ilivyo kwa kutokuwa mwangalifu. Kuna wakati kwenye maisha ambapo utahitaji kufanya mambo ambayo yanaweza kuwa ni ya hatari.
17. Uchaguzi mbovu wa mshirika wa biashara. Hii ni sababu kubwa ya kushindwa kwenye biashara. Chagua mtu ambaye ana hamasa ya kufanya kazi, mwenye ushirikiano wa kutosha, mwaminifu na anayejituma. Chagua mtu ambaye utakuwa tayari kuiga kile anachofanya.
18. Ushirikina na chuki. Ushirikina ni aina ya hofu. Pia ni dalili ya ujinga. Kama unaogopa kwamba kuna watu wanakufanyia ushirikina ndio maana hufanikiwa basi unayazuia mafanikio yako mwenyewe kwa hofu na ujinga. Watu wanaofanikiwa hawana hofu na ujinga wa aina hii.
19. Uchaguzi mbovu wa kitu unachofanya. Hakuna mtu anayeweza kufanikiwa kw akufanya kitu ambacho hakipendi. Hatua ya kwanza kabisa ya kufanikiwa ni kuchagua kazi au biashara ambayo utakuwa tayari kuifanya kwa moyo wako wote na kwa akili zako zote.
20. Kushindwa kukazainia vitu vichache. Mtu anayetaka kufanya kila kitu huishia kushindwa kufanya chochote. Wekeza nguvu zako zote kweye kufanya kitu kimoja na utapata mafanikio makubwa.
21. Kushindwa kudhibiti matumizi. Mtu ambaye hawezi kudhibiti matumizi yake hawezi kufanikiwa. Hii ni kwa sababu kila mara atakuwa hana fedha. Unapoweza kudhibiti matumizi yako na kuweka akiba, akiba yako inakupa ujasiri na kukuwezesha kuchagua kazi ambayo unakubaliana nayo kwa malipo. Ila kama huna akiba, utakubali kazi yoyote ile hata kama malipo ni kidogo.
22. Kukosa shauku. Kama huna shauku, huwezi kuwashawishi watu wengine. Mtu mwenye shauku anaweza kushawishi kundi lolote la watu na wakashirikiana nae katika kufikia mafanikio.
23. Kuwa na mawazo mgando. Watu ambao wameamua kufunga mawazo yao kwenye jambo lolote ni vigumu sana kupata mafanikio. Hawa ni watu ambao wameamua kutokuongeza maarifa na wanaamini kile wanachokijua wao tu, hawakubali kusahihishwa au kujifunza mambo mapya. Baadhi ya vitu vinavyowafanya watu kuwa na mawazo mgando ni dini, siasa na ukabila.
24. Kutokuwa na kiasi. Watu ambao hawana kiasi kwenye jambo lolote wanalofanya hawawezi kufikia mafanikio. Baadhi ya maeneo ambayo kukosa kiasi kunaharibu kabisa mafanikio ni chakula, ulevi, na kufanya mapenzi. Kuendekeza sana vitu hivi ni kikwazo cha kufikia mafanikio.
25. Kushindwa kushirikiana na wengine. Watu wengi sana wanapoteza nafasi zao na fursa nzuri kwenye maisha kwa kushindwa kushirikiana na wengine. Hili ni tatizo kubwa kuliko hata mengine yote.
26. Kuwa na nguvu ambazo hukuzipata kwa juhudi zako. Mfano mzuri ni watoto wanaorithi mali za wazazi wao. Kuwa na kitu ambacho hujakitolea jasho ni chanzo kikubwa sana cha kushindwa kwenye maisha. Utajiri wa haraka ni mbaya kuliko hata umasikini.
27. Kukosa uaminifu. Hakuna mbadala wa uaminifu, mtu ambaye sio muaminifu hawezi kufanikiwa kamwe. Anaweza kufanikiwa kwa muda mfupi ila baadae mambo yote yanajulikana na anapotez akila kitu ikiwepo heshima yake mwenyewe.
28. Ubinafsi na majivuno. Vitu hivi viwili ni kama taa nyekundu inayowatahadharisha wengine wakae mbali. Ni sumu kubwa sana kwenye kufikia mafanikio.
29. Kudhani badala ya kufikiri. Watu wengi ni wavivu sana kutafuta taraifa ambazo ni za kweli. Badala yake wanafanya maamuzi yao kwa kutumia maoni ya watu wengine au kwa kudhani kitu fulani kinaweza kuwa katika hali fulani. Unahitaji kutafuta ukweli ili uweze kufikia mafanikio.
30. Kukosa mtaji. Hii ni sababu kubw aya kushindwa kwa watu wanaoingia kwenye biashara kwa mara ya kwanza. Unahitaji kuwa na kiasi cha mtaji kitakachowezesha biashara yako kusimama kabla hata haijaanza kutengeneza faida.
Hizo ndio sababu 30 zinazowafanya watu wengi kushindwa kama zilivyofanyiwa utafiti na mwandishi wa kitabu THINK AND GROW RICH.
Je katika sababu hizi ni zipi ambazo zimekuwa zinakuzuia wewe? Tafadhali tushirikishane kwenye maoni hapo chini. Pia kama kuna sababu nyingine unayoona ni kikwazo kwa mafanikio ila haikutajwa hapo pia tushirikishe.
Karibu sana tushiriksihane.
TUPO PAMOJA.
Uchaguzi wa mambo ambayo siyo sahihi Na uchaguzi usio sahihi
LikeLike