Kila biashara ina ushindani, kama unaamini kwamba biashara yako wewe haina ushindani basi bado hujaijua vizuri biashara unayofanya. Na kwa maana hiyo basi upo kwenye hatari kubwa sana ya kuondolewa kwenye biashara hiyo kama hutobadilika. Katika makala ya leo hapa kwenye KONA YA MJASIRIAMALI, tutajadili umuhimu wa kujuwa mshindani au washindani wako na mbinu nzuri unazoweza kutumia kufaidika na ushindani uliopo.
Kabla hatujaingia kwenye kujua washindani wako na jinsi ya kutumia ushindani kufanikiwa zaidi nikueleze mapema kabisa usiwe na fikra za kishindani. Yaani usiwekeze nguvu zako zote katika kumuondoa mshindani wako sokoni. Kwa kufanya hivi utaua biashara yake nay a kwako pia. Badala ya kuwekeza nguvu nyingi kwenye kumuondoa mpinzani wako sokoni au kwenye kuepuka kuondolewa sokoni leo utajifunza kuwekeza nguvu zako kwenye kile unachofanya vizuri na hatimaye kuwaacha washindani nyuma.
Washindani wako ni nani?
Kuna aina mbili za ushindani kwenye biashara;
Aina ya kwanza ni ushindani wa moja kwa moja. Huu ni ule ushindani ambapo kuna mtu anafanya biashara ambayo unaifanya wewe. Kwa hiyo mnakuw amnafanya kitu kimoja na mnagombea wateja wa aina moja. Ushindani huu uko wazi kabisa na hivyo wengi huhofia zaidi ushindani huu. Wajue watu wote ambao wanafanya biashara inayofanana na biashara unayofanya ili kuweza kujua jinsi ya kuwa mbele yao zaidi.
Aina ya pili ya ushindani ni ushindani usio wa moja kwa moja. Huu ni ushindani ambao unatokana na mbinu unazotumia kufanya biashara na pia mazingira unayofanyia biashara. Inawezekana mazingira uliyopo na mbinu unazotumia vinamzuia mteja kuweza kukufikia au kufanya biashara na wewe. Jua vitu vyote ambavyo vinaweza kuwazuia wateja kufanya biashara na wewe na baada ya hapo utajua ni jinsi gani utakavyoweza kuvivuka.
Mbinu bora za kufaidika na ushindani.
Hapa tutaangalia mbinu bora unazoweza kutumia kufaidika na ushindani wa moja kw amoja.
1. Jua ni vitu gani unavyofanya kwa ubora sana ambavyo washindani wako hawawezi kufanya kama wewe. Kila biashara ina kitu ambacho ni tofauti na biashara nyingine. Jua kitu hiki na jinsi ya kukitumia vyema ili kuweza kwenda mbele zaidi ya wapinzani wako.
2. Jua ni kitu gani cha ziada alichonacho mpinzani wako. Mpinzani wako ana kitu ambacho wewe huna na hiki kinamwezesha yeye kufanya vizuri kwenye biashara yake. Jua kitu hiko na angalia ni jinsi gani unaweza na wewe kukitumia kwenye biashara yako ili kupata wateja wengi zaidi. Unapochukua kitu chochote hakikisha huigi moja kwamoja, bali tumia ubunifu kuweza kuboresha zaidi kile ambacho umechukua kwa wengine.
3. Jua mapungufu ya mpinzani wako. Kila biashara ina mapungufu yake na ukiweza kuyajua mapungufu ya mpinzani wako unaweza kuyaboresha zaidi kwako. Hivyo wateja wanaokosa kile wanachotaka kwa mpinzani wako watakuwa wateja wazuri sana kwako kama watakuwa na uhakika wa kupata wanachotaka kwako.
4. Ijue vizuri biashara unayoifanya kuliko wengine wote. Unapoijua vizuri biashara unayoifanya inakuwa rahisi kwako kuziona fursa mapema zaidi kabla ya wengine. Kwa kuwa mbele yaw engine inakupa nafasi ya kunufaika zaidi kabla wengine hawajastuka. Jua kila eneo la biashara yako na kila siku angalia ni jinsi gani unavyoweza kuboresha zaidi.
5. Toa huduma bora kabisa kwa wateja. Kama huna chochote cha kuchukua kwa wapinzani wako, au hupati nafasi ya kuwajua vizuri basi una kitu kimoja muhimu cha kufanya. Toa huduma bora kabisa kwa wateja wako. Hakikisha mteja anayekuja kwenye biashara yako anapata huduma bora ambayo hawezi kuipata sehem nyingine yoyote na atakuja tena nakuwaambia na wenzake pia.
Hizi sio zama za kupambana na mshindani wako ili kumuondoa kwenye biashara. Hizi ni zama za wewe kuwekeza kwenye biashara yako zaidi ili kuwa bora na kutoa huduma bora kabisa wka wateja wako. Tumia mbinu hizo hapo juu kujiweke mbele kabisa ya wapinzani wako bila hata ya kuumiza kichwa.
Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.