Moja ya changamoto ambazo zinawazuia watu wengi kuingia kwenye biashara au kukuza biashara zao ni kufikiria ni biashara gani sahihi kwao kufanya.

Watu wengi hupoteza muda mwingi wakitafuta wazo bora kabisa la biashara ambalo litawaletea faida kubwa na mafanikio makubwa pia.

Wafanyabiashara wengine huumia sana pale ambapo wazo lao la biashara haliwaletei matokeo waliyotarajia. Hii huwapelekea kukata tamaa na kuona hawawezi kufikia mafanikio kupitia biashara.

Sasa leo nataka nikupe mbinu moja rahisi sana. Mbinu hiyo ni kwmaba usihangaike sana kutafuta wazo la biashara na pia usiumie sana pale ambapo wazo ulilotegemea halijaleta mafanikio uliyotaka.

Kama unaanza biashara anza na wazo lolote ambalo linawezekana kwenye mazingira uliyopo. Angalia chochote ambacho unaweza kufanya na watu wakakulipa hata kama ni kiasi kidogo. Lengo lako kubwa sio kupata faida kubwa kwenye biashara ya kwanza, hakuna uhakika wa hilo, ila lengo lako ni kujifunz akuhusu biashara hiyo na biashara kwa ujumla. Na elimu bora utakayoipata pale utaweza kuitumia kwenye biashara yoyote utakayofanya baada ya hiyo. Hivyo usipoteze muda kufikiria ni biashara gani bora unayoweza kuanza nayo, mabadiliko yanatokea kila siku hivyo fanya kile ambacho kitakupa elimu nzuri kuhusiana na biashara. Kumbuka hakuna elimu bora kama utakayoipata kwa kufanya mwenyewe, utakapopata hasara utajifunz ani jinsi gani yakukwepa hasara baadae.

Kama tayari upo kwenye biashara ila haifanyi vizuri usipoteze muda wako kulalamika kwamba biashara hailipi ay hutaweza kufikia mafanikio. Badala yake angalia ni kitu gani unachoweza kubadili kwenye biashara hiyo ili iweze kuleta faida. Kumbuka biashara yoyote ambayo unafanya, hata iwe ngumu kiasi gani, kuna wenzako wanaifanya na wanapata faida kubwa. Hivyo angalia ni kitu gani wenzako wanafanya kwa utofauti na wewe ukifanye ili uweze kupata faida. Biashara yako haiwezi kubadilika kama wewe hutobadilika. Kama biashara yako ni ngumu na haikupatii faida nina neno moja la kukuambia, BADILIKA. Ukibadilika na kuanza kuibadili biashara yako utaona mabadiliko kwenyekipato chako pia.

SOMA KITABU; JINSI YA KUFAIDIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA na utajifunza mbinu nzuri sana za kujiandaa na mabadiliko kwenye biashara.

Fanyia kazi mbinu hii ya leo na kesho tukutane hapa kwa mbinu nyingine nzuri.

Kwa ushauri zaidi wa kibiashara piga simu 0717396253.

Kila la kheri.