Kila kitu kwenye maisha kina vitu ambavyo ni muhimu sana ili kiweze kuendelea kuwepo. Kama ilivyo kwetu binadamu, kuna vitu muhimu kwenye miili yetu ambavyo visipokuwepo maisha pia hayawezi kuwepo. Biashara pia ina vitu vyake muhimu sana ambavyo vinahitajika kuwepo na kuwepo kwa kiwango kizuri ili iweze kuendele ana kukuletea faida. Matatizo mengi yanayopelekea biashara nyingi kupata hasara na hata kufa kabisa yanaanzia kwenye vitu hivi vitano vinavyojenga biashara yoyote. Katika makala ya leo tutapata nafasi ya kujifunz akuhusu vitu hivi vitano na jinsi unavyoweza kuvitumia vizuri kwa maendelea ya biashara yako.

Kitu cha kwanza ni kutengeneza na kutoa kitu chenye thamani. Kama hakuna thamani inayotengenezwa au kutolewa basi kw akifupi tunaweza kusema kwamba hakuna biashara. Msingi wa kwanza kabiasa wa biashara yoyote ni kutengeneza na kutoa kitu cha thamani. Thamani hii ya kitu inapimwa kw auwezo wa kitu hiko kuweza kutatua matatizo ya watu wengine na kuboresha maisha yao zaidi. Biashara yoyote ambayo inatoa kitu cha thamani ina nafasi kubwa sana ya kutengeneza faida na kuendelea. Lakini thamani tu haitoshi, inategemea sana na vitu vingine muhimu tunavyoendelea kujadili hapo chini.

Kitu cha pili ni uhitaji wa watu kwa thamani hiyo. Haijalishi unatengeneza na kutoa kitu chenye thamani kubwa kisi gani, kama hakuna watu wanaohitaji kitu hiko basi huna biashara. Biashara inaweza kuwepo pale ambapo unatengeneza na kutoa thamani ambayo pia watu wanaihitaji. Kama unauza miavuli eneo ambalo kwa mwaka mzima hakuna mvua wala jua kazi, hata kama miavuli yako ingekuwa mizuri kiasi gani ni vigumu sana kufanya biashara. Uhitaji wa watu unabadilika kulingana na eneo husika na hata majira husika. Ni muhimu sana kujua jambo hili la pili kabla hujaingia kwenye biashara husika.

Kitu cha tatu ni gharama ambayo watu wapo tayari kulipia kwa thamani unayotoa. Tayari una thamani na kweli watu wanaihitaji swali la msingi ni je wanaweza kuimudu gharama ya thamani unayotoa? Je kipato cha watu uliowalenga kinawawezesha wao kuweza kulipia bidhaa au huduma ya thamani unayotoa? Kama jibu ni ndio basi unayo biashara. Kama jibu ni hapana basi biashara huna na unahitaji kufanya mababiliko makubwa kwenye biashara yako. Uwezo wa watu kuweza kumudu bei ya thamani unayotoa ni kitu muhimu sana kwenye mafanikio ya bishara yako. Hivyo kabla ya kupanga bei ya bidhaa au huduma zako unahitaji kujua soko lako ni lipi na uwezo wao ukoje. Bila ya kufanya utafiti wa aina hii unajitengenezea mazingira ya kushindwa kwenye biashara unayofanya.

Kitu cha nne ni mteja kuridhika. Pamoja na mteja kuiona thamani, kuwa tayari kuipata na kuweza kumudu kuilipia kuna kitu kingine muhimu sana kwa upande wa mteja. Kitu hiki ni kuridhika na thamani uliyompatia. Biashara za zama hizi zimebadilika sana, hufanyi biashra na mtu mara moja tu, bali unahitaji kujenga wateja ambao wataendele akurudi kwenye biashara yako na kuleta watu wao wa karibu pia. Kama utaweza kumshawishi mtu anunue thamani unayotoa, lakini isiweze kutatua matatizo yake, mtu huyu hatorudi tena wkenye biashara hiyo. Hivyo unakuwa umepoteza mteja mmoja. Mbaya zaidi mambo hayaishii hapo, atawaambia watu wake wa karibu jinsi gani hajanufaika na thamani aliyolipia, unakosa wateja wengi zaidi. Na kwa Bahati mbaya zaidi hawa walioambiwa nao wanaendelea kusambaza habari hizi, kwa hali hii muda sio mrefu biashara yako inakuw ana picha mbaya na inapoteza wateja wengi kitu kitakachopelekea biashara hiyo kufa. Hakikisha thamani unayotoa itamridhisha kweli mteja na hapo utaweza kujenga biashara yenye mafanikio.

Kitu cha tano ni kutengeneza faida. Kitu ambacho ulifikiri kingekuwa cha kwanza kabisa kwenye maendeleo ya biashara ndio hiki cha mwisho. Kimekuwa cha mwisho kwa sababu hata umuhimu wake ukilinganisha na hivyo vingine sio mkubwa. Ndio najua unafanya biashara ili upate faida, ila je unaweza kupata faida kama huna wateja? Jukumu lako kubwa kwenye biashara ni kutengeneza wateja waaminifu na hayo mengine ya faida yatafuata. Ukikazana kuangalia faida tu utajikuta unapoteza wateja wengi sana. Baada ya kuhakikisha kwmaba unao wateja na ambao wananufaika na kile unachotoa sasa unakuja kuangalia kitu hiki chabtano, je biashara inapata faida ya kuiwezesha kuendelea kuwepo na kukua zaidi? Kama jibu ni hapana, huna biashara kw amuda mrefu. Kama jibu ni ndio, hongera sana maana unayobiashara itakayoweza kuendelea na kukuletea mafanikio makubwa.

Fanya tathmini kwenye biashara yako kuona ni jinsi gani mambo hayo matano yapo kwenye biashara yako. Na kama kuna sehemu ambayo haijakaa vizuri unahitaji kufanya mabadiliko haraka kabla mambo hayajaendelea kuwa mabaya. Kama utakwamba kwenye mabadiliko unayotaka kufanya, tunaweza kuwasiliana kwa mawasiliano yaliyopo hapo chini ili tuone ni jinsi gani tunaweza kusaidiana. Kila la kheri.