Katika moja ya makala zilizopita hapa kwenye KONA YA MJASIRIAMALI tuliwahi kujadili lengo kuu la biashara ni nini. Kama hukumbuki au hukupata nafasi ya kusoma makala ile tuliona kwamba lengo kuu la biashara sio kupata faida kama watu wengi wanavyofikiria. Bali lengo kuu la biashara ni kutengeneza wateja. Kama biashara itaweza kutengeneza wateja wanaoiamini biashara hiyo, faida ni lazima itafuata.
Wewe kama mjasiriamali unahitaji kuweka nguvu zako nyingi kwenye kutengeneza wateja ambao wanaiamini biashara yako na wanakuamini wewe pia. Ukiwekeza nguvu nyingi kwenye kupata faida unaweza kufanya mambo ambayo yatawafanya wateja wakose imani na wewe na wasirudi tena kwenye biashara yako. Mteja ni muhimu sana kwenye biashara yako na lengo lako kubwa ni kutengeneza mteja atakayefanya biashara na wewe kwa muda mrefu na kuwa tayari kuitangaza biashara yako kwa wengine pia.
Leo tutaangalia mteja wa kwanza na wa muhimu sana kwenye biashara yako. Wajasiriamali na wafanyabiashara wengi huangalia wateja wanaokuja kwenye biashara zao na kukazana kuwapa huduma nzuri ili warudi tena na hata kuwaambia wenzao. Lakini wanasahau mteja wa kwanza na wa muhimu sana kwenye biashara yeyote ambaye ndio anatakiwa kuwa wa kwanza kuridhishwa na biashara unayoifanya.
Mteja tunayemzungumzia hapa ni mfanyakazi au wafanyakazi wako. Kama biashara yako imeajiri wafanyakazi wako ni wateja wa kwanza kwenye biashara yako. Hawa ndio unaotakiwa kuwaridhisha kwanza kabla hata mteja wa kununua hajafika kwenye biashara yako. Hawa ndio wanaotakiwa kuwa watu wa kwanza kufurahia na kuwa na shauku kubwa kwa bidhaa au huduma unayotoa. Kwa kuwa na wafanyakazi wanaofurahia na kupenda kazi wanayofanya watavutia wateja wengi zaidi na watakuwa tayari kutangaza biashara yako hata kama hawapo sehemu ya kazi.
Kama wafanyakazi watakuwa hawapendi biashara unayofanya, hawatakuwa na hamasa kubwa nah ii itaonekana hata kwa wateja. Kwa hali hii wateja watapata huduma mbovu sana na hawatafurahia kufanya biashara na wewe.
Tunaposema wafanyakazi wako ndio wateja wako wa kwanza tunamaanisha wafanyakazi wote na sio wale wanaokutana na wateja moja kwa moja. Hata kama mfanyakazi hakutani uso kwa uso na mteja, kumbuka kwmaba kazi anayoifanya pale ina mchango kwa mteja. Hivyo anapoifanya kazi yake vizuri anaongeza thamani ya biashara yako na kumridhisha mteja na hatimaye mteja anaipenda biashara yako na kuwa mteja wa kudumu.
Mfanyakazi anayefanya kazi kwenye biashara yako kwa sababu yeye anaangalia ni kipi unamlipa ni mfanyakazi hatari sana. Mfanyakazi ambaye hawezi kujituma, mpaka wewe umwambie ni kitu gani cha kufanya ataishuhudia biashara yako ikifa bila ya kuchukua hatua yoyote iliyopo ndani ya uwezo wake. Mfanyakazi wako anatakiwa kuwa mteja wako wa kwanza kabisa, anayeamini kwenye biashara unayofanya na anayekuamini wewe pia.
Unahitaji kuitangaza biashara yako kwa wafanyakazi wako kwanza kabla hata hujaitangaza kwa wateja wengine. Ni lazima kila mfanyakazi ajue ni kazi gani ameajiriwa kufanya na anategemewa kuzalisha nini. Ni lazima kila mfanyakazi ajue kwamba huduma bora kwa mteja ndio lengo la biashara hiyo na hivyo ajue kitengo chake kinahusiana vipi na kutoa huduma bora kwa wateja. Pia ni lazima kila mfanyakazi ajue kwamba kuendelea kuwepo kwa biashara kutatokana na juhudi zao katika kazi zao wanazofanya.
Kwa kufanya hivi utakuwa na timu nzuri ya wafanyakazi ambao wanapenda kile wanachofanya na wapo tayari kutoa huduma bora kabisa kwa mteja atakayefika kwenye biashara yako. Pia watakuwa tayari kuitangaza biashara yako popote pale watakapokuwepo hata kama ni nje ya kazi.
Anza juhudi hizi za kuhakikisha wateja wako wa kwanza kabisa ni wafanyakazi wako. Wiki ijayo tutangalia vigezo unavyoweza kutumia wakati wa kuajiri ili kupata wafanyakazi ambao ni bora kwa biashara yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.