Kama umekuwa mfuatiliaji mzuri wa mafunzo ninayotoa utakuwa unaelewa kwamba tunajaribu kujenga utamaduni mpya kwenye biashara. Na utamaduni huu ni ule wa kufanya biashara kirafiki na kuwa na wateja ambao wanakuamini na kukutegemea.
Mbinu nyingi tunazoshirikishana ni za kuweza kumfanya mteja awe rafiki yako na afurahie kufanya biashara na wewe. Hatutaki kufanya biashara ya kukutana na mteja mara moja halafu baada ya hapo asirudi tena. Hii ilikuwa biashara ya zamani na kwa sasa haiwezi kukulipa tena.
SOMA; Siri Ya Kutambua Kampuni Nzuri Ya Kuwekeza Ili Upate Faida.
Katika kujenga uhusiano mzuri na wateja wako ili waendelee kukuamini unahitaji kuwa makini sana kwenye mabadiliko yako ya bei. Kama biashara unayofanya sio ya uchuuzi, yaani unauza bidhaa au huduma zako mwenyewe, basi unapohitaji kubadili bei kuwa makini sana.
Jambo moja la kuzingatia kwenye bei za bidhaa au huduma unazotengeneza mwenyewe ni kwamba kama utahitaji kubadili bei, basi bei iwe inaongezeka na sio kupungua.
SOMA; Huyu Ni Mjasiriamali Mwenye Hamasa Kubwa sana. Unaweza kujifunza kila kitu kutoka kwake.
Kama umetoa bidhaa tuseme labda ni kitabu, halafu ukawa unakiuza kwa tsh elfu kumi, tayari una wateja wako ambao wanakuamini na watanunua kitabu hiki, tena haraka sana. Ikifika baadae ukapunguza bei ya kitabu hiki na ikawa tsh elfu tano, huenda utapata wateja wengine wengi ila wale walionunua mwanzo wataona kama waliibiwa. Wanaweza wasikuambie lakini watakuwa na wasi wasi na wewe, hata utakapotoa bidhaa nyingine hawatakuwa tayari kununua kwa haraka kwa sababu wanajua baadae bei inaweza kupungua.
Lakini unapoongeza bei, kwa mfano kitabu kikapanda na kuwa tsh elfu kumi na tano, wale walionunua mwanzo watajisikia kama walipata upendeleo na hata pale utakapotoa bidhaa nyingine watakimbilia kununua haraka ili wasikose nafasi hiyo ya kupata kwa bei ndogo.
SOMA; Unajaribu Kumdanganya Nani?
Mbinu hii inatumika vizuri kwa bidhaa au huduma ambazo unatengeneza mwenyewe au unaweza kuzisimamia mwenywe. Ila kama unanunua kwa jumla na kuuza kwa reja reja huna umiliki mkubwa kwenye bei.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.