Katika makala ya wiki iliyopita tuliona mteja wa kwanza na wa muhimu sana kwenye biashara yako. Tulijifunza kwmaba mteja huyu ni muhimu sana na ndiye wa kwanza kuridhishwa kabla hata mteja mwingine hajafika kwenye biashara yako. Mteja huyu ni mfanyakazi wako au msaidizi katika biashara yako. Tuliona kwamba msaidizi yeyote katika biashara yako, haijalishi ana majukumu gani, jukumu lake la kwanza kabisa ni kutoa huduma bora kabisa kwa mteja anayefika kwenye biashara yako.

Ili kugakikisha unapata wafanyakazi walio bora sana kwenye biashara yako unahitaji kuwa makini sana tangu mwazo wakati ambapo unaajiri. Kwa sababu hakuna njia nyingine ambayo wafanyakazi watakuja wkenye biashara yako, ni muhimu kujua mambo ya kuzingatia wakati unaajiri ili uweze kupata wafanyakazi ambao wana uwezo mkubwa wa kukuza na kuendeleza biashara yako.

Yafuatayo ni mambo muhimu sana ya kuzingatia wakati unaajiri ili uweze kupata wafanyakazi ambao ni borab sana kwenye biashara yako.

Ajiri uwezo na sio elimu.

Njia rahisi ambayo watu wengi hutumia kuajiri ni kigezo cha elimu. Kwamba kwa sababu mtu ana elimu ya chuo kikuu na amesomea kitu fulani basi atakufaa kwenye biashara yako. Elimu ni kigezo muhimu sana lakini uwezo binafsi wa mtu ni kigezo muhimu zaidi. Kuna watu wengi ambao wana elimu nzuri lakini uwezo wao binafsi ni mdogo sana. Wewe unahitaji mtu ambaye anaweza kufikiri na kutumia rasilimali zilizopo kwenye biashara yako kuikuza zaidi. Unahitaji mtu ambaye anaweza kukushauri vizuri kuhusiana na kile anachofanya. Na mtu huyu ni mtu mwenye uwezo mkubwa na sio tu ufaulu wa darasani. Kama unafanya usaili wakati wa kuajiri hakikisha una mua mtu vizuri na kile anachoweza kufanya.

Ajiri mtu anayependa biashara unayofanya, au kazi unayomwajiri.

Kama mtu hapendi kitu ambacho anafanya, hakuna msaada mkubwa kwake, hawezi kufikia mafanikio kupitia kitu hiko. Kuwa makini sana usije ukaajiri mtu ambaye hapendi kufanya kile ambacho umemwajiri kufanya au hapendi kabisa aina ya biashara unayofanya. Mtu huyu atakuwa mzigo mkubwa sana kwako na kwa biashara yako. Wakati wewe unakazana kukuza biashara yako, yeye atakuwa anairudisha nyuma bila hata ya wewe kujua. Unapopata mtu anayependa anachofanya, anakuwa mtu wa kujituma na kufanya akzi yake wka ubora wa hali ya juu. Unapopata mtu ambaye hapendi anachofanya, anakuwa mtu wa kusukumwa na utakuwa mzigo mkubwa kwako na kwa biashara yako.

Ajiri mtu anayeweza kujiongoza mwenyewe.

Katika wafanyakazi unaoajiri hakikisha wanawez akujiongoza wenyewe. Hakikisha mtu ukishampatia majukumu yake anaweza kuyatekeleza kwa wakati bila hata ya kuwa na usimamizi mkubwa. Wewe huna muda wa kuanza kumuangalia kila mfanyakazi anafanya nini na kwa wakati gani. Wewe una majukumu makubwa sana ya kukuza biashara yako na ndio maana umetafuta watu wa kukusaidia. Sasa kama watu hawa watahitaji kusimamiwa kila wakati, itakuwa haina maana ya kuwa na msaidizi.

Epuka kuajiri watu ambao una uhusiano nao wa karibu.

Moja ya changamoto kubwa ambayo watu wanaipata ni pale ambapo wanaajiri watu ambao wana uhusiano nao wa karibu kama ndugu, jamaa au rafiki. Epuka kufanya hivi kwa sababu watu hawa wanaweza wasiwe waelewa sana na wakakurudisha nyuma. Unaweza kuwa unakazana kukuza biashara yako huku mwenzako anafanya uzembe kwa sababu anajua huwezi kumchukulia hatua kubwa. Kama itakubidi kuajiri watu ambao una uhusiano nao wa karibu, basi hakikisha wanajua kuanzia mwanzo kwamba kwenye biashara hakutakuwa na uhusiano wa aina hiyo na kama watashindwa kutimiza majukumu yao, watawajibishwa kama wanavyowajibishwa watu wengine. Kwa kufanya hivi utawafanya wawe makini na kazi zao na wafanye kazi kwa ubora unaohitaji ili biashara yako kuendelea.

Tumia vigezo hivi katika kuajiri ili uweze kupata wafanyakazi bora watakaoiwezesha biashara yako kukua na kuendelea zaidi. Wiki ijayo tutamalizia eneo hili la mteja wa kwanza kwenye biashara yako kwa kuangalia njia unazoweza kutumia kuwapa motisha wafanyakazi wako ili waweze kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.