Katika makala mbili zilizopita tumekuwa tunajadili kuhusu mteja muhimu na wa kwanza kwenye biashara yako. Tuliona mteja huyu ni mfanyakazi au wafanyakazi wako uliowaajiri kwenye biashara yako. Hawa ni watu ambao wanatakiwa kuwa washabiki wa kwanza kabisa wa kile amabcho unafanya. Wanatakiwa kuwa wanakipenda na wapo tayari kuwashawishi wengine wajihusishe na biashara hiyo. Pia tuliona vigezo muhimu vya kutumia wakati wa kuajiri. Baadhi ya vigezo hivyo ni uwezo wa mtu, mtazamo wake na utayari wake wa kujituma.

Katika makala ya leo tutajadili njia unazoweza kutumia kuwahamasisha wafanyakazi wako ili waweze kuwa na uzalishaji mkubwa kwenye biashara yako. Hitoshi tu kuwa na wafanyakazi wenye uwezo mkubwa na wanaopenda kile wanachofanya, wafanyakazi wanahitaji kuhamasishwa ili waweze kutoa kile kilichopo ndani yao.

Kinyume na wengi wanavyoamini, fedha sio kitu muhimu sana kwenye kuwahamasisha watu kufanya kazi. Kama unafikiri kwamba watu wakilipwa mshahara mkubwa basi watakuwa na uzalishaji mkubwa unakosea sana. Kama watu hawana hamasa kufanya kazi, ya kuwa wabunifu, mshahara mkubwa hauwezi kuwaletea hamasa hiyo. Je ni vitu gani ambavyo unaweza kufanya na ukaongeza hamasa ya wafanyakazi wako? Karibu ujifunze hapa.

Wafanyakazi wanahitaji maana. Mtu anapoona maana kwenye kile anachofanya anasukumwa kukifanya kwa ubora zaidi na kuweka ubunifu mkubwa. Mfanye mfanyakazi aone kwamba kile anachokifanya ni sehemu ya maisha yake na kina maana kubwa kwake na kwa wale ambao wanakwenda kukitumia. Kwa kuiona maan hii wafanyakazi watakuwa tayari kuweka juhudi kubwa ili kuboresha zaidi.

Biashara yako inahitaji kuwa na maono(vision) na kila mfanyakazi anatakiwa kuyajua maono hayo na jinsi gani yanahusika na kazi anayoifanya. Kwa mfano kama unafanya biashara ya mgahawa, maono yako yanaweza kuwa kutoa huduma boras ana za vyakula kwa watu wote wenye uhitaji wa chakula. Maono haya ndio yanayotakiwa kuendesha biashara yako. Kila jambo linalofanyika kwenye biashara yako lazima liwe linasaidia kufikia maono hayo. Ni muhimu kila mfanyakazi ajue maono hayo na pia ajue yanahusika vipi na eneo lake la kazi. Kama mfanyakazi ana jukumu la kufanya usafi anatakiwa kujua kwmaba ili huduma ya chakula iwe bora basi usafi ni sehemu muhimu sana. Hakuna mtu anayependa kula sehemu ambayo ni chafu. Hivyo yeye kufanya usafi vizuri kunachangia huduma ya chakula kuwa boras ana na hivyo biashara kukua. Kwa kulijua hili mfanyakazi atakuwa tayari kwenda hatua ya ziada ili kufikia maono ya biashara.

Mpe mfanyakazi uhuru wa kupangilia kazi zake. Binadamu wote wanapenda uhuru na kuona kwamba maamuzi muhimu wanafanya wao wenyewe. Toa uhuru huu kwa wafanyakazi wako, waweze kujipangia kazi zao wenyewe. Unachotakiw akufanya wewe ni kumkabidhi majukumu kisha kumwambia apangilie kazi zake ili kuweza kutekeleza majukumu yake. Au unaweza kusaidiana naye kupangilia kazi zake. Kwa njia hii mfanyakazi atahamasika kufanya kazi kwa bidii ili aweze kukamilsiha majukumu yake. Lakini kama utampangia kila kitu cha kufanya na wakati huo huo kumkatisha na kumpa kazi nyingine, utamfanya aone kama anatumikishwa na hivyo hamasa yote ya kazi inaisha.

Thamini mchango wa kila mfanyakazi. Kila mtu anapend akuonekana ni muhimu, na hata wafanyakazi wako pia wanapenda kuonekana ni muhimu hasa kwenye kazi wanazofanya. Tambua mchango wa wafanyakazi kwako katika ukuaji wa biashara yako. Kama mtu amefanya jambo zuri na ambalo limewezesha biashara kukua, mpatie zawadi. Hii itawafanya wengine nao wafanye kwa juhudi ili nao wapewe zawadi. Zawadi sio lazima iwe kubwa ila kile kitendo cha kukubalika na kutunukiwa zawadi ndio muhimu sana kwa mfanyakazi.

Haya ni mambo muhimu unayoweza kuyafanya sasa kwenye biashara yako na ukawahamasisha sana wafanyakazi wako kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Anza kuyaweka hayo kwenye biashara yako na baada ya muda utaona matunda mazuri. Kila la kheri.

TUPO PAMOJA.