Wahenga walisema kwamba unaweza kumlazimisha farasi kwenda mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji. Kwa upande wa biashara, kauli hii sio kweli hata kidogo.
Kwenye biashara unaweza kumlazimisha farasi kwenda mtoni na pia ukamlazimisha kunywa maji. Na wala hutumii nguvu kubwa sana, yaani ukishamfikisha karibu na maji tu yeye mwenyewe akayakimbilia. Hujui unawezaje kufanya hivyo? Utajifunza hapa leo.
SOMA; Dalili Kwamba Unaweza Kufikia Mafanikio Makubwa.
Kabla hujampeleka farasi mtoni, kwanza mpe pumba ya kutosha, halafu pumba hiyo changanya na chumvi. Pumba ni chakula kitamu sana kwa farasi, lakini pia inaleta kiu sana. Na chumvi pia inaongeza ladha lakini pia inazidisha kiu. Sasa utakapomfikisha farasi huyu mtoni atakimbia na kuanza kuyafakamia maji, atayanywa haraka sana.
Sasa unatumiaje hali hii kwenye biashara yako? Hakikisha mteja wako anakuwa na shauku kubwa ya kupata kile unachomuuzia kabla hata hujajaribu kumuuzia. Hapa ndio pale ambapo unalijua tatizo la mteja wako na una bidhaa au huduma ambayo itamtatulia tatizo lake. Badala ya kumweleza ni jinsi gani bidhaa au huduma yako ina ubora, mwambie ni jinsi gani itamsaidia kuondokana na tatizo lake na atakuwa na shauku kubwa ya kuitumia bidhaa/huduma hiyo.
SOMA; Fanya Tukio Hili La Kihistoria Ambalo Litakupa Uhuru Uliopoteza.
Na kama itampatia majibu aliyokuwa anategemea, unajua ni nini kitatokea? Atakuwa mteja wako mzuri sana na atamwambia kila mwenye tatizo kama lake aje kwako maana atapata suluhishi. Hivi kuna njia bora ya kufanya biashara zaidi ya hii kweli? Rahisi na haihitaji uwe na stashahada au shahada yoyote, unahitaji kuijua biashara yako vizuri na matatizo ya mteja wako inayokwenda kutatua.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.