Huwa napata nafasi ya kukutana na kuwasiliana na wajasiriamali na wafanyabiashara mbalimbali. Na kikubwa nilichojifunza ni kwamba kwanza, watu wanakutafuta pale ambapo biashara imeshafikia hali ngumu sana kiasi kwamba inahitaji nguvu kubwa sana kuirudisha kwenye mstari. Na pili, watu wengi hawajui sababu hasa ya kushindwa kw abiashara zao, wanakuwa wana sababu nyingi ila hawajui sababu ya kweli ya biashara zao kushindwa.

Kutokujua sababu halisi ya biashara kushindwa, kunawafanya wajasiriamali na wafanyabiashara wengi kurudia makosa yale yale ambayo yamewaingiza kwenye matatizo na hivyo kushindwa tena. Kwenye makala ya leo tutajadili sababu halisi ya biashara kushindwa na ni jinsi gani unavyoweza kuepuka biashara yako isiingie kwenye mkondo huo. Kama wewe ni mjasiriamali au mfanyabiashara jifunze sana hapa kwani ndio utakapopata ukombozi wa biashara yako.

Ukimuuliza mtu ambaye biashara yake inashindwa, kwa nini inashindwa atakupa kila aina ya jibu linalowezekana duniani. Kuna ambao watakuambia hali ya uchumi imekuwa ngumu, watu hawana fedha na hivyo hawawezi kununua. Kuna ambao watakuambia wafanyakazi wao hawajitumi au sio waaminifu na hivyo kuwasababishia hasara na kupoteza wateja. Wengine watasema kwmaba biashara yao ipo kwenye eneo ambalo sio zuri, ipo nje ya mji au mkoani ambapo watu sio wengi kama mjini. Kuna ambao watakuambia fedha ndio tatizo, mtaji ni mdogo na umeshindwa kuisimamisha biashara.

Kwa kifupi utapata majibu ya kila aina ila katika majibu yote hayo, hakuna lile jibu halisi. Hayo mengi yanayotajwa ni dalili za nje tu za tatizo halisi la biashara. Kujaribu kutatua dalili hizo hakuondoi tatizo la msingi. Ndio maana mtu anyefikiria tatizo la biashara yake ni fedha, anapokwend akukopa fedha na kuiweka kwenye biashara anajikuta anaongeza kupata hasara kubwa zaidi. Mtu anayefikiri eneo alilopo ndio linamzuia kufanikiwa kwenye biashara, akihama na kwenda kwenye eneo jingine bado anaona changamoto ni nyingi kwenye biashara yake.

Kwa haya yote basi, tatizo halisi la biashara kushindwa ni nini? Tatizo halisi na ambalo ni kubwa sana linaanzia kwenye muundo wenyewe wa biashara. Tatizo linaanza na mtazamo wa wewe mfanyabiashara mwenyewe, muundo wa ndani wa biashara na usimamizi ulionao kwenye biashara yako.

Katika mtazamo wako wewe mfanyabiashara, kama unaamini unaweza kufanikiwa kwenye biashara unayofanya, utaweka juhudi na hata ukikutana na changamoto hutokata tama. Ila kama unaamini wewe ni wa kushindwa, unapokutana na changamoto ya kawaida kwenye baishara unakubali kwamba wewe huwezi na hivyo kutangaza kushindwa. Jinsi unavyoichukulia biashara yako ndivyo utakavyoweka juhudi za kuikuza au kuibomoa kabisa.

Katika muundo wa ndani wa biashara hapa ndio muhimu zaidi. Watu wengi wamekuwa wakiingia wkenye biashara kwa sababu tu wamesikia biashara hiyo inalipa au kwa sababu wanaona watu wengi wanafanya biashara hiyo. Ila hawakai chini na kuijua vizuri biashara wanayoifanya, kujua mazingira yanayowazunguka na jinsi wanavyoweza kuyatumia kuboresha baishara zao. Kama upo kwenye eneo ambalo ni la kijijini huwezi kuweka biashara uliyoiona mjini na ukategemea ikuletee faida. Unatakiwa kujifunza ni jinsi gani unaweza kuyatumia mazingira ya kijijini ulipo, kukuza biashara yako ambayo umeona ina uhutaji. Ni lazima uwe na muundo wako wa biashara unaoendana na biashara unayofanya, eneo ulipo na wateja ulionao.

Katika usimamizi wa biashara hapa pia kuna changamoto kubwa sana inayosababisha wengi kushindwa. Kama biashara imekosa usimamizi mzuri, ni lazima itakufa, hata kama utalalamikia mazingira yako kiasi gani. Usimamizi mzuri na biashara yako utakufanya uweze kuona dalili za mwanzo kabisa za kushindwa kwa biashara yako na hivyo kuweza kuchukua hatua mapema kabla hali haijawa mbaya. Kama hali ya uchumi imebadilika, unaweza kujipanga vizuri na kuona unatumiaje hali hiyo kukuza biashara yako zaidi. Hata uchumi ukiwa mbaya kiasi gani, kuna biashara ambazo zinakua kwneye kipindi hiko, kwa nini isiwe ya kwako?

Biashara yako itashindwa kama utakuwa na mtazamo hasi kuhusu biashara, utakuwa na muundo mbovu wa biashara yako na kama hutakuwa na usimamizi mzuri. Haya mengine yote ya hali ya uchumi, mazingira, wafanyakazi na hata wateja yanatibika kwa kuanza na matatizo hayo matatu muhimu. Kuwa na mtizamo sahihi wa biashara yako, tengeneza muundo unaoendana na biashara yako, mazingira yako na wateja wako na pia kuwa na usimamizi mzuri kwenye biashara yako. Kama utakuwa na tatizo linalohitaji ushauri zaidi kwenye biashara yako tuwasiliane.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.